MKASA WA PILI -Sehemu ya 4
Inaendelea.............
Safari ya kutoka Geita mjini kuelekea Mwanza ilianza,nilifika Mwanza mida ya saa 9 alasiri,kiukweli nilimshukuru sana Mungu maana niliona ilikuwa ni bahati mimi kupata taarifa zile za kazi haramu aliyokuwa akiifanya jamaa!.Baada ya kuwa nimefika hapo nyumbani kuna kiasi kidogo cha pesa nilimpatia mama,sikutaka kupoteza muda nilimuomba mama anieleze yule mtoto wa mama alikuwa kamueleza nini kuhusiana na hiyo kazi?mama aliniambia kuna namba ya simu alimwachia na akasema nitakapo rudi nihakikishe namtafuta!,Kumbe siku ambayo mimi nilimpigia simu mama,huyo mtoto wa mama mdogo alikuwa kamaliza kama siku mbili toka kaondoka kurudi Kwao Bunda.Iilibidi nimtafute dogo akaniambia kama ninaweza kwenda Bunda siku hiyo au kesho niende,kwani kuongelea ishu kama ile kwenye simu nisingeweza kuielewa vizuri,basi kulipo kucha mrume ndago nilimueleza mama kwamba inabidi nielekee Bunda kwa mama mdogo nikaonane na dogo ili nikaone kama hiyo kazi inalipa tukaifanye ili niweze kupata kipato.
Kauli ya mama yangu mara zote ilikuwa ni "Kuwa makini".
Basi nilielekea stendi ya buzuruga kwa ajili kukata tikiti kwa ajili ya safari ya kuelekea wilaya ya Bunda,mida ya saa 7 mchana nilikuwa tayari nishafika mji wa Bunda,ni mji uliyokuwa umechangamka,kulikuwa na pilikapilika za hapa na pale zilizochochewa na watafutaji,baada ya muda dogo alifika kunichukua tukaanza kuelekea nyumbani kwao,tulikuwa tukipiga stori za hapa na pale hasa ukizingatia mimi na huyo dogo tulikuwa hatukuonana muda mrefu,dogo alikuwa akinikubali sana na ndiyo maana anasema ilibidi aje Mwanza kunitafuta maana alisikia tayari nishamaliza shule,hivyo nilikuwa tu nyumbani bila kazi, hakujua kwa wakati ule kama nilikuwa nimeenda Geita.Basi baada ya kuwa tulifika hapo nyumbani kwa mama mdogo,niliwakuta ndugu zangu upande wa mama mdogo,tulisalimiana nao na kisha nilimsalimia na mama mdogo,stori za hapa na pale ziliendelea hasa ukizingatia ulikuwa umepita muda mrefu bila kuonana na hao ndugu zangu,baada ya kupita muda kidogo,yule dogo tukaelekea mitaa flani ya shule ya msingi Miembeni,japo pia mama mdogo mitaa aliyokuwa akikaa ni huko huko Miembeni lakini haikuwa jirani na shule,Kuna nyumba moja tuliingia tukamkuta jamaa mmoja alikuwa akiongea kiswahili chenye rafudhi ya Kikenya,ilitosha kuonyesha kabisa yule jamaa hakuwa mtanzania bali alikuwa Mkenya!.Mazungumzo yakaanza pale na yule dogo alinitambulisha kwa jamaa kuwa mimi ni mtoto wa mama yake mkubwa.Jamaa pia alijitambulisha kuwa anaitwa Gachui n hapo Bunda alikuwa kaja kwa kazi moja tu,akaniuliza "bila shaka dogo atakuwa amekwambia".
Mimi nikasema "hapana kaka sijaambiwa kitu chochote".
Alimgeukia dogo na kumuuliza "Mbona hujamwambia jamaa yako".
Dogo alimjibu "Mimi sikutaka kumuelezea kitu bro niliona nije kwako maana ndiye unaelewa namna mchongo ulivyo na bila shaka ataelewa zaidi kuliko ningemueleza mimi".
Yule Mkenya akamwambia "Nyie watanzania mko na maneno mingi sana!".
Yule jamaa aliongea rafudhi ya Kiswahili cha Kikenya ambacho kilimfanya maneno mengi kutoyatamka kwa ufasaha.Basi jamaa akaanza kutuelezea tena ule mchongo namna ulivyo,kwamba kuna kampuni huko Kenya ambayo walikuwa wanahusika zaidi na pesa za zamani,zikiwemo pesa za sarafu na noti!,sasa akawa anasema kwamba,amekuja Tanzania kama wakala wa hiyo kampuni na lengo la yeye kuwa pale ni kuitafuta sarafu ya shilingi 100 ya mwaka 1993,jamaa alikuwa anasema hiyo sarafu ilikuwa inahitajika kama vile Almasi!.Jamaa akatuambia hiyo sarafu ingepatikana,basi tulikuwa tunapewa Tsh milioni 100.Kiukweli niliona kama maigizo lakini ndiyo maelezo jamaa aliyotupatia,nilimuuliza maswali kadhaa ya kujiridhisha ili kwamba atuhakikishie kama kweli tukipata hiyo sarafu tungelipwa na hiyo kampuni hizo hela au ilikuwa janja janja tu za matapeli wa mjini?.
Jamaa alituambia endapo tungepata hiyo sarafu,kabla ya mambo yote zingewekwa hizo pesa kwenye akaunti na tukishajiridhisha ndiyo nasi tungeitoa hiyo sarafu.Maelezo yake kidogo kama yaliniingia akilini na jamaa akasema yeye si tapeli maana alikuwa katoka Kenya kuja Tanzania kufanya hiyo kazi tu,baada ya kuondoka pale kwa huyo mkenya nilihitaji kufahamu siri ya ile sarafu ya 100 ya mwaka 1993 ilikuwa ni nini?.
Tulipofika nyumbani nilijaribu kumshirikisha mama mdogo naye akaniambia "Tayari mwenzio alishaniambia mwanangu".
Ndipo nilimuuliza siri ya ile sarafu ya ilikuwa ni nini?,mama mdogo aliniambia siri ya hiyo hela kiukweli haijui ila anachofahamu hiyo sarafu ya 100 ya mwaka 1993 kipindi fulani waliitumia kama dawa!.
Mama mdogo alisema "miaka fulani ulikuwa ukiumwa na nyoka au ng'e au kitu chochote chenye sumu ulikuwa ukichanja na wembe yale maeneo ulipong'atwa na ukiiweka ile shilingi 100 basi ilikuwa ikinata kama sumaku na kunyonya sumu yote,na endapo sumu ingeisha mwilini basi ile sarafu ilianguka chini yenyewe ikiashiria kwamba sumu imeisha!".
Akaendelea kusema "miaka ya karibuni hizo sarafu zimeadimika sana,pia zilikuwaga nzito sana tofauti na hizi za sasa,ulikuwa ukiichukua sarafu ile ukilinganisha na sarafu ya sasa hazilingani kabisa kwa uzito".
Basi baada ya maelezo yale ya mama mdogo kiukweli nilianza kupata mwanga,Mama mdogo alituambia hizo hela za zamani kuna mzee anamfahamu aliwahi kupata shilingi 10 za zamani zilikuwa zinatafutwa na yeye alikuwa nazo 2,hivyo yule mzee alilipwa milioni 10,Hivyo mama mdogo alituelekeza kwa huyo mzee twende tukamuulize labda angetusaidia kupata angalau mwanga kidogo!.Basi mimi na yule dogo tulielekea maeneo fulani panaitwa Balili,kiongozi wangu alikuwa yule dogo maana mimi mitaa nilikuwa siifahamu,Kweli baada ya kuwa tumefika ile mitaa ambayo mama mdogo alimpatia yule dogo maelekezo,tulimuulizia yule mzee kwenye hayo maeneo na tukaelekezwa mpaka kwake,tulipofika hapo kwenye huo mji wake tulimkuta mzee mmoja wa makamo tukamsalimia,dogo akajitambulisha na akamueleza sisi ni watoto wa mama.......,Yule mzee alikuwa akimfahamu vizuri mama mdogo,hivyo haikuwa taabu sana kujieleza,ilibidi nianze kufunguka,Yule mzee akatuambia hiyo nyumba anayokaa yeye na familia yake waliijenga baada ya kupewa pesa kiasi cha shilingi milioni 10 miaka kadhaa nyuma iliyopita kwani walitokea watu fulani kipindi hicho wakawa wanatafuta shilingi 10 zamani na kwa bahati nzuri yule mzee anaseman alikuwa nazo 2 ndiyo kupewa hiyo milioni 10!.
Yule mzee alitupatia maelekezo kama ya Mama mdogo aliyotupatia kuhusu hiyo sarafu ya 100 na akasema "si nyinyi peke yenu mnaoitafuta bali kuna watu kadhaa nimekutana nao wakitafuta hiyo shilingi 100".
Basi nikajisemea "kumbe hii ishu iko very serious!".
Yule Mzee alitushauri ya kwamba kwa hapo mjini tutapoteza muda hatutaambulia chochote,mzee akasema "nendeni vijijini na ikiwezekana kwa waganga wa kienyeji maana wale huwa wanakuwaga na kila pesa ya miaka ya zamani".
Hilo wazo la mzee lilituingia akilini,Yule mzee akatuambia twende wilaya ya Musoma vijijini sehemu moja inaitwa Bukima,akatuelekeza kwa Mganga mmoja ambaye alikuwa ndugu yake,kwamba tukifika hapo Bukima center tuulizie hilo jina alilokuwa ametutajia,tutakapofika kwa huyo mganga akituuliza tumtaje huyo mzee kwamba ndiye aliyetuagiza hapo kwake na tumueleze shida yetu!.Basi tulirudi nyumbani kujipanga kwa ajili ya safari ya kuelekea Bukima.
Itaendelea................