Mikoa yote kutumia mfumo wa e-Ardhi ifikapo Juni 2027

Mikoa yote kutumia mfumo wa e-Ardhi ifikapo Juni 2027

Zack Abdul

JF-Expert Member
Joined
Mar 9, 2026
Posts
1,194
Reaction score
911
Na Mwandishi Wetu

Serikali imepanga kuhakikisha mikoa yote nchini inatumia mfumo wa kidijitali wa usimamizi na umilikishaji wa ardhi, e-Ardhi, ifikapo Juni 2027.

Hatua hiyo inayolenga kurahisisha upatikanaji wa hati za ardhi na kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhandisi Anthony Sanga, amesema mfumo huo umeanza kutumika katika mikoa 17 na Serikali inaendelea na juhudi za kuusambaza katika mikoa iliyosalia.

Akizungumzia mafanikio na maboresho yanayofanywa na wizara hiyo kuelekea uzinduzi wa majengo ya ofisi za wizara na taasisi za Serikali pamoja na barabara za lami katika Mji wa Serikali wa Mtumba, jijini Dodoma, unaotarajiwa kufanyika Oktoba 30, 2026, Sanga amesema mfumo huo umetengenezwa kwa kutumia utaalamu wa ndani.

Amesema e-Ardhi umerahisisha shughuli mbalimbali za sekta ya ardhi, zikiwamo umilikishaji wa ardhi na utoaji wa hati, ambazo sasa zinaweza kutolewa kwa njia ya kidijitali na kuchapishwa kwa urahisi.

Ameeleza kuwa mfumo huo ni sehemu ya maboresho yanayolenga kupunguza changamoto za kiutendaji zilizokuwapo katika taratibu za awali za utoaji wa huduma za ardhi.

“Mpaka sasa mfumo huu umeenea katika mikoa 17, na tuna lengo la kuhakikisha ifikapo Juni mwaka ujao mikoa yote nchini inakuwa na mfumo huu unaofanya kazi kidijitali,” amesema Sanga.

Ameongeza kuwa Serikali inaendelea kuboresha upimaji wa maeneo na umilikishaji wa ardhi ili kuhakikisha wananchi wanapata haki zao na huduma kwa urahisi zaidi.
 
Back
Top Bottom