SoC04 Mikopo kwa wanafunzi wa vyuo vya kati na vyuo vikuu itolewe kwa wote watakaoomba

SoC04 Mikopo kwa wanafunzi wa vyuo vya kati na vyuo vikuu itolewe kwa wote watakaoomba

Tanzania Tuitakayo competition threads

Tukuza hospitality

JF-Expert Member
Joined
Jul 30, 2022
Posts
321
Reaction score
691
Miaka ya nyuma, yaani 1995 na kurudi nyuma, elimu ya vyuo vya kati na vyuo vikuu vya serikali, iligharamiwa na serikali kwa asilimia 100. Miaka ya 1990, kufuatia utekelezaji wa mageuzi ya kiuchumi (“Structural Adjustment Programme”), mpango uliofadhiliwa na Benki ya Dunia (“World Bank - WB”) na Shirika la Fedha la Kimataifa (“International Monetary Fund – IMF” ), serikali ilianzisha utaratibu wa kuchangia elimu, ambapo wanafunzi walichangia sehemu ya gharama za elimu, na serikali kulipia sehemu iliyobakia.

Jambo hili lilizua mgogoro mkubwa kati ya wanachuo (hasa vyuo vikuu) na serikali; wanafunzi wengi kipindi hicho walipinga mpango wa kuchangia gharama (“Cost Sharing”), wakidai wengi wao wanatoka katika familia masikini sana vijijini ambapo wanategemea kilimo. Utakubaliana na mimi kwamba watanzania karibu asilimia 80 wanaishi vijijini na chanzo kikuu cha mapato ni kilimo cha kujikimu kwa chakula.

Serikali ilishindwa kufuta huo mpango, kwa kuwa ilikuwa ni moja ya masharti ya mkopo kutoka kwa mashirika haya ya fedha niliyoyataja hapo juu.

Muda sii mrefu, serikali ikajitoa kabisa kugharamia elimu ya vyuo vya kati na vyuo vikuu, badala yake ikaanzisha mpango wa kutoa mikopo (Mikopo ya elimu ya Juu) kwa wanafunzi wachache wa vyuo vikuu waliokidhi vigezo kadhaa (ikiwa ni pamoja na wale wanaotoka katika familia duni).

Wanafunzi Wote Wanastahili Kupata Mikopo au Ufadhili
Ni dhahiri kwamba familia nyingi, ziwe za mijini au vijijini, ni maskini wa vipato kiasi cha kushindwa kugharamia elimu ya watoto. Wananchi wengi hawafurahishwi na mpango wa serikali kujiondoa kufadhili elimu ya vyuo vya kati na vyuo vikuu; hii ni kwa sababu wengi wana kipato cha kujikimu. Lakini, pia kuna familia ambazo ni maskini zaidi, baadhi yake zikifadhiliwa na Mfuko wa Kunusuru Kaya Maskini, maarufu kama “TASAF”. Natambua mikopo inatolewa kwa wanafunzi wachache, na hawa wachache wengi wao hawapati mkopo wa kutosha kugharamia masomo, kutokana na ukweli kwamba serikali haina fungu la kutosha kwa ajili ya mpango huo.

Kwa mtizamo wangu, karibu wanafunzi wote wana uhitaji wa mikopo na/au ufadhili kwa ajili ya kugharamia elimu yao vyuoni. Vigezo vilivyowekwa na serikali kupata mikopo hii, ikiwa ni pamoja na umaskini wa kaya wanazotoka wanafunzi, ni kama kubagua watoto wa Tanzania, maana karibu wanafunzi wote wanatoka katika kaya masikini.

Kama serikali imeamua kutoa mikopo kwa wanafunzi, basi wanafunzi wote wana haki ya kuomba na kupata mikopo, kwa sababu itarejeshwa, tena kwa riba. Kwa zile kaya masikini kabisa, serikali inaweza kutoa ufadhili (“grant”). Hii itaondoa dhana ya ubaguzi inayojengeka miongoni mwa wanafunzi na wazazi, pale inapoonekana mwanafunzi ambaye anatoka katika kaya yenye kipato cha juu anapata mkopo, na mwingine anayetoka kaya masikini zaidi anakosa mkopo.

Mfumo wa Kuomba Mkopo ni Mgumu na wa Gharama

Ni ukweli usiopingika kwamba tupo kwenye enzi ya kidigitali, na hatuwezi kurudi nyuma. Mfumo wa kuomba mkopo ni wa kidigitali, lakini umefanywa kuwa mgumu na wa gharama sana, kwani mwanafunzi anapaswa kulipa ada ya maombi, shilingi za kitanzania elfu thelathini (30,000/=), kulipia uhakiki wa cha cheti cha kuzaliwa (RITA), sh. Elfu tano (5,000/=); jumla ya fedha inayolipwa serikalini ni sh elfu thelathini na tano (35,000/=). Gharama nyingine ni malipo ya mwanasheria kushuhudia taarifa katika fomu ya maombi yasiyopungua sh. elfu kumi (10,000/=) na gharama za huduma ya uchapaji zisizopungua sh elfu kumi (10,000/=).

Kwa hiyo mwanafunzi anahitaji kuwa na sh elfu hamsini na tano au zaidi ili akamilishe maombi ya mkopo.

Kama lengo ni kumlenga mtoto wa maskini, ni dhahiri kwamba hatapatikana kirahisi; fikiria mtu anaishi kijijini ambapo akihitaji huduma ya tarakilishi (komputa) inayopatikana mjini, itabidi asafiri umbali wa kilomita hadi mia moja au zaidi, ambapo atapaswa kugharamia usafiri, chakula na malazi kwa siku atakazotumia kukamilisha kujaza fomu ya maombi ya mkopo na kutuma.

Endapo mwanafunzi hajapata mkopo mwaka wa kwanza, anaweza kuomba tena mwaka unaofuata. Kuna wanafunzi wanaomba zaidi ya mara mbili, na baadhi wanapata mkopo wakiwa mwaka wa tatu chuoni. Jambo linaloumiza zaidi ni kwamba kila mwaka maombi hufanyika upya, kwa maana ya kulipia gharama zote kama ilivyotajwa hapo juu.

Swali la msingi: Kwa nini watoto hawa wa masikini ambao serikali inalenga kuwasaidia wanalazimika kulipa kiasi hicho cha fedha? Kama ni masikini serikali inadhani wanapata wapi fedha hizo ilhali wanahitaji msaada?

Sina uhakika karma viongozi wa juu, akiwemo raisi wa nchi wanafahamu adha wanazopata hawa wanafunzi katika swala la mikopo.

Dhana ya Rushwa katika Bodi ya Mikopo
Baadhi ya wanafunzi na wazazi wanashuku uwepo wa rushwa katika mchakato wa kutoa mikopo kwa wanafunzi wa vyuo. Hii ni kwa sababu, unakuta kuna mwanafunzi ambaye familia yake inajiweza kwa maana ya kuweza kugharamia masomo ya mwanafunzi sii tu hapa nchini, bali hata nje ya nchi, lakini anapata mkopo kwa asilimia mia moja (100%), ilhali mwingine ambaye familia yake inapata mlo mmoja kwa siku kwa tabu hajapatiwa mkopo (hata kama ameomba).

Binafsi siamini kama kuna dhana ya rushwa katika Bodi ya Kutoa Mikopo ya Elimu ya Juu, lakini mazingira magumu yaliyowekwa, yanasababisha kuwafanya watu kuamini kwamba kuna rushwa

Dira ya Miaka 25 (2025 – 2050)
Kuelekea dira ya miaka 25 ijayo, natamani kuwe na mageuzi makubwa katika mfumo wa elimu ya vyuo vya kati na vyuo vikuu, kuhakikisha kila mwanafunzi anayepata nafasi ya kujiunga na chuo anagharamiwa masomo yake kwa asilimia mia moja (100%), aidha kwa kupatiwa ufadhili, au mkopo.

Bila shaka, wengi watasema, serikali itapata wapi fedha za kutosha kumlipia kila mtu? Mageuzi haya yawe ni pamoja na serikali kuacha kubeba peke yake hili jukumu la kutoa mikopo, badala yake ikaribishe taasisi za fedha nchini (ambazo zina ueledi wa kutoa mikopo) kufanya kazi hiyo. Serikali itapaswa kuwa mdhamini mkuu kwa kila mwanafunzi anayeomba mkopo. Lakini, serikali inaweza kutoa ufadhili kwa wanafunzi kutoka kaya maskini na/au wanafunzi wenye ulemavu mbalimbali wasioweza kugharamia elimu yao.

Hii italeta usawa na kuondoa manung'uniko mbalimbali ikiwa ni pamoja na baadhi ya wanafunzi kuhisi kubaguliwa na serikali.

Hitimisho
Serikali iunde tume maalumu itakayoshirikisha wataalamu mbalimbali kutoka ndani na nje ya serikali kutathmini mpango wa kugharamia elimu ya vyuo vya kati na vyuo vikuu na kupendekeza mpango mpya utakaohakikisha watanzania wanapata elimu hiyo kwa usawa.
 
Upvote 14
Serikali ikiweka mazingira mazuri yatakayowezesha wananchi kutumia vyema rasilimali za nchi hii, ajira zitaongezeka kwa kiasi kikubwa. Hili litawezesha wahitimu wengi wa vyuo mbalimbali kuwa na uhakika wa kujiajiri na kuajiriwa, na hivyo kuweza kurejesha mikopo waliyotumia kugharamia elimu yao kwa wakati.
 
Cuba ni nchi ndogo na inayoendelea, lakini wananchi wote wana fursa ya kusoma kuanzia shule ya msingi hadi chuo kikuu ngazi zote BURE!
 
Malipo yanayopokelewa na serikali kutoka kwa waombaji wa mikopo kupitia ada za maombi, ni kiasi takriban sh. Bilioni 17 kila mwaka. Sijawahi kuona maelezo yoyote kuhusiana na matumizi ya fedha hii!! Vinginevyo hiki ni kiasi kinachoweza kufadhili wanachuo karibu 5,800 kwa kiasi cha sh. Milioni 3 kila mmoja.
 
Wanafunzi wa vyuo, husumbuliwa sana kama hawajalipa ada, kutokana kutopata mkopo au mkopo kuchelewa.
 
Urejeshaji wa mikopo ya elimu huwa mgumu kwa sababu wahitimu hawaandaliwi vizuri kuajiriwa na/au kujiajiajiri. Pia hamna mfumo sahihi wa kumfutilia mhitimu kujua ameajiriwa au kujiajiri wapi!
 
Watanzania wakipewa kipaumbele cha kwanza kuwekeza katika rasilimali zilizopo nchini, uchumi utachechemka, na hivyo kuwezesha watu wengi kupata elimu ya juu bila ya kuitegemea serikali.
 
Serikali kuu igatue jukumu la kugharamia elimu, kwa serikali za mitaa, taasisi mbalimbali (za umma na binafsi). Kabla ya Uhuru vyama vya ushirika viligharamia elimu ya watoto wa wanachama wao kuanzia msingi hadi vyuo vikuu! Jambo hili linawezekana hata Leo.
 
Back
Top Bottom