Je wewe binafsi unafahamu nini kuhusu Roho na akili?
Umeuliza swali zuri sana. Niliwahi kuandika mada maalumu kuhusu ROHO. Nikaipa anuani hii "Ukweli kuhus Roho na yote yanayo ihusu".
Hapa nakuwekea kama ilivyo mada hiyo.
"Katika mambo makubwa mno yenye kuwatatiza watu tangu dunia inaumbwa ni hili jambo kuhusu
ROHO.
Wamepita Wanafalsafa wa kale na wa sasa, Wanasayansi wa zamani na wasasa, watu wa dini, na wasio kuwa hao katika kuelezea Roho ni nini, hatimae wamekuja na mitazamo mingi yenye kutatiza watu na isiyokuwa na ithibati wala hakika yoyote.
Lakini hao wote mpaka Wakana Mungu ( Atheists) wakakubaliana ya kuwa KIFO ni ule muda ambao maisha hukoma kwa kiumbe, au Roho kuacha mwili. Suala la Roho limebaki kuwa jambo lililo fichikana kuhusu hakika yake na undani wake, na Mola wetu hakutoa elimu juu ya Roho isipokuwa kidogo mno, na jambo hili limebaki kwake kwa mapana yake.
Mola wetu anasema katika Qur'aan, juu ya ukweli kuhusu ROHO.
85. Na wanakuuliza khabari za Roho. Sema: Roho ni katika mambo ya Mola wangu Mlezi. Nanyi hamkupewa katika ilimu ila kidogo. (Israa : 85)
Hii inaonyesha ya kuwa suala la elimu juu ya Roho ni elimu kubwa mno na sisi tumepewa elimu ndogo sana juu ya ROHO na jambo hili linabaki kuwa kwake Mola wetu kwa undani wake.
Kama hali iko hivi, ni nini Roho ? Ni zipi sifa zake? Ni zipi tabia zake na ni upi uwezo wake ? Maswali haya watu hujiuliza sana.
Katika Elimu hiyo ndogo tuliyopewa na Mola wetu, tunaipata kutoka katika vyanzo vya uhakika na kuaminika ya kuwa, Roho ni kitu kisicho onekana, chenye mafungamano ya moja kwa moja na mwili.
Lakini Roho hiyo ina sifa kadhaa kwazo huwa tunazitumia kuelezea vitu vyenye kushikika (Tangible things), kama vile hupulizwa na Malaika kuupa mwili uhai na hutolewa kipindi mja anapokufa, hukutana na kuzungumza.
Mwili unakufa ila Roho haifi, roho hubaki milele. ROHO ni katika vile viumbe ambavyo vina mwanzo ila havina mwisho.
Huu ndiyo ukweli kuhusu ROHO kwa ufupi.
Zingatia : Wasomi wakubwa na wahakiki wa mambo, wametofautiana juu ya Roho na Nafsi, ya kuwa je ni kitu kimoja au ni vitu viwili vyenye kutofautiana. Wapo walio sema ya kuwa Roho na Nafsi ni vitu viwili tofauti na kutofautiana kwake hulingana na muktadha wa hali, wengine wakasema ya kuwa Nafsi ni mjumuiko kati ya Roho na Mwili, na wapo waliosema ya kuwa Roho ni Nafsi na Nafsi ni Roho.".
Hiki ndicho nilichokiandika katika mada hiyo.
Ama kuhusu akili, akili kiasili ni tamko la Kiarabu lenye maana ya "Kizuizi", waarabu kamba ya kumfungia mbuzi asitoke nje ya eneo iliitwa "aql" . Kwa maana ya kisheria AKILI ni kizuizi kinachomfanya mwanadamu asikozee katika maamuzi. Ndiyo maana ukisoma katika elimu ya Mantiki (Logic) wanakwambia ya kuwa Mantiki ni ya kutumia akilo kwayo humfanya mtu asikosee katika kujenga hoja. Tunarudi kule kule katika maana ya msingi. Yaani akili ni kizuizi kinachomfanya mja asikosee katika kutenda mambo.
Tuendelee na mjadala kutokea hapo.