Sipendi tena sitaki wabunge wajiongezee mishahara
Lula wa Ndali-Mwananzela Mei 13, 2009
Raia Mwema~Muungwana ni Vitendo
SITAKI tena sipendi kusikia kuna mbunge ana wazo, nia, ombi, njozi au kisingizio chochote cha kujiongezea mshahara mwaka huu.
Na sitaki kabisa kufikiria kuwa katika hali mbaya ya uchumi inayoikabili dunia ambayo imefanya tuombe msaada wa kichocheo cha uchumi toka kwa IMF na Benki ya Dunia, kuna watu wanataka kujiongezea mshahara kwa sababu wana uwezo huo.
Na nachukizwa na mtu yeyote ambaye ameshuhudia wafanyakazi wa nchi yetu wakinyimwa nyongeza ya mshahara mwaka huu, wakati yeye ana uwezo wa kujiongezea mshahara kwa kupiga kura!
Endapo wabunge wa Tanzania wataamua kujiongezea mishahara yao mwaka huu kufikia kiasi cha shilingi bilioni karibu 3.5 kwa watu wasiozidi 325 kwa mwezi, basi kwa mara ya kwanza tutakuwa na ushahidi wa kundi dogo la watu ambao si tu wamefikia mahali kwamba wanaamini wanaweza kufanya lolote, bali kwa kutumia uwezo wao kisheria wameamua kuchomeka mirija yao yenye ncha kali kwenye mgongo wa kila Mtanzania.
Kuna sababu kubwa tatu ambazo zinaweza kumfanya mtu aongezewe mshahara. Kustahili (pongezi, kupanda cheo n.k), kurekebisha kulingana na hali ya uchumi/maisha, na kujigawia kwa sababu mtu anaweza.
Hebu tuziangalie sababu hizi na kuona zinahusiana vipi na wabunge wetu na kama zinatosha kutufanya wananchi tukubali nyongeza hiyo ambayo wanataka kujipa.
Kustahili
Hii ni sababu inayoongoza katika watu kupewa nyongeza ya mishahara. Baada ya kufanya kazi kwa muda fulani basi mtu anaweza kwenda kwa waajiri wake na kujenga hoja ya kwa nini anastahili nyongeza ya mishahara.
Hata hivyo, kwa kawaida waajiri wenyewe wanawapima watumishi wao kila baada ya muda fulani na wakiridhika na vipimo wanavyotumia basi mtumishi yule hata kama cheo chake kinabakia pale pale, anaweza kuongezewa mishahara kwa sababu anastahili. Na wengine wanaongezwa mshahara kutokana na makubaliano na waajiri wao; makubaliano ambayo yanaelezea ni kwa kiasi gani mshahara wake utapanda na katika muda gani.
Zaidi ya yote, kuna wakati ambapo mtumishi anakuwa amefanya kazi nzuri sana kwa shirika au kampuni na kazi hiyo imelisababishia shirika au kampuni hiyo faida au kuijenga kwa namna fulani na hivyo mchango wa mtumishi huo unaheshimiwa kwa kumuongezea mshahara na hata cheo kwa sababu kutokana na mchango wake amestahili nyongeza hiyo.
Sasa hapa tunajiuliza ni kitu gani kimewafanya wabunge wetu waamini kuwa wanastahili nyongeza ya mishahara? Hivi wameisoma ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali? Wanafuatilia mambo ya ufisadi uliokubuhu? Ni kitu gani ambacho wanafikiri wao wamekifanya ambacho kinawafanya wastahili. Kuzungumza bungeni kwa jazba? Mbona hata walevi vilabuni na vijana vijiweni wanafanya vizuri tu?
Kwamba wameweza kutembea huku na huko na kukagua hili na lile basi wanastahili nyongeza na mishahara? Vipi wale wakaguzi wa afya na walimu, polisi wanaosimama kuongoza magari na wanajeshi wanaochezea hatari kila kukicha kama tulivyoona Mbagala? Hawastahili nyongeza?
Hakuna kitu chochote ambacho tunaweza kusema wabunge hawa wamekifanya vizuri na wanastahili pongezi. Ndani yao wamegawanyika. Maslahi yao yanafuata makundi ya watu wachache, wengine ndiyo hata kukemea ufisadi hawawezi kwa sababu kuchaguliwa kwao tena mwakani kunategemea ufadhili wa hao hao mafisadii, na bado wanataka nyongeza ya mishahara?
Kwamba wanahisia ya kustahili ni sawa na mlevi ambaye amekaa karibu na gudulia la chimpumu, kwa vile gudulia lipo karibu na mama "fulani" anawahudumia wengine basi mlevi huyo anaona anastahili kugida tena kama la kwake. Kwa kifupi, wabunge hawa waliopo sasa hawastahili nyongeza ya mishahara ambayo wananchi wengine hawastahili.
Kurebisha mshahara kulingana na hali ya uchumi.
Mara nyingi mishahara pia hurekebishwa ili kupatanisha na nguvu mbalimbali za kiuchumi na hivyo kufanya ilingane au ikabiriane na hali ya maisha.
Kwa kufanya hivyo maofisi, idara na hata serikali hupitia mishahara ya watumishi wake na pale inapobidi basi wanairekebisha aidha kwenda juu au kwenda chini kulingana na mafanikio ya kampuni, idara au serikali hiyo.
Kama kuna faida ya kutosha basi taasisi hizo zinawaongezea watumishi wake mishahara. Leo hii hali ya kiuchumi duniani yawezekana ni nzuri kabisa Tanzania kiasi cha kutaka wabunge wajiongezee mishahara!
Dalili zote na kauli za viongozi wengine ni kuwa Tanzania inakabiliwa na hali mbaya ya kiuchumi na mikutano ya hivi karibuni na ombaomba ya misaada inayoendelea inataka tuamini hivyo. Sasa kama hali ni mbaya hivyo hawa wenzetu wameona nini cha kuwafanya waamini kuwa huu ni wakati muafaka kufikiria na kuzungumzia kujiongezea mishahara?
Kama hali ni nzuri namna hiyo, hivi hawaamini kuwa Watanzania wengine nao wangependa kufaidi matunda hayo ya uchumi ambayo wenzetu wameyaona? Je, wakulima wao wanapata faida gani wakati pamba yao na kahawa inapata shida kuuzika kwenye soko la dunia?
Je, walimu, madaktari na manesi ambao wanafanya kazi katika mazingira magumu kabisa nao hawastahili nyongeza ya aina fulani kutokana na kazi yao ngumu na ya hatari?
Sasa hawa wasahaulifu wetu ambao wameweka mbele maslahi ya matumbo yao wamepata wapi ujasiri wa kufikiria na hatimaye kutamka kuwa wanafikiria kujiongezea mishahara yao kana kwamba hii ni paradiso ya Bongo ambayo wao ndiyo wameumbwa kufurahia maisha yake milele?
Wakijiongezea mishahara wallah, hapatakalika hapa! Tutaandamana hadi kwenye kijiji cha Spika na wabunge wote hawa watakaopiga kura kujiongezea mishahara katika mwaka huu tutawataja kwa majina yao kwani hilo peke yake linatosha kabisa kuwawekea alama ya kutorudi mwakani.
Kama ni kuibiwa tumekwisha kuibiwa vya kutosha, kama kuibiwa huku tunaambiwa ni "kujiongezea" ni kulitukana Taifa hili la wakulima na wafanyakazi!
Bilioni 3.5 kwa mwezi (kwa mwaka ni shilingi bilioni 42 sawa na za Kagoda!) kwa watu 320? Kweli jamani haki hii? Hata shetani anaweza kufumba macho kwa aibu!
Wakisema kwa sababu ya kazi ngumu, tuwakatalie kwani kuna watu wanafanya kazi ngumu kuliko ya kutembea na kuzungumza! Kama kuna watu wanastahili nyongeza basi ni wale waliofichua ufisadi kwenye taasisi mbalimbali na waandishi wa habari wamejifunga vibwebwe kuongoza mapambano haya wakati wanasiasa wetu wakituzungushia maneno kama pia.
Kama ni hali ngumu na maisha magumu na majukumu muhimu, hoja yangu ni kuwa wafanyakazi wote wapewe nyongeza tena kwa kiwango kinacholingana kitakwimu na nyongeza wanayotaka kujipa tuone kama hatutatangaza nchi kufilisika!!
Kujiongezea kwa sababu wanaweza.
Kati ya watumishi wote wa Watanzania ni wabunge pekee ambao wanajiongezea mishahara kwa kujipigia kura! Yaani, wanajadiliana na wanaamua kama wanastahili nyongeza na wakikubaliana wanapiga kura kujipa nyongeza na kama vile mazingaombwe, basi hao wanaanza kutafuna!
Hata Rais hajipangii mshahara na marupurupu, majaji hawajipangii mishahara (kuna chombo kinachosimamia hilo), watumishi wa umma wengine hadi mambo yakubalike huko "Utumishi" tena bajeti ipitishwe na wabunge!
Sasa hii ndiyo sababu pekee ya wao kufikiri wanataka nyongeza ya mishahara. Kwa sababu wanaweza. Ndiyo maana wabunge wengine wamekasirika na kuja juu baada ya Dk. Wilbroad Slaa kutangaza hiyo mishahara na kusema kuwa fedha wanayolipwa wabunge kweli ni fedha nyingi.
Wabunge wetu wakacharuka kwa nini "mheshimiwa" mwenzao anawaambia wananchi juu ya fedha "zao"! Watu na akili zao wakiwa wamelewa madaraka wakaunganika wapinzani na watawala, kushangazwa na kitendo hicho!
Hii ni kashfa. Kwa taifa linalotegemea misaada na ambalo haliachi kuombaomba, ni kufuru kubwa kufanya kikundi cha watu 320 kuishi kama wako mbinguni! Kwa taifa ambalo licha ya kujitosheleza kwa kuzalisha asilimia zaidi ya 100 ya mahitaji yake ya chakula na bado likalia njaa hii ni kashfa!
Kwa taifa ambalo viongozi wake hawawezi kutulia nyumbani kwa mwezi mzima bila hamu ya kwenda nje kutumia mamilioni ya shilingi wakikamua ng'ombe wa Mtanzania hadi chuchu zinatoboka, ni kashfa!
Hii ni kashfa kwa Taifa ambalo liliwarudisha watoto 30 kutoka kusoma Ukraine kwa "kukosa shilingi milioni 400. Ndiyo ni kashfa kwa nchi ambayo Jiji lake kuu lina kituo kimoja tu cha Zima Moto cha umma kwenye watu zaidi ya milioni 4 huku vituo vingine vya binafsi vikitengeneza hela kwa kwenda kuokoa (sijui nchi gani nyingine idara ya Zima Moto inaendeshwa kibinafsi hivyo!).
Ni kashfa kwa sababu tukio kama la Mbagala linatokea na hakuna mfumo mzuri wa uokoaji na watu wanakufa kutokana na uzembe wa watu wachache walioshindwa kuandaa maeneo hayo kwa janga la aina hiyo, huku wakiangalia miaka nenda miaka rudi watu wakijenga karibu na badala ya serikali kuhamisha ghala ndio wanajenga na shule si mbali na ghala hiyo! Halafu kuna watu 320 wanasema wanataka "nyongeza".
Kwa kimombo niseme "hell to the no!" Hawastahili nyongeza hata thumni! Ninachotaka kusema ni kuwa kwa wakati huu na saa hii hakuna mbunge hata mmoja anayestahili nyongeza ya mshahara hata wa thumni.
Hakuna kati yao ambaye anaweza kusimama na kusema "mimi nastahili!". Wote kama kundi wamepitisha sheria za ajabu kabisa nchini, sheria ambazo ni mwanzo na muendelezo mkubwa wa mambo ya kifisadi tunayoyashuhudia.
Hawa hawa ambao walitakiwa kuisimamia serikali wanarudi mwaka wa tatu leo kuiangalia tena ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu ikifinua mambo yale yale ya Meremeta, NSSF na Mwananchi Gold huku fedha zetu zikiwa zimeliwa kama kilichoenda kwa mganga!
Wamebakia kuzungumza na waandishi wa habari na kutoa maneno ya ukali. Watu hawa hawa wanauangalia usalama wa taifa uliokatwa nguvu zake kwa sheria mbovu kabisa ya Usalama wa Taifa ya 1996, na hakuna mpango mwaka huu kuifanyia marekebisho wala mwakani!
Wakitaka nyongeza ya mshahara ni lazima kwanza kabisa wahakikishe kabla ya nyongeza yoyote mambo yafuatayo yamepatiwa ufumbuzi wa kudumu.
Suala la Rada limemalizika na wahusika wote kushughulikiwa kisheria (si kesi bado iko mahakamani, hiyo haihesabiki.
Suala la EPA na kesi zote zimekwisha kwanza na fedha zote zimerudishwa.
Suala la Kagoda limefikia tamati kwa wahusika kutiwa pingu na kufikishwa mahakamani na uamuzi kutolewa.
Suala la Meremeta limefikia tamati kwa wahusika kujulikana na fedha zilizochotwa kurudishwa na wahusika kutinga kizimbani.
Suala la Deep Green Finance ile kampuni inayohusishwa na waziri mmoja linajulikana na fedha iliyoingia kule inarudishwa na waliyopewa mawakili nayo inarudishwa (wizi kwa jina lolote bado ni wizi!).
Suala la Mabadiliko ya Katiba kuruhusu wagombea huru linatekelezwa kulingana na amri ya Mahakama ya Rufaa.
Suala la Dowans limemalizika kwa serikali kutaifisha mitambo ya Dowans (kuhakikisha mitambo hiyo haiondolewi), kuwachunguza wanaotuhumiwa kushiriki katika kampuni hiyo hata kama ni wabunge wenzao kama wamekiuka maadili na kuhakikisha watu kama yule mfanyabiashara wa Mashariki ya Kati hawaruhusiwi kufanya biashara yoyote na serikali kwa miaka 10 ijayo au zaidi!
Suala la matatizo ya mikopo ya elimu ya juu linatatuliwa mara moja na daima na kuhakikisha hakuna kijana wa Kitanzania anayetaka elimu ya juu na ana uwezo huo asipate nafasi hiyo kwa kupitisha mabadiliko ya sheria ya bodi ya mikopo mapema iwezekanavyo.
Kuhakikisha mabadiliko ya sheria ya vyama vya siasa ambayo yamependekezwa hayapitishwi kama yalivyo bali yanaakisi kweli uhuru wa demokrasia na usawa wa vyama vya siasa na uwazi wa vyama vyote vinavyopokea hata senti moja ya fedha za wananchi kama ruzuku.
Nje ya hapo hakuna mshahara wala nyongeza ya mshahara, kwani najua ni kwa nini hasa wanataka nyongeza hiyo. Hii ndiyo sababu ya kweli.
Janja ya nyani! Lengo kubwa la wabunge kutaka kujiongezea mshahara sasa ni kwa ajili ya kujiandaa kwa mafao yao baada ya Bunge linalokuja kwani wakijiongezea mshahara sasa na wakaanza kulipwa hadi mwisho wa Bunge hili, wale wabunge ambao hawatarudi baada ya Uchaguzi Mkuu mwakani (ambao wanajijua ni makuwadi wa ufisadi) wanataka kuhakikisha mambo yao yako poa.
Maneno yote wanayosema ni janja ya nyani! Tusiwakubalie.
Vinginevyo, kama kweli wanataka nyongeza ya mshahara kwa wabunge, napendekeza tufanye uchaguzi mpya mwaka huu ili nyongeza hiyo iwahusu wabunge wapya tu na si wa sasa! Vinginevyo, nyongeza hiyo ije na Bunge jipya, kama watumishi wengine hawaongezewi mshahara mwaka huu, basi siyo Rais, Jaji, wala Mbunge mwingine anayestahili nyongeza hata senti tano!
Barua-pepe:
lulawanzela@yahoo.co.uk