Maaskofu: Dawa ya Mwasapile inaponya
- Ni maaskofu wa KKKT Laizer, Shao na Akyoo
- Wathibitisha kuwa waliinywa na wameponywa
Mchungaji mstaafu Ambilikile Mwasapile akiongea na wageni wake waliofuata huduma yake ya tiba nyumbani kwake Loliondo.
Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), limesema linatambua na kubariki dawa inayotolewa na Mchungaji wake mstaafu anayefanyia shughuli zake Loliondo, Ambilikile Mwasapile, huku baadhi ya maaskofu wa kanisa hilo wakithibitisha kwamba wamekunywa dawa hiyo na kuponywa.
Wakizungumza na gazeti hili kwa nyakati tofauti kwa njia ya simu, Maaskofu wa kanisa hilo Thomas Laizer wa Dayosisi ya Mkoani Arusha, Dk. Martin Shao wa Dayosisi ya Kaskazini, walisema huduma inayotolewa na Mchungaji Mwasapile ni sahihi na imeanza siku nyingi na kwamba wao ni miongoni mwa watu wa mwanzoni waliowahi kunywa dawa hiyo na kupona.
Askafu Laizer alisema kwa mujibu wa imani na taratibu za KKKT, mchungaji huyo yupo sahihi na Kanisa halina mgogoro naye.
"Ifahamike kwamba kazi ya utoaji dawa haikuanza jana, ilianza siku nyingi na mimi kama Askofu niliyembariki Mchungaji Mwasapile, nililetewa taarifa na wachungaji wengine pamoja na wakuu wangu wa majimbo juu ya mafunuo ya Mchungaji na ndipo tulipoanza kufuatilia na kufanya mahojiano naye na Kanisa likagundua kwamba tiba yake ipo sahihi," alisema Askofu Laizer.
Askofu Laizer alisema binafsi alikuwa akisumbuliwa na kisukari pamoja na shinikizo la damu kwa muda mrefu, lakini baada ya kupewa dawa ya mchungaji huyo amepona na hajapata kunywa dawa nyingine.
"Unajua kuna watu wanashangaa kinachofanyika pale, ni kwamba dawa ile inaambatana na sala pamoja na imani," alisema.
Alisema akiwa kiongozi wa kanisa alipopata habari hizo aliunda jopo la wachungaji kufuatilia kwa kina ufunuo na uwezo wa kuponya wa mchungaji huyo na ikagundulika kwamba hajaenda kinyume cha imani ya KKKT.
Alisema hata mti ambao mchungaji huyo anautumia kuchemsha na kuwapa watu, unajulikana na kila mtu, hivyo hakuna kukengeuka kunakofanywa naye.
"Zaidi sana kinachofanyika pale ni sala na imani, hakuna kitu kibaya tulichokiona sisi kama viongozi wa Kanisa," alisema.
Pamoja naye aliwataka maaskofu wenzake, ambao walikwenda kumtembelea mchungaji huyo mstaafu kwamba ni Paul Akyoo wa Dayosisi ya Meru aliyefuatana na mkewe, pamoja na Dk. Martin Shao wa Dayosisi ya Kaskazini.
"Mke wa Askofu mwenzangu Akyoo alikuwa hawezi kutoka alikuwa akisumbuliwa na kisukari, lakini baada ya kupewa dawa hiyo juzi nilipompigia simu, akasema amepona na yupo kwenye harusi," alisema.
Askofu Laizer alisema pamoja na jambo jema linalofanywa na mchungaji huyo, kuna watu wameshaanza kutia fitina kutokana na wivu tu.
Akizungumzia historia ya mchungaji huyo, alisema tangu aanze kazi ya kuchunga kondoo alikuwa mtiifu na mnyenyekevu.
Alisema alimbariki Mwasapile kuwa Mchungaji mwaka 1980 mjini Babati na alikaa eneo hilo kwa miaka saba.
Alisema baada ya hapo alihamia eneo la Sombe ambako alikaa kwa miaka 12.
Kwa upande wake Askofu Dk. Shao alisema anamshukuru Askofu mwenzake Laizer aliyemshirikisha katika msafara huo, pamoja na Akyoo.
Alisema baada ya kufika na kuzungumza na Mchungaji huyo waligundua kwamba hakuna dalili yoyote ya ushirikina katika utoaji wa dawa hiyo wala hakuna udanganyifu wa aina yoyote.
Alisema baada ya kufika huko na kukuta umati wa watu, waliwatoa hufu wagonjwa wote kwamba mtu aliyekuwa akiwapa tiba wanamfahamu na ni mtumishi mwenzao wa muda mrefu.
Alipoulizwa kama na yeye alikunywa dawa hiyo, Askofu Shao alisema: "Nilikunywa, ukishasema kwamba kitu fulani ni halali, basi unatakiwa ushiriki, mimi nilikunywa dawa hiyo, hasa ikizingatiwa kwamba inatibu magonjwa mengi."
Alisema watu wanaopuuza dawa ya Mchungaji huyo ni wale ambao hawajui njia anazotumia Mwenyezi Mungu kuwaponya watu wake.
Alisema walijadiliana na wagonjwa wote, na kumuuliza maswali kadhaa mchungaji huyo na kubaini kwamba maono aliyopewa na Mungu ni sahihi.
"Mungu ana njia nyingi sana za kugawa vipaji kwa watu wake,"alisema Askofu Shao.
Aliwataka wananchi wote kumuomba Mchungji huyo ili aendelee kuwa na afya, hasa ikizingatiwa kwamba ana majukumu makubwa ya kuhudumia watu kuanzia alfajiri hadi usiku.
"Kwa hiyo sasa tunachojadili ni kumsaidia ili aendelee vema na pia kuhakikisha utaratibu mzuri unakuwepo katika kutoa huduma zake, pia tunaangalia suala zima la mazingira ili mti unaotumika kutibu usitoweke,"alisema.