MJADALA: Namna makuzi/ malezi yanavyoweza kuwa chanzo cha matatizo ya afya ya akili

MJADALA: Namna makuzi/ malezi yanavyoweza kuwa chanzo cha matatizo ya afya ya akili

JamiiTalks

JF Advocacy Team
Joined
Aug 7, 2018
Posts
685
Reaction score
1,124
1679301068197.png

Je, unafahamu kuwa Kumbukumbu ya Matukio Mabaya (Trauma) ya Utotoni huweza kuathiri Afya ya Akili ya Wahusika?

Tafiti zimeonesha kuwa Watoto wanaopitia changamoto kama Unyanyasaji, Kutelekezwa au Kuishi katika Mazingira magumu wana uwezekano mkubwa wa kupata na kuishi na changamoto za afya ya akili bila hata wao kujua.

Kwa haya na mengine mengi, usikose kujiunga nasi katika Mjadala na Wataalamu katika Twitter Spaces ya Jamiiforums Machi 23, 2023 kuanzia saa 12:00 jioni mpaka saa 02:00 Usiku.

Mjadala huu utahudhuriwa na wataalamu wa afya na wanasaikoojia mbalimbali kama na Dkt. Esther Steven- Psychiatrist MUHAS, Dkt. Isaac Maro, George Boniface- Mental Health activist, Chris Mauki, Jiwa Hassan - Mshauri Mwanasaikolojia na Masuma Somji - Mental Health Advocate. Ambapo utapata fursa ya kujifunza na kuuliza mambo mbalimbali yanayohusu mada.

Pia, unaweza kutoa maoni na kuuliza maswali kupitia uzi huu. Maoni na maswali yako yatasomwa wakati wa mjadala.

Karibuni

DKT. ISAAC MARO
Afya ya Akili inapoanza kuhitaji umakini wengi huwa wanaipuuzia, hapo ndipo changamoto inapoanza kuwa kubwa, mfano ubongo unapohitaji kulala wewe usipolala, inaweza kupelekea matatizo mengine ya kiafya

Msongo wa Mawazo si kitu kibaya, lengo lake ni kukufanya uamke na kufanya jambo, mfano uwe na wivu wa maendeleo na vitu kama hivyo. Lakini unapozidi ndipo inapokuwa changamoto

Changamoto za Afya ya Akili sio lazima ziwe zilezile ambazo zinatajwa na Wataalamu, lakini hali hiyo inaweza kuja katika mazingira mengine tofauti kabisa kwa kutegemea na aina ya mazingira yanayotuzunguka

Inawezekana changamoto za Afya ya Akili zilizopo sasa zimetengenezwa na aina ya mazingira na maisha yetu, hivyo tunapokuwa na nafasi ya kuzungumza kwa uwazi tunaweza kutengeneza kizazi bora cha baadaye kuhusu Afya ya Akili

GEORGE BONIPHACE CHACHA (Mnasihi & Mwanasaikolojia)
Mtu anayekutana na changamoto ya Afya ya Akili anapoteza uwezo wa kutambua mazingira, uwezo wa kutambua nyakati, uwezo wa kufanya kazi na hana kitu anachochangia katika jamii yake

'Trauma' tunaweza kuitambua katika Kiswahili kama kumbukizi mbaya, hii inaweza kumtokea mtu anapokuwa na kumbukizi ya matukio mabaya kama vile ya ukatili (Mfano kubakwa), vita n.k

Trauma inaweza kuwa na viwango:
  • Ya kwanza ni ile ya tukio moja na linaloweza kusahaulika baada ya muda
  • Hatua ya pili ni kukutwa na matukio mabaya mfululizo
  • Tatu ni kukumbwa na matukio makubwa kama vile vita, ajali mbaya, kushuhudia mauaji n.k
Trauma inamfanya binadamu yeyote kuwa anafanya maamuzi sahihi katika muda ambao si sahihi Mfano unaweza kujihisi kulia wakati ambao huna mazingira ya kulia

DKT. ESTER STEVEN (Daktari Bingwa wa Afya na Magonjwa ya Akili)
Magonjwa ya Akili yapo mengi, ni zaidi ya 200. Tunayaweka katika makundi tofauti yanayoweza kufika makundi 20 Magonjwa hayo ni ambayo yaathiri fikra/tafsiri, hisia na tabia, yenyewe ni tofauti na Magonjwa mengine

Tunakisia kuwa kuna 4% ya Watanzania ambao wameugua ugonjwa wa akili, Duniani takwimu zinaonesha mtu mmoja kati ya watu nane ameugua Ugonjwa wa Akili

Hospitali ya Muhimbili kuanzia Januari – Machi 2023 kuna wagonjwa wa Akili 7,390 Hapo kuna ongezeko la robo tatu ya ilivyokuwa mwaka uliopita kwa kipindi kama hicho, kati yao Watoto ni 730, sehemu ya hao wagonjwa ni wale wanaopata tiba ya uraibu wa 'Heroine'

Wagonjwa wa Akili tunaowapokea wawili kati ya watatu ni Wanaume, ndivyo ilivyo kwa upande wa Watoto na watu wazima Pamoja na hivyo takwimu za kidunia zinaonesha wanaougua zaidi ugonjwa wa akili ni Wanawake, lakini kwa Hospitali hapa Nchini wanaokuja zaidi ni Wanaume

Mfano Mama mjamzito anapokunywa pombe, Mtoto wa tumboni naye anakuwa anakunywa kwa kiwango kilekile anachokunywa mama Pia, pombe ina kawaida ya kuathiri Ubongo, hivyo Mama anapokunywa inamaanisha inaenda kuathiri Ubongo wa Mtoto pia kwa kuwa Ubongo wake unakuwa haujakomaa

Trauma ya Mama inaweza kusababisha mtoto aliye tumboni naye kupata Ugonjwa huo japokuwa inaweza kutokea Mtoto mwenyewe tu akaumwa Ugonjwa wa Akili Kati ya Mama na Mtoto wa tumboni kuna masuala ya homoni yanayowaunganisha, mfano matukio kama manyanyaso na kila kinachomtokea Mama mjamzito kinaenda kumuathiri mtoto pia

Kugundua kama Mtoto ana Ugonjwa wa Akili unaweza kuona kuanzia miaka miwili au mitatu Mara nyingi Muhimbili huwa tunapokea wagonjwa katika hatua ambazo wamechelewa kugundulika Ili kumgundua mgonjwa ni mabadiliko ya ghafla au taratibu anayoyafanya tofauti na uhalisia wa jambo

Mtu anapoanza kubadilika tabia zake mfano kuanza kusali sana ingawa kusali sio jambo baya lakini kuna wakati tunapokea watu kutoka Sehemu za Ibada wameletwa na waumini wakiwa na tabia zisizo za kawaida na wengi wao wanakuwa wameanza kuonesha dalili za matatizo ya Afya ya Akili

DKT. CHRIS MAUKI
80% ya vile tulivyo leo ni kutokana na Malezi tuliyopitia utotoni na 20% ni sisi wenyewe tunayoamua kuwa Mtoto anapofanyiwa unyanyasaji inamuachia Trauma ambazo zinakuja kuathiri Afya yake ya Akili Na huu unyanyasaji unagawanywa kwenye makundi matatu, Unyanyasaji wa Kimwili, Kisaikolojia na Kihisia

Wazazi wengi wanadhani ili mtoto awe na utulivu wa akili ni kumtafutia Vitu kama Simu, Ipad au Kompyuta (Gadgets) Matokeo yake hivyo vitu vinachangia kuathiri Afya ya Akili ya Mtoto na wengine wanaanza kukosa usingizi mapema kwasababu ya matumizi ya vifaa vya Kidigitali

AUNT SADAKA
Msingi wa kwanza wa maisha ya Mtoto yaliyosimama unaanzia kwa wazazi Inapotokea labda mtoto kupelekwa Shule za Bweni moja kwa moja Mtoto anaanza kujisikia yeye hapendwi, anajuta na kuhisi labda yeye ni tatizo kwenye familia Mtoto anaanza kujenga hisia za huzuni na kupata 'Stress' na kusababisha mtoto ashindwe kulala au kula

Kama mtoto alitokea familia yenye huzuni au mambo mabaya hata uwezo wake wa akili unashuka Tabia zake zinaanza kubadilika na bahati mbaya watu wanaomzunguka wakianza kumsema waziwazi moja kwa moja mtoto anaanza kuvurugika, anaingia kwenye 'depression' na kuanza kujitenga Hapo ataanza kuingia kwenye kutegemea vitu kama Ulevi au Dawa na mwisho anakuwa kwenye tatizo la Afya ya Akili na mawazo ya hatari yatamjia ikiwemo kutaka kujiua

DKT. CHRIS MAUKI
Umri wa Mtoto unaweza kuchangia kukaa na vitu au kumbukumbu mbaya na kumletea majeraha na kuteseka mfano wazazi kutalikiana Wazazi wasipokuwa makini inawezekana wakafanya vitu ambavyo vinaweza kuwaachiwa watoto kumbukumbu mbaya hata kwa kutofuatilia vitu gani watoto wanapitia wakiwa nyumbani Kuna chapisho nilisoma linaonesha Unyanyasaji wa kingono unafanyika majumbani wanakoishi watoto

DKT. ESTER STEVEN (Daktari Bingwa wa Afya na Magonjwa ya Akili)
Kupata changamoto ya Afya ya Akili haitakiwi mtu mpaka apate Tatizo kamili ndiyo apate matibabu Matibabu ya Matatizo ya Afya ya Akili yapo ya Dawa na yasiyohitaji Dawa ambayo yanahusisha Tiba ya Kisaikolojia na wengine wanapewa Tiba ya Kazi ambayo humsaidia Mgonjwa kujengewa uwezo wa kikazi alioupoteza baada ya kukabiliwa na shida ya Afya ya Akili

Changamoto tunayokutana nayo kwenye matibabu ya wenye matatizo ya Afya ya Akili ni tabia ya Unyanyapaa kwa wengi wao kudhani kwenda Hospitali wanakuwa wakionwa kama Wagonjwa wa Akili au Vichaa. Wito wangu ni watu wasiogope kutafuta msaada kwa wataalamu

GEORGE B. CHACHA (Mnasihi & Mwanasaikolojia)
Trauma au kumbukumbu mbaya za Utotoni zinaweza kusababisha mtu ajenge tabia au imani ya vitu hata vile ambayo ni vibaya ikiwemo ukatili na kuishi navyo akiamini hata akija kuwa mzazi atawafanyia vilevile watoto Mfano kama alikuwa akipigwa utotoni anaweza kudhani akimpiga sana mtoto wake ndio njia ya kumnyoosha ili awe kama yeye

DKT. ESTER STEVEN (Daktari Bingwa wa Afya na Magonjwa ya Akili)
Ni kweli kuna changamoto ya gharama kubwa za matibabu na ndio maana tunahamasisha watu kujiunga na Bima ya Afya

Kuhusu matibabu ya Magonjwa ya Afya ya Akili, yapo ambayo yanaweza kutibika na kumalizika kabisa na yapo ambayo yanapunguzwa madhara na mgonjwa anaendelea na maisha lakini matibabu yake yanaendelea kwa muda mrefu

Kuhusu matibabu ya Magonjwa ya Afya ya Akili, yapo ambayo yanaweza kutibika na kumalizika kabisa na yapo ambayo yanapunguzwa madhara na mgonjwa anaendelea na maisha lakini matibabu yake yanaendelea kwa muda mrefu

MASUMA SOMJI (Mwanaharakati wa Masuala ya Afya ya Akili)
Kama jamii tunatakiwa kujitambua na kujua Afya ya Akili ni nini kwasababu mtu anaweza kuonekana kuwa yuko sawa kabisa lakini kumbe anakabiliwa na tatizo la Afya ya Akili Ni muhimu kuwepo kwa utambuzi wa tatizo na kuepuka unyanyapaa. Watu wengi wanasumbuliwa na Trauma za Utotoni na wengine wamekuwa wazazi wenye imani ya kupiga watoto kwasababu wao walipigwa, kitu ambacho sio sawa

Mimi mwenyewe nilikuwa na Sonona, lakini ukiniona unaona niko sawa na sina tatizo, hali hiyo ilikuwa inaniumiza Hivyo kinachotakiwa ni kutambua aina ya changamoto tunazokutana nazo na jinsi gani ambavyo zinaweza kutatuliwa
 
Nimemsikia Bw. George Chacha akisema kuwa mtu anaye-experience highs and lows kuna uwezekano ana changamoto kwenye afya yake ya akili. Nimekwisha!
 
Back
Top Bottom