Mkuu, huyo mwenzako aliyenitusi kabla ya mimi kumjibu hukuona matusi yake au yeye hakustahili kupewa hizo nasaha unazonipa??--- yeye kaanza kunitusi na mimi nilikuwa najibu mapigo, juu ya yote mimi niko peace tu.
Tuje katika mada, umeandika maneno katika lugha ya kiarabu nadhani ni watu wachache sana humu ndani wanaojua lugha ya kiarabu na hata kama wapo sio fasaha sana katika lugha hiyo kama waiivyokuwa fasaha katika Kiswahili na kiingereza, hivyo ni vyema unapoona "raha" kuandika kwa kiarabu basi pembeni weka tafsiri yake kwa kiswahili ili wengi wetu tusiojua vyema kiarabu tupate kufahamu.
Tarjama ya maneno yako ya kiarabu ni kama ifuatavyo (nakubali kurekebishwa nitakapo kosea);-
" Majini ni viumbe, mbali na kujibadili, haiwezekani kuonekana kwa macho ya kawaida ili kuwaona lazima uwe na maarifa".
Katika hadithi fulani za mtukufu mtume Muhammad (saw, aliwakataza masahaba zake kutumia mifupa na vinyesi vikavu vya ngamia kuchambia na akasema mifupa na vinyesi hivyo ni vyakula vya majini, na pia akatufundisha tuingiapo vyooni tusome dua ili kujikinga na majini waliomo vyooni.
Elimu ya kisayansi inatuambia kwamba katika mifupa na vinyesi vya wanyama kuna bakteria kibao ambao kama utatumia hivyo vinyesi na mifupa kuchambia utakuwa na nafasi kubwa sana ya kupata maambukizi katika njia ya haja kubwa halikadhalika chooni kulingana na mazingira yake kuna aina mbalimbali za bakteria wa maradhi mfano, Chorela, dysentery, hepatitis, kisonono nk, (hasa vyoo vya umma).
Hivyo mtukufu mtume (saw), aliposema neno "jinn" alikuwa na maana ya wadudu wadogo wasioweza kuonekana kwa macho ya kawaida na hapa nakubaliana na maneno yako ya kiarabu, na ili uweze kuwaona ni lazima utumie nyenzo maalumu kama darubini (microscope) au kwa maneno mengine uwe na maarifa (معرفة) kama ulivyosema.
Sifa kuu ya jinn ni kutokuonekana kirahisi kwa macho ya kawaida na mzizi wa neno "jinn" ni neno "janna" ambalo maana yake ni kutokuonekana, hivyo basi katika lugha ya kiarabu, kitu chochote au tukio lolote lenye sifa ya kutokuonekana kirahisi linawezwa kwa ki-SIFA likaitwa kwa jina la "jinn", na hii ipo karibu katika lugha zote hata katika kiswahili mtu shujaa anaweza kuitwa "Simba" kwa sababu tu ya ushujaa wake.
Kwa muktadha huo ki-sifa , jinn anaweza kuwa mtu mkubwa, kiongozi, tajiri, mtu mashuhuri nk--- ambao kwa hizo sifa zao kuonekana kwao mbele za watu huwa ni kwa nadra sana na inapotokea akaonekana basi lazima kuwae na jambo muhimu, na hapa ndipo Allah katika Qur'an aliposema; "Sikuwaumba majini na watu isipokuwa watuabudu"-- Majini waliotajwa hapa ni viongozi, watu mashuhuri, matajiri nk, ambao kwa umashuhuri na utajiri na uongozi wao wanaweza kujawa na kiburi kujiona kwamba wao hawastahili kufanya ibada, Watu katika aya hiyo ni watu wa kawaida wasiokuwa na utajiri, umashuhuri, uongozi nk ambao nao kulingana na hali zao za kimaisha wanaweza kusema ibada haiwahusu ila inawahusu hao waheshimiwa wakubwa (majini), ndipo Allah akakata mzuzi wa fitna akasema wote lazima tumuabudu hakuna adhuru.
Allah katika Qur'an anasema "Na majinni tumewaumba mwanzo kwa mwale wa moto," (sikumbuki aya). sayansi ambayo ni elimu kutoka kwa huyohuyo Allah inasema kwamba viumbe wa mwanzo kabisa kuumbwa walikuwa ni bakteria ainavya (Eukaryotes na prykaryotes. Check spelling) ambao waliumbwa kutokana na nuru ya radi (lightining sparks).
Qur'an katika Surah jinn, Majinn waliposikia Qur'an ikisomwa walisema, "hakika tumesikia Qur'an ya ajabu inayoongoza kwenye uongofu"(sikumbuki aya) na tena wakasema; "hakika tumesikia kitabu kilichoteremshwa baada ya Musa"(sikumbuki aya), na baadaye mtume (saw) alikuwa akifanya maombi na hao majinn "wakamzonga/ wakamzingira" (sikumbuki aya). Majinn waliotajwa katika hiyo sura ni watu wageni wasiokuwa waarabu, katika lugha ya kiarabu neno "jinn" linaruhusiwa kutumika kwa mgeni/wageni kwa sababu mgeni anaonekana kipindi tu anapokuwa na wenyeji lakini yeye sio mtu wa hapo na hivyo kuonekana kwake ni kama kuonekana kwa "jinn" na hii ni katika matumizi yale yale ya Ki- sifa ya neno jinn--, na hao wageni walikuwa ni mayahudi kutoka Nasibin, ndiyo maana wakasema; "innaa sami'i'naa kitaaba unzila min baa'd Musa" (Hakika tumesikia kitabu kilichoteremshwa baada ya Musa).
Ugonjwa unaowashika kina mama na akina dada, (Hysteria), kama nilivyosema hapo awali kuwa neno "jinn" linaweza kutumika hata kwa jambo lenye sababu isiyoonekana bali athari inayoonekana (unseen cause but seen effects). Akina mama maranyingi husumbuliwa na ugonjwa wa akili ambao watu wengi huuita mapepo, majinni na hata Maruhani, mtu anayeshikwa na ugonjwa huo kutokana na sababu mbalimbali za ndani ya mwili na nje ya mwili anashindwa kabisa kujidhibiti (uncontroll) kiakili na hivyo wakati huo akili inajiendesha yenyewe (run amok), na mgonjwa anaweza kutamka maneno au hisia alizokuwa nazo kichwani kabla ya kushikwa na huo ugonjwa (ravings) au anaweza kutamka maneno katika lugha ngeni kabisa (labda aliisikia zamani alipokuwa mdogo kwani akili ni kama memory card), na watu wakashangaa na wakaanza kuhisi kwamba; "LAZIMA KUNA KIUMBE KISICHOONEKANA KWA MACHO KUTOKA NJE KIMEMUINGIA KICHWANI NDICHO KINACHOZUNGUMZA HIYO LUGHA"😁😁---- na hapo ndipo dhana na fikra za upotishaji juu ya majinn zinapoanzia hapo, kwamba majinni ni viumbe mithili ya watu na wanaweza kumuingia mtu kichwani na wanapenda kuishi chooni, kwenye milima mirefu, magogu, baharini, katika misitu minene nk, ilmradi kila mtu anatoa fikra zake anazojenga juu ya majinni, mbaya zaidi Waalimu na Masheikh Ubwabwa biashara ya kupunga majinn kwa akina mama imekuwa ni dili kubwa na Wachungaji pia hawako nyuma katika kukemea majini mapepo. Kifupi, hayo yanayoitwa mapepo, Maruhani, jinn, Mahaba nk, yanaweza kuitwa kwa jina la "jinn" kwa sifa tu kwasababu kitu kinachosababisha mama au dada ashikwe na hali ya kuweweseka haionekani kwa macho lakini madhara yake yanaonekana kwa mgonjwa, hakuna jinn mahaba, Subiani, Affrit nk, mwenye umbo la mtu kutoka nje anayemuingia mtu, hakuna, never ever there is none.
Kutupiwa "jinn"--- unaweza kusikia watu wakisema, mfano; " Jamaa katupiwa "jinn" ndiyo maana kapata ajali, naam-- zipo elimu za "spirits", mfano, Telepathy, Hynotism (mesmerism) nk, ni elimu ambazo baadhi ya watu wanazaliwa nazo naturally au kwa kujifunza, ni elimu ambayo mtu anaweza kumuathiri mtu mwingine kwa kufanya baadhi ya mambo fulani na mtu akaathirika hata akiwa maelfu ya kilometres na mtu akaathirika huko alipo, nalo jambo hili waweza kuliita "jinn" kwasababu tu nguvu inayotenda kazi haionekani kwa macho, lakini si kwamba kuna kiumbe mfano wa mtu au watu kinaruka hewani baada ya kutumwa na "fundi" kwenda kufanya madhara kwa mlengwa.
Majini kuumbwa kwa moto, naomba nimalizie kwa kutoa ufafanuzi wa maana nyingine ya jinn kuumbwa kwa moto, mtu au kitu kuumbwa kwa moto maana yake pia yaweza kuwa ni mtu mwenye kiburi, majivuno, mwenye asili ya ukali nk, kama alivyokuwa Firauni na Ibilisi katika Qur'an.