Kila jambo lina mwisho wake.
Kuna waliokuwa wanazijua dhulma hizi kwa miaka mingi sana na kutahadharisha serikali.
Dhulma kwa Waislam si agenda mpya hata kidogo.
Wengi tulioitahadharisha serikali tulipuuzwa na kupewa majina kadhaa si haba.
Siasa kali, mujahiduna nk.
Maneno haya hapo chini nimeandika miaka mingi sana iliyopita hebu yapitie kwa kujikumbusha ikiwa ulipata kuyasoma:
"Baada ya kupatikana uhuru, Kanisa lilipohisi wasiwasi, limeweza kwa urahisi kabisa kuwazuia na kuwadhibiti Waislam. Serikali imeweza kutumia nguvu iliyokuwanayo katika kudhibiti siasa kuzuia harakati za Waislam kudai fursa sawa na Wakristo katika kugawana madaraka katika serikali. Kanisa limehakikisha kuwa kupinduliwa kwa ukoloni si kizingiti kwa Ukristo, ingawa ingetegemewa kuwa Kanisa lingeathirika kwa kuanguka kwa ukoloni. Katika miaka yake zaidi ya mia moja, Kanisa lilikuwa limestarehe kama muokozi wa nafsi na watu wenyewe. Kanisa lilikuwa salama na halikupambana na msukosuko wowote kutoka kwa serikali kwa kuwa lilikuwa Kanisa ndilo lilishika hatamu ya serikali. Baada ya kueleza hayo yote ni muhimu sasa kuangalia jinsi ukereketwa wa Kikristo unavyofanya kazi katika serikali na jinsi kazi hiyo inavyoathiri Uislam.
Wizara ya Elimu inachukuliwa kama mfano kwa sababu ya umuhimu wake katika jamii. Katika wizara hii, inaweza kuonekana kwa uwazi kabisa jinsi Ukristo unavyofanya kazi na jinsi udini ulivyoshamiri katika kugawa nafasi muhimu kati ya Waislam na Wakristo. Ilikuwa katika wizara hii katika historia ya Tanzania ndipo kwa mara ya kwanza waziri Muislam alipochaguliwa kuongoza wizara, Kanisa likaingilia kati waziwazi kumpiga waziri vita na kuhoji nafasi nyingine za juu ambazo zilipewa Waislam.
Serikali haikuweza kupingana na Kanisa na waziri huyo, marehemu Profesa Kighoma Ali Malima aliondoshwa katika wizara hiyo. Mwaka 1987 Profesa Malima aliteuliwa kuwa Waziri wa Elimu akiwa Muislam wa kwanza kushika nafasi hiyo. Mawaziri 8 waliopita walikuwa Wakristo. Kulikuwa na malalamiko kutoka kwa Waislam kuwa wizara hiyo imegeuzwa jimbo la Wakristo, hasa pale padri alipoteuliwa na Julius Nyerere kuongoza wizara hiyo. Profesa Malima aliposhika wizara hiyo aliona upo umuhimu wa kufanya marekebisho kadhaa ili kurejesha imani ya Waislam katika serikali na wizara hiyo. Kulikuwa na tuhuma kuwa Wizara ya Elimu ilikuwa ikiwabagua vijana wa Kiislam kupata nafasi katika vyuo vya elimu ya juu na ilikuwa ikizuia kupanda vyeo kwa Waislam.
Profesa Malima alipoona dhulma ile iliyokuwapo katika wizara ile dhidi ya Waislam, Profesa Malima aliwateua Waislam 4 kushika nafasi katika kurugenzi mbalimbali na akaandika taarifa ya siri kwa Rais Ali Hassan Mwinyi kumtaarifu udini alioukuta katika wizara ile. Katika taarifa ile kwa rais, Profesa Malima alieleza kuhusu kudumazwa kwa Waislam katika mgao wa elimu. Taarifa hii ilivuja kwa vyombo vya habari na kwa Wakristo wengine. Katika watu walioipata taarifa hii ni Rais Mstaafu Julius Nyerere wakati ule akiwa Mwenyekiti wa chama tawala CCM."
Kutoka kitabu: "Maisha na Nyakati za Abdulwahid Sykes…"