5
Waziri wa Afya alipofika hospitali alishangaa kumuona baba yake Kay. Baba alieleza kwamba alikuwa akiishi na binti yake, lakini tangu Jumapili, Kay alipotea. Alijaribu kwenda kumtafuta kwa Dr. Mbalu Mkasa ambako alikutana na taarifa za kifo cha daktari huyo. Baada ya mazungumzo mafupi, Waziri aliachana naye.
Waziri alirudi nyumbani. Ilipofika saa kumi na mbili jioni, mke wa Waziri, Teresa, aliyekuwa mfanyakazi wa Hospitali ya Mulago alirudi nyumbani na taarifa mpya. Alimweleza mumewe kwamba alipokea mwili wa mwanamke ukiwa umetenganishwa viungo na alielezwa ulikuwa mwili wa Kay Amin. Waziri kwa mshituko, alimpigia simu Amin na kumweleza kuwa alikuwa na taarifa muhimu. Waziri alikwenda moja kwa moja mpaka Ikulu. Alikuwa akitetemeka na alisema, “Mheshimiwa, mke wako amefariki, na mwili upo katika hali mbaya.” Amin hakushtuka, aliuliza taratibu, “Nini kimetokea?” waziri akajibu, “Mwili umegawanywa vipandevipande!” Amin akasema, “Umefika?” Waziri akajibu, “Hapana,” Amin akamaliza kwa kusema, “Nenda ukaone kisha unipe taarifa.”
Waziri wa Afya alikwenda mpaka hospitali, mochwari ikafunguliwa akisindikizwa na watumishi wawili. Walifungua jokofu mojawapo ambamo mwili ulihifadhiwa. Jokofu likafunguka na mwili ukaonekana. Waziri hakuwahi kushuhudia alichokiona, mwili ulikuwa wa Kay Amin, lakini umetenganishwa vipandevipande. Miguu na mikono ilikatwa. Kiwiliwili hakikuungana na kichwa na ilitengeneza picha ya kutisha! Zoezi la kukata viungo vya Kay lilifaywa kwa utaalamu wa hali ya juu. Hakuna mfupa uliovunjwa, maungio yalikatwa vyema, kila kitu kilikuwa sawasawa. Kwa vyovyote, kazi hii ilifaywa na mtaalamu aliyebobea tena akitumia vifaa sahihi vya upasuaji. Waziri aliyekosa neno la kusema, alirudi hatua mbili nyuma akaagiza jokofu lifungwe.
Waziri alikaa dakika chache ili kutuliza kichwa kwa kile alichokiona, kisha akaendesha gari mpaka makazi ya Amin, ‘Nakasero Lodge’. alimweleza yote aliyoyaona, Amin hakushangaa, akasema kwa sauti tulivu, “Imekuwa hivyo? Nenda nyumbani sasa.”
Usiku huohuo Amin aliagiza miguu ya Kay ishonwe katika mwili ili kesho watoto waje kuuona mwili wa mama yao. Siku iliyofuata, agizo la Amin lilitekelezwa.
Mwili wa kay ulilazwa kitandani na kufunikwa mpaka kidevuni. Saa tano asubuhi, kwa amri ya Amin, baba yake Kay na watoto watatu wa Kay umri kuanzia miaka mitatu mpaka nane walipelekwa hospitali. Amin naye akafika. Kisha, mbele ya Kamera za Televisheni ya Taifa na waandishi wa habari waliokuwa kazini, waliingia kuuona mwili. Amin hakuwafariji wafiwa. “Mama yenu alikuwa mwanamke mbaya,” aliwafokea watoto. “Tazameni kilichompata!”
Inaendelea...
Soma:
Jinsi ya Kuandika CV na Barua ya Maombi ya Kazi