JamiiTalks
JF Advocacy Team
- Aug 7, 2018
- 685
- 1,124
Kifungu cha 9 cha Mkataba wa Afrika kinalinda haki ya uhuru wa kujieleza na kutoa maoni:
1. Kila mtu atakuwa na haki ya kupokea taarifa.
2. Kila mtu atakuwa na haki ya kujieleza na kusambaza mawazo yake kwa kuzingatia misingi ya sheria. Tume ya Haki za Binadamu na Haki za Watu ya Umoja wa Afrika (ACHPR) ina wajibu wa kufasiri Mkataba huo.Tume hiyo imekuwa ikitekeleza wajibu huo kwa namna, ikiwemo njia ya kutoa Maazimio na Matamko.
Maazimio na Matamko ya Msingi ya ACHPR:
Azimio Kuhusu Haki ya Uhuru wa Taarifa na Kujieleza Kupitia Teknolojia ya Intaneti Barani Afrika (lilikubaliwa Tarehe 4 Novemba 2016): Nchi zilizoridhia Mkataba wa Afrika hazina budi kutunga sheria zitakazohakikisha kupatikana, kuheshimu na kulinda haki ya wananchi ya uhuru wa taarifa na kujielezakwa kupitia teknolojia ya intaneti.
Azimio Kuhusu Usalama wa Waandishi na Watendaji Wengine wa Tasnia ya Habari (lilikubaliwa Tarehe 12 Mei 2011): Nchi (na mamlaka zake husika) zilizoridhia Mkataba wa Afrika hazina budi kutekeleza wajibu wao wa kuzuia na kuchunguza matukio yote ya uhalifu dhidi ya waandishi au watendaji wengine wa tasnia ya habari na kuwashughulikia wahusika wote waliofanya vitendo hivyo kwa mujibu wa sheria.
Pande zote zinazohusika kwenye mapigano au migogoro inayohusisha matumizi ya silaha zina wajibu wa kuheshimu uhuru wa wanahabari kutekeleza majukumu yao ya kitaaluma, pia zina wajibu wa kuhakikisha usalama wa waandishi na watendaji wengine kwenye tasnia ya habari kwa mujibu wa sheria za kimataifa za masuala ya kiutu.
Azimio Kuhusu Kudorora kwa Uhuru wa Kujieleza na Kupata Taarifa Barani Afrika (lilikubaliwa Tarehe 26 Mei 2010): Nchi zilizoridhia Mkataba wa Afrika zina wajibu wa kutunga sheria ili kulinda haki ya uhuru wa kujieleza na kupata taarifa. Sheria hizo ni sharti ziongozwe na kanuni za kimataifa na zile za barani Afrika, zinazolenga kuzuia ukiukwaji wa haki hizi. Nchi zina
jukumu la kufanya uchunguzi wa ukiukwaji wowote wa haki hizi, hasa vifo vya waandishi wa habari waliowekwa kizuizini, na kuwafikisha wahusika kwenye vyombo vya sheria.
Tamko Kuhusu Kanuni Misingi ya Uhuru wa Kujieleza barani Afrika (lilikubaliwa mwaka 2002): Nchi zilizoridhia Mkataba wa Afrika zina wajibu wa kuhakikisha kupatikana kwa uhuru wa kujieleza nakupata taarifa, ambao pia unahusisha haki ya kutafuta, kupokea na kusambaza taarifa na mawazo ya aina mbalimbali kwa njia ya mdomo au maandishi, na bila ya kujali mipaka, kwa kuandika au kuchapisha, kwa njia ya sanaa, au njia nyingine yoyote atakayoichagua, hata kamani nje ya mipaka ya nchi. Tamko hili linafafanua misingi mbalimbali, ikiwemo:
Kuwapo kwa tasnia ya utangazaji habari yenye washiriki wa aina mbalimbali, vyombo huru vinavyomilikiwa na watu au taasisi binafsi, kuliko kuwapo kwa ukiritimba wa Dola (Serikali), ambao ni kinyume cha kuwapo kwa uhuru wa kujieleza.
Uwajibikaji wa vyombo vya utangazaji vya umma kwa wananchi kupitia muhimili wa kutunga sheria (Bunge), kuliko muhimili wautawala.
Mamlaka huru za udhibiti wa vyombo vya utangazaji na mawasiliano ya simu, zinazolindwa ipasavyo dhidi ya kuingiliwa kwenye utendaji wao kisiasa au kiuchumI.
Mtumo wa usajili wa magazeti na machapisho mengineyo usioweka vikwazo dhidi ya uhuru wa kujieleza.
Sheria dhidi ya kashfa zisizozuia usambazaji wa habari au taarifa zenye maslahi mapana kwa jamii.
Kulinda vyanzo vya habari au taarifa za siri isipokuwa katika mazingira maalum yaliyoainishwa.
=====#UhuruWaKujieleza=====
JamiiTalks
Upvote
2