Sheria ya Ndoa ya Mwaka 1971 imeruhusu mke akope fedha anunue mahitaji ya familia kama mumewe hatoi fedha za matumizi.
Kifungu cha 64 (1) cha sheria hiyo kinasema mke ana haki ya kukopa fedha kwa ajili ya matumizi ya kuhudumia familia kwa jina la mumewe na mume ana wajibu wa kulipa deni hilo.
Pia, sheria hiyo imeweka wazi kuwa mke ana haki ya kutumia fedha za mume wake zilizo mikononi mwake au kubadilisha mali inayohamishika ya mume kuwa fedha na kutumia fedha hizo.
View attachment 3699407 Wakili wa Ofisi ya Mawakili wa Kujitegemea ya Avis Legal, Henry Mwinuka alilieleza kuwa ikitokea mume bila sababu za msingi akaacha kuhudumia familia yake mke ana haki ya kuchukua mkopo kwa ajili ya kuhudumia familia tu na kwa kiwango ambacho fedha hizo zinahitajika kununua mahitaji muhimu kwa ajili yake na watoto wadogo wa ndoa yanayolingana na uwezo wa kifedha na mtindo wa maisha wa mume wake.
Mwinuka alisema kama mwanamke ataingia kwenye ndoa na madeni ya mkopo basi madeni hayo hayatahesabika kama madeni ya mume wake bali ni madeni yake mwenyewe. “Ikiwa mwanaume hahudumii na hana sababu ya msingi ya kutohudumia mke na watoto mke anaweza kwenda kukopa kwa jina la mume na deni hilo litachukulia kuwa ni la mwanaume na atapaswa kulilipa,” alisema.
Aliongezea “Madeni yale ambayo mwanamke ameingia nayo kwenye ndoa hayo mwanaume hayamuhusu yaani madeni yako ni yako haliwezi kuwa deni la mume wako”.
Mwisho akasema sheria hiyo inatambua mali za wanandoa kama mali zote zilizopatikana kihalali ikiwemo nyumba, shamba, magari, kiwanja, kampuni, biashara na mali nyinginezo
Source; Habari Leo