SEHEMU YA 53
Siku kadhaa zikapita na mume wangu akatakiwa kurejeshwa nyumbani, na kabla ya kurejeshwa nyumbani, docta aliyekuwa akimuhudumia, akaniita ofisini kwake, na kunishauri mambo mengi ili kuhakikisha mume wangu anaondoka kwenye hatari na kupona mapema.
'Unasikia wewe ni mke wake, na mtu muhimu kwake, wewe ndiye utamfanya apone haraka au....unasikia, muhimu tena sana,jitahidi kuwa karibu sana na mume wangu, na kukwepa kauli yoyote ya kumkwaza...unasikia...'akasema docta akinisisitiza hilo sana
'Nakusikia docta...'nikasema
'Mume wako, yupo kwenye hali ambayo akipata mshtuko tu inaweza kuzua tatizo kubwa ambalo litamfanya ashindwe kutembea kabisa....na ukijitahidi akawa hana mawazo, mazoezi...na kufuta masharti nilikuambia awali, ...atapona haraka tu...'akasema docta
‘Sawa docta mimi nitajitahidi kadri ya uwezo wangu, maana huyo ni mume wangu, sina jinsi…ila nimegundua kitu, hivi sasa ni mbishi sana, na ubishi huu hakuwa nao , nahisi umeanza baada ya hili tatizo, kila kitu anataka nimsikilize yeye tu, sasa sijui nikiwa naye huko nyumbani itakuwaje...’nikasema.
‘Ndio hivyo, jitahidi uwezevyo, kama kweli unamjali mume wako na unataka apone haraka, basi acha kila kitu kwa ajili ya mume wako …’akasema docta
'Sawa docta...'nikasema
Kabla ya kuondoka hapo hospitalini baba akanipigia simu, baba siku hizi amekuwa kila mara akinipigia simu , hasa baada ya kushuhudia nikipoteza fahamu hapo hospitalini, tukio hilo limemfanya awe karibu na mimi, kuliko alivyokuwa baada ya mimi kuolewa..;
‘Vipi hali yako na ya mume wako…?’ akaniuliza
‘Hajambo jambo, kama walivyokuwa wamesema leo tunaweza kuondoka naye…hapa tu, tupo nje tunataka kuondoka kurudi nyumbani..’nikasema
‘Ok, vizuri…sasa ok, naaah, umefikiriaje wazo langu..?’ akaniuliza kwa lugha ya upole, sio tabia ya baba akiongea na mimi, hasa nilipolazimisha kuolewa na mume ambaye hawamtaki.
‘Baba mengine yasubirie kwanza, ngoja nibebe hili jukumu la mume wangu maana nimejitakia mwenyewe, na sihitajii msaada kwenu baba, nitajimudu mwenyewe…’nikasema
‘Usiwe mkaidi kwa hilo, hilo ni tatizo kubwa sana, kama unafikia kupoteza fahamu, sio kitu kidogo hicho, sisi wazazi wako hatuwezi kukaa kimia, na mama yako atakuja akae nawewe, tuone jinsi gani ya kukusaidia, unasikia…’akasema
‘Baba hapana, mama mwenyewe mbovu, tutazidi kumchosha tu bure, nakuomba hilo liacheni kama lilivyo, ikibidi nitawaambia…’nikasema
Kila nikiombea na baba ni lazima akimbilie kwenye lawama, akasema;
‘Nilishakuambia huyo mwanaume hakufai, atakuhangaisha mwishowe atakuepeleka kubaya, utaumwa, unaweza hata kupooza mwili, mwishowe utaingia kaburini, wenzako wanastarehe..kitu ambacho kinatuuma sana sisi wazazi wako...'akasema
'Baba...'nikataka kujitetea lakini hakunipa nafasi akaendelea kuongea
'Nikuambie ukweli mume wako halijali hilo, la afya yako,... yeye anachojali ni masilahi yake tu, na anataka akukamue mpaka basi,..na sasa hivi utayaona hayo, hatukuombei mabaya, lakini yale tuliyowahi kuyasema sasa utaanza kuyaona kwa macho yako,..huyo mume wako atakusumbua sana...'akasema
'Baba lakini ni mume wangu...'nikasema
'Sawa..ni mume wako,....ngoja tuone itakavyokuwa,….ila ukikwama usiache kutuambia, mimi nitajitahidi kufika kwako mara kwa mara, kulifuatilia hili mimi mwenyewe…’akasema
‘Baba nashukuruni kwa kunijali, lakini nakuomba usisumbuke sana kwa ajili ya hili, sasa hivi mume wangu anaumwa, na naona akikuona wewe anakuwa hana amani, kwa hivi sasa, anahitajia, huruma, na baba sio kwamba sitaki ufike, ila ukifika naomba sana baba usije kuzungumza maneno ya kumweka kwenye wakati mgumu, ongea naye maneno ya kumfariji, asiogope, kama alivyotushauri docta...’nikajaribu kumtetea.
'Hilo sio la kunifundisha, nafahamu sana,...muda utafika nitapambana naye, sio sasa..usiwe na wasiwasi kwa hilo...'akasema
'Nashukuru sana baba...'nikasema
‘Ila kuna kitu nataka uniambie, siku ile nilipofika hospitalini nilisikia akiongea maneno, kama anakuomba msamaha, na akasema kitu kama wewe ulikuwa humjali kitu kama hicho, sikusikia vyema, alikuwa akiongea nini..?’ baba akauliza
‘Baba , ....mgonjwa alikuwa anaongea hivyo ni katika hali ya kuchanganyikiwa tu, kwasababu ya huko kuumwa, yeye alijiona kama ni mtu wa kufa tu, kwahiyo ndio akawa anajaribu kujitakasa, akihisi hili kakosea, basi anaomba msamaha, hata wewe ungelikuwepo angalikuomba msamaha ni katika kuhangaika tu baba…’ nilisema sikuelewa baba alisikia kiasi gani, na docta akawa anaongea baadae akasema
‘Vyovyote iwavyo mimi nataka maelezo,..najua kakuoa akiwa na malengo yake binafsi,..yeye kama hawezi kuishi na binti yangu labda ana mipango yake mingine au alikuwa na ndoto zake nyingine , basi awe muwazi tu, nimegundua mambo mengi ambayo hayafai kwa familia yangu…’akasema
‘Baba mengine ni ya kuharibu bora tuyapuuze tu..’nikasema
‘Sikiliza…anyway,a sitaki nikuumize kwa mawazo, hayo ni yake anatakiwa kuwajibika nayo, sasa.. ngoja apone, sawa poleni sana binti yangu, usijali mimi nitapambana na hili jambo mpaka nione mwisho wake, unasikia, usijali, nipo pamoja na wewe, …’akawa anaongea hivyona kipindi hicho ndio nimepata fahamu.
‘Baba, usiwazie hivyo…mengine yametokea tu, ile iwe sababu , mimi nina imani yatakwisha tu, ni sehemu ya changamoto za maisha, sasa nyie kama wazazi wangu sitaki mnitenge mimi tofauti na mume wangu, ….sipendi hivyo baba…’nikasema
‘Binti yangu usione nasema hivyo, sisi wazazi wako tunakupenda sana, lakini tunaumia, tunajitahidi kadri tuwezavyo ili uondokane na shida hizi, lakini wewe unakuwa mkaidi, sisi tunafahamu tatizo lipo wapi, hich ni kizalia , asili ya hulka ya mtu, hutaweza kumbadili mume wako, abadani…’akasema na mimi nikataka kuongea lakini hakunipa nafasi, akasema
‘Mengi tunayaona lakini hatusemi, lakini kwa hili, hapa lilipofikia, sisi kama wazazi tutalifuatilia mpaka tuone mwisho wake ni nini, ina maana gani ya ndoa eeh, niambie…, na kama nilivyosema awali, sitaki kashfa katika familia yangu…, na anyway, wewe angalia afya yako, unasikia, kama kuna lolote linahitajika niambie….’alisema .
Na leo ndio akanipigia simu akitaka kujua mimi nimefikia wapi, kwani anahitajika kutoa maamuzi kwenye kikao cha wakurugenzi, ..anasema hicho kikao ni muhimu , hata kama mimi sitakuwepo au mume wangu, maamuzi ya wengi yataheshimiwa.
‘Baba mimi naomba usifanye lolote kwenye kampuni ya mume wangu, utoe hija kuwa kwa upande wa hiyo kampuni tusubirie kwanza, …itakuwa sio vyema, hata kama inafirisika, …na madeni yabakie tu, kama wadaiwa wanataka kushitaki waache tu wafanye hivyo, tutapambana huko mahakamani…’nikasema
‘Sio rahis hivyo binti yangu…mimi kama mwenyekiti wa makampuni yote, siwezi kukubali hali hiyo ifikie huko, kuna wakurugenzi wa hisa kwenye hiyo kampuni, wananihoji,…wamewekeza pia huko, unataka niwaambieje…wewe sikiliza, wewe endelea na mume wako, mengine niachie mimi, ninajua ni nini cha kufanya, unasikia eeh,…tuliza kichwa chako, ila mume wako akipona nataka nipambane naye mimi mwenyewe, …hilo sitaki majadala…’akasema
‘Baba…’nikalalamika
‘Kwahiyo leo mimi sitakuja huko , nitakuwa na kikao, na nitakuwa napitia taarifa za uchunguzi, kuhusu mume wako, kuna mengi yamegundulikana, lakini mengine sitaki yawepo kwenye hiyo taarifa, ni aibu, uliweza kuisoma ile taarifa niliyowahi kukupatia ile kila kitu kipo, na mengi ambayo siamini...hebu nikuulize kwanza huyo rafiki yako kwanini kasafiri na mtoto mchanga..?’ akaniuliza
‘Ilibidi afanye hivyo kwa vile muhula wa masomo umeanzia hapo, na hakutaka kusubiria, tukaona ni bora tu aende….na huko kuna watu watamsaidia hatapata shida…’nikaongea kujifanya na mimi nimehusika kwenye maamuzi ya rafiki yangu kuondoka.
‘Una uhakika,…??... sio kuwa kakimbia,…?? anaogopa ukweli ukija kugundulikana awe keshajipanga vyema kimaisha, binti yangu hao watu wanakutumia vibaya, huyo rafiki yako, anataka ahakikishe hata likitokea jambo awe anajiweza mwenyewe..sawa sio mbaya, lakini kwanini aharibu nyumba iliyombeba..’akasema
‘Baba hayo mengine hata sitaki kuyafikiria kwanza,…’nikasema
‘Sawa sawa, usijali…nitapambana na hao watu mimi mwenyewe, ilimradi…’akasema na kukata simu.
**********
Mume wangu akawa hataki mimi niondoke karibu yake , ikawa ni kero, ina maana nisitoke au kwenda mbali na yeye, hata akija mgeni, anataka atoke awe pembeni nikiongea na mgeni,..kwa maagizo ya docta nikawa nafanya kila atakavyo, ila moyoni, pamoja na huruma kila nikiwazia hayo yanayosemwa nilimuona mume wangu kama sio yule ninayemfahamu.
Nilitaka niwe na nafasi ya kuipata ile taarifa aliyotayarisha rafiki yangu, lakini sikutakiwa nisome mbele ya mume wangu,..ikafika muda nikaagiza niletewe hiyo taarifa nyumbani,…lakini muda gani wa kuisoma nikawa sina,
Ikatokea siku moja mume wangu amelala kutokana na madawa nilikuja kugundua akinywa hizo dawa anaweza kulala hata saa nzima au zaidi..na siku hiyo ilipoletwa hiyoo taarifa ya rafiki yangu, nikaona nitumie huo mwanya..., ndio nikaanza kuipitia hiyo taarifa ni ndefu kidogo...;
Taarifa ya uchunguzi wa ajali ya mume wangu, aliandika jina la mume wangu, na akaelezea ilivyotokea, kuwa ni sababu ya mwendo kasi, katika kukata kona akakutana uso kwa uso na lori,..akajaribu kulikwepa, na gari likapinduka na kugeuka mara mbili…
Dereva aliwahi kutoka, hapo haijulikani aliwezaje kutoka katika hali hiyo, ni kwa uwezo wa mungu tu.
Je kipindi ajali hiyo inatokea mlengwa alikuwa katokea wapi, taarifa inasema alitokea kazini, akapitia sehemu za wateja wake, ndivyo alivyoaga kazini, lakini akiwa kwa wateja wake, akaamua kwenda sehemu nyingine …(yawezekana,) akaandika hivyo na kuzungushia hayo maneno,...
Kuna kauli za watu kuwa kwa muda huo ndio alimua kwenda kumuona mzazi, huyo mzazi ni nani, (bado sijamtambua)!.
Hili la mzazi halina uzito, ila limetokana na maelezo ya siku kadhaa nyuma kuwa aliondoka kazini akisema anakwenda kumuona mzazi, hospitalini, huyo mzazi hospitalini hakuweza kugundulikana ni nani..(kwahiyo ili kupata jibu kamili, aulizwe yeye mwenyewe)!
'Ssshti...'nikajikuta nikisema hivyo.
Kabla hajapatwa na ajali, gari lilisimamishwa kwenye geraji, sehemu ambayo pia panaoshwa magari kwa pembeni yake..., na wakati gari lake linafanyiwa usafi, yeye alikwenda mgahawani, kupata chochote,..lakini hakunywa kilevi…akiwa hapo, inaonekana alipokea simu , ya haraka, na kutoka hapo akaenda kulichukua gari kuwa muosha magari,
Muosha magari anasema ni kweli, aliwahi kuosha gari la mtu huyo, na ...hata la mdogo wake, na anachokumbuka, yeye, mlengwa, aliondoka hapo kwa mwendo wa kasi, lakini sio kasi kubwa, kama ilivyokuwa huko alipopatia ajali... ila alionekana ana haraka, hata chenji ya pesa yake hakuichukua.
Kwahiyo hapo akahitimisha kuwa,.simu aliyopigiwa inaonyesha ilikuwa na jambo, la kumfanya aharakishe kufika nyumbani na sivyo kama watu wanavyosema kuwa huenda alikuwa akikimbia jambo la hatari, hata hivyo bado haijafahamika simu hiyo ilitoka kwa nani, na kwanini aliharakisha hivyo (haijafahamika bado). Na huyo aliyefika kwake ni siri yake...akaandika hivyo!
‘Hii taarifa haina maana kabisa..’nikasema ni kuiweka pembeni.
Na wakati nawazia hiyo taarifa : huyo mzazi ni nani huyo au ni nani huyo alimpigia simu mume wangu na kumfanya awe na haraka kihivyo, ndio akaja docta rafiki, akanikuta nipo kwenye mawazo, akaniuliza kuna nini kimtokea…
‘Mambo ya kazi tu…na nilikuwa naipitia ile taarifa aliyoacha rafiki yangu, lakini hakuna alichokifanya, sio kawaida yake, ni taarifa ya mtu ambaye hajui kazi kabisa, sio yeye aliyeitayarisha…’nikasema
‘Hiyo taarifa ina muhimu gani kwako kwa hivi sasa…?’ akaniuliza
‘Bado nawajibika kuufahamu ukweli, najua baada ya hili, mume wangu akipata nafuu, nitahitajika kukaa kikao na baba, na wawekezaji wengine, kuna maswali mengi nitaulizwa, nitayajibu vipi kama siufahamu ukweli..’nikasema
‘Ukweli kuhusu mumeo au ukweli kuhusu maswala ya kikazi…ama kuhusu mume wako yeye alishakuambia kila kitu, sasa kama hayo yanaweza kuingiliana na kazi yake, ni jambo jingine linaelezeka... kwa hivi sasa mimi siioni kwanini unabeba mzigo kabla haujatua kichwani mwako…utachoka hata kabla hujahisi uzito wake, tulia kwanza..’akasema
‘Unajua siwezi nikaamini yale aliyoongea mume wangu moja kwa moja, na hakuwahi kusema ni kitu gani alikifanya, mpaka afikie kuniomba msamaha..tunahis tu..pale aliongea akiwa kachanganyikiwa, sawa yawezekana ni hilo kuwa kafanya madhambi…lakini mbona taarifa ya rafiki yangu haijabainisha hilo. Sawa naweza kuhitimisha hivyo kuwa ni kweli, labda ni kweli, je hilo latosha tu, hapana ni lazima niwe na ushahidi....’nikasema
‘Nikuambie kitu hiyo taarifa ya rafiki yale lengo lake ni kuvuta muda, kuhakikisha kuwa anakuchanganya ili yeye aweze kutimiza haja zake,..na huyo mzazi mume wako aliyewahi kuaga kuwa anakwenda kumuona, sio mwingine ni huyo huyo rafiki yako, amini usiamini huo ndio ukweli….’akasema docta
‘Sawa, tunaweza kusema ndivyo hivyo, haya nipeni ushahidi, hapa anasema mdogo wake siku hiyo alifika pia kuosha gari,...swali gari lipi, na muda gani, hajaelezea hapa…kama kweli ni yeye, maana kama ni kweli, basi, huyo sio rafiki yangu ninayemfahamu mimi...'nikatulia kidogo.
'Mimi sio mjinga wa kukataa kauli za watu...najua nahisi hata mimi hivyo hivyo, ….lakini siwezi kukubali hivi hivi tu, na kuchukua hatua hiyo kubwa niliyodhamiria moyoni, maana ni kweli nitafanya hivyo,...je nichukue haua hiyo bila ya kujirizisha, ushahidi, upo wapi, unanielewa hapo,…au wewe unao huo ushahidi.?’ nikauliza
‘Kwasababu rafiki yako anajua kafanya makosa, anajua yeye alishirikiana na mume wako kulifanikisha hilo, ...'akasema
'Ushahidi...'nikasema
'Ndio tunaweka nadharia hii sawa,...kuna kitu nataka unielewe, kuwa huenda rafiki yako, alipanga hivyo, au kuna kitu kilimsukuma kufanya hivyo, na kitu hicho akakitumia kama ngao yake, lakini yanayokuja kutokea sasa imekuwa kinyume na alivyotarajia, ndio maana kaamua kukimbia ili kuepusha shari, naanzia hapo…’akasema docta.
‘Mimi nataka ushahidi maana baada ya huo ushahidi, mimi nitachukua hatua kali, hutaamini, na sitaweza kurudi nyuma kwa hilo..bila kujali ni nani, sitak nadharia za kuhisi hisi, wewe ni docta, au... …’nikasema
‘Sasa hebu nikuulize utachukua hatua kwa nani, kwa mumeo au kwa huyo rafiki yako...maana kam ni kutenda kosa wametenda wote, ?’ akaniuliza
‘Ndio maana nataka ushahidi..na nikiupata huo ushahidi…, sitaojali kuwa ni mume au rafiki yangu, yoyote ataumia,…na kila mtu ataumia kutegemeana na kosa lake yeye mwenyewe, wewe ngoja utaona nitakachokifanya…’nikasema
‘Kwa maelezo ya mume wako, wewe ulishirikiana na rafiki yako kulifanikisha hilo, sasa sijui kwa vipi, yeye kadai kuwa wewe ulimtuma, afanye hivyo ni kweli si kweli, ulisikia mwenyewe akiongea pale hospitalini, …’akasema docta, kama ananiuliza
‘Mimi nina kichaa!!!…hahaha, hivi kweli inaingia akilini hiyo, mimi nimtume rafiki yangu akazini na mume wangu, hata wewe unaweza kuliamini hilo…?’ nikauliza
‘Ili kuweza kulijibu hilo, labda nikuulize wewe, je hamkuwahi kukaa na rafiki yako mkapanga kuwa labda rafiki yake ajitahidi kupata mimba, kwa...sio lazima useme kwa mume wako, kwa yoyote, labda yeye akaona kwa mume wako, au...hatuna uhakika bado hapo, nasema hivyo kukuuliza wewe...?’ akauliza
‘Wewe uliwahi kuongea na rafiki yangu akakuambia hivyo...?' nikauliza
'Hapana, baada ya kujifungue amekuwa makini sana, hata nikiongea naye ahataki nimuulize chochote,...'akasema
'Sasa umelitolea wapi hilo, kuwa mimi nimtume rafiki yangu akazini na mume wangu, au sio…ndio una maana hiyo, kuwa mimi nilimshauri hivyo, na ...yeye akaona kwa mume wangu ndio kwenye usiri ..huo ni ujinga haliji akilini kabisa, rafiki yangu mwenyewe, sawa na ndugu yangu aje kufanya hivyo...ingelikuwa wewe ungelifanya hivyo kweli hebnu jiulize kwanza kabla ya kutoa nadharia yako?’ nikauliza
‘Yawezekana mlikaa mkaongea kwa namna ambayo aliona akifanya hivyo haitaleta walakini, lakini sio kwa moja kwa moja kuwa akafanya hivyo kwa mume wako, yawezekana ushauri wako,..ndio uliomsukuma kufanya hivyo labda…’akasema
‘Hakuna kitu kama hicho,..kama kweli yeye ni rafiki yangu ananijali na kujali masilahi ya familia yangu, asingeliweza kufanya kitu kama hicho, yeye anafahamu mambo mengi ambayo kama mimi, au mume wangu akiyafanya hakutakuwa na huruma kwa baba, hilo analifahamu, na anamfahamu sana baba yangu, ..ndio maana mimi siamini kuwa kafanya hivyo, ndio maana nataka ushahidi, baba anauhitajia pia huo ushahidi.., …’nikasema
‘Baba yako keshajua hilo, kuwa huenda huyo mtoto wa rafiki yako kazaa na mumeo,a u mdogo wa mume wako, keshaniulizia hilo, akataka ushauri wangu kama docta , mdogo wa mume wako, hataki kusema ukweli, ukiongea naye, unaweza ukahisi ndio yeye, kwa jinsi anavyojiuma uma, lakini lengwa mkubwa ni mume wako, unahisi ni kwanini...?’ akauliza
‘Baba taarifa alizo nazo ni kama nijuavyo mimi..bado anafuatilia, kasema kama ni kweli, basi, na yeye atakuwa na maamuzii yake, mimi sitaki kusimamia mambo ya wazazi wangu maana nafahamu hukumu yao ni nini…mimi nina namna yangu ya kuhakikisha hao watu, kama ni kweli, wanapata kitu ambacho hawataweza kukisahau maishani mwao…’nikasema
‘Hebu niambiea ukweli wako..utachukuaje hukumu, wakati labda na wewe unahusika, ni kwanini hutaki kusema ukweli kuwa wewe na rafiki yako mlikaa mkakubaliana jambo fulani..?’ akauliza
‘Hata kama tulikaa tukaongea tukajadili mambo, lakini tunakaa sana, tunaongea sana, lakini sio kwa ….hapana, siwezi mimi na akili zangu nimwambie akatembee na mume wangu, na yeye...'mara kukawa kama kuna sauti, nikahisi huenda ni mume wangu, lakini kwa hizo dawa, bado atakuwa kwenye usingizi.
'Anaweza kufanya hayo kwa malengo fulani, au ...kutokana na jinsi mlivyoongea, mimi sijui....na kama anafahamu kuwa kitu kama hicho kikitendeka, yaweza kuharibu kabisa ndoa yako, au..mimi sijui, ...ni kwanini afanye...huoni kuwa kuna kitu ndani yake, na baba yako ndio anakitafuta...'akasema
‘Mimi sijui, ila nijuavyo, baba hataki kashfa, hatua ya kwanza ambayo nahisi ataanza nayo, akiugundua ukweli, ni yeye kutoa hisa zake, na kujitoa kwa baba kwenye kampuni ya mume wangu, ndio kuiua , maana baba ndiye mdau mkubwa wa hiyo kampuni...'nikasema
'Na kuna madeni,...'akasema
'Ni kweli hata ukiangalia hii taarifa kampuni hiyo ina madeni, ya nje, baba mwenye anamdai pesa nyingi…je hao wanaodai wengine watalipwa na nani…kiufupi kampuni ya mume wangu haipo…na hili ni moja ya mambo yanayomuumiza mume wangu..nimemuambia baba, na sio hayo anayofikiria yeye,…’nikasema
‘Je baba yako alisemaje, hawezi kusaidia vyovyote..?’ akauliza
‘Kasema anaweza kusaidia iwapo, hakuna kashfa, kama kuna baya, kuna kshfa mbaya, kaifanya mume wangu yenye kutia dosari, familia yake hataweza kusaidia kwa lolote lile, na atajitoa, na kudai pesa zake zote, na atachukua hatua nyingine kubwa zaidi…’nikasema
‘Na wewe huwezi kusaidia chochote..?’ akauliza docta
‘Mimi, hahaha...siwezi, maana hata mimi kampuni yangu haifanyi vizuri..na tatizo ni kuwa kampuni ya mume wangu, inataswira fulani kwa wateja wangu pia, sijui kwanini, kuna wateja wangu wameanza kukimbia kisa ni kutokana na mwenendo wa kampuni ya mume wangu,.. unajua siasa za biashara zilivyo, kuna vita ya chni kwa chini, katika ushindani wa biashara, wateja wengine, hutafuta visa tu,…’nikasema
‘Je unahisi kilichotokea kwa mume wako ni sababu hizo za kibiashara, au kuna jingine limajificha…?’ akauliza
Nikaichukua ile taarifa, nikamuonyesha naye akaipitia halafu akasema;
‘Unaona sehemu zote alizoweka mabano kuwa haijakamilika ni zile ambazo zinamgusa yeye…na simu ya mume wako mmh, haiwezi kusaidia kitu, ...lakini itasaidia nini hapa, kuna mambo kayafunika kiaina, ila haya kuwa mumeo anadaiwa, kampuni haiwendi vizuri, kaongea ukweli, na kayachukua kama sababu kubwa, huoni ni kitu kama kimelengwa kinamna fulani..?’ akaniuliza
‘Simu ya mume wangu haijulikani wapi ilipo hata yeye anasema hakumbuki, huenda iliungua kwenye gari, au iliibiwa..na nimejaribu kuulizia watu wa mitandao kama wanaweza kunisaidia wamesema hilo ni vigumu kwao…’nikasema
‘Ulishaongea na huyu muosha magari, kuhakikisha kuwa huyo aliyeondoka hapo kweli alikuwa mume wako au ni mdogo wa mume wako, maana hapa kwenye taarifa ni kama kulikuwa na watu wawili, huyo hapa alikwenda kupata kitu mgahawani, na huyo aliyekuja kwa rafiki yako ni nani.?’ akaniuliza
‘Huyo muosha magari, hayupo…kasafiri, na hata simu yake haipatikani…’nikasema
‘Je sio mbinu za kumuondoa hapo Dar….hana jamaa yoyote anayemfahamu, tukajaribu kumfuatilia, nahisi hapa tunaweza kugundua kitu..?’ akauliza
‘Sijaweza kufuatilia kiasi hicho, nitategemea hili angalifanya huyo rafiki yangu, lakini ndio hivyo…kama unavyoona, hii sio taarifa ya mtu aliyesomea kazi hiyo, ni kama kaandikiwa na mwanafunzi wake..’nikasema
‘Huku kwenye maelezo, ya uoni wake, katupia lawama ndoa yenu kuwa inaweza ikawa sababu nyingine, unahisi kuna ukweli wowote hapa…?’ akauliza
‘Sizani, kama kuna ukweli, kwanini hilo lisitokee nyuma, lije litokee siku hiyo..nakiri kuwa mimi nina madhaifu yangu, lakini haijafikia hadi yatendeke hayo,…na ndio maana bado sijaamini..’nikasema
‘Hujaamini nini sasa hapo..?’ akauliza
‘Kuwa kwanza ajali hiyo inatokana na matendo ya nyuma, pili, hapa kuna matatizo ya mume wangu na kampuni yake kwa upande mmoja, na huku kuna huyo mtoto wa rafiki yangu, lipi lenye uzito, tatu.... rafiki yangu anahusikanaje na mume wangu kwenye kusababisha kampuni ya mume wangu kufikia hapo ilipo, maana baba kalisema hilo. ukiangalia kuna mkanganyiko, na kwanini mdogo wa mume wangu ananipiga chenga, unajua ananikwepa sana, huoni anaweza kuhusika kama sio yeye…’nikasema
‘Baba yako anasemaje kwa ujumla wake..?’ akauliza
‘Baba yeye hataki kusema lolote mpaka sasa, anasema kuna taarifa anaisubiria, akiipata ndio itampa mwanya wa kusema jambo, ila kaahidi kulifuatilia hili tatizo la familia yangu na kampuni zote, hadi mwisho wake, na kasema sasa hatarudi nyuma, …’nikasema
‘Atasamehe tu, nyie ni watoto wake,…maana vyovyote iwavyo, itasaidia nini sasa eeh, atamfukuza, atavunja ndoa yenu, unaonaeeh, hawezi, na ukiangalia kwa makini,.. kampuni ya mumeo ikifa, mumeo atakuwa anategemea ajira yake tu…ambayo haiwezi kumkidhi haja zake,..na nimesikia huko kazini kwake kuna matatizo pia ni kweli…?’ akauliza
‘Nimesikia sasa hivi na kusoma kwenye taarifa ya huyo mdada, nilikuwa sijui, kiukweli kuna matatizo,…sijui alifanya nini huko…’nikasema
‘Mdada hakuelezea hilo…mmh, hapa…ngoja nisome, anasema, alikopa pesa, na kujikopesha bila idhini,…mmh, kwanini alifanya hivyo, …hapa anasema bado uchunguzi unaendelea…sasa mume akifukuzwa itakuwaje na kampuni ndio hiyonayo inayumba…huo sasa ni mzigo wako ambao sizani kama utaweza kuubeba…’ akasema
‘Hilo sio tatizo kwangu, yeye ni mume, na mengi kajitakia yeye mwenyewe, lakini je hayo ndio yamesababisha hayo yote, hiyo ajali sabau ni hayo, au ...na mmh, bado kichwa changu kina giza, ?’ nikauliza
‘Jibu hasa la haya yote tutalipata kutoka kwa mume wako,... je atakubali kusema ukweli…?’ akauliza
‘Akipona, ni lazima asema ukweli, nitahakikisha hilo analifanya na nitajua la kufanya, wewe subiria tu…’nikasema
‘Lakini usije kuongea chochote kwa hivi sasa, wala kumuuliza..’akasema docta
‘Nafahamu hilo sana, hapa nipo kama mtumwa, kila analotaka nalifanya, kila kitu kimesimama, nitafanyaje, lakini kuna ukweli huo nautaka, ..hata kabla hajapona, nautaka niufahamu, je ni kweli kuwa mume wangu kazaa na rafiki yangu, nikiwa na uhakika na hilo, basi mengine yote hayana maana kwangu, ….mimi na baba tutakiwa hivi, …’nikasema nikishikisha vidole viwili kwa pamoja.
Nikashtuka kusikia mtu anakohoa nyuma yangu,, …nikageuka na kumkuta mume wangu akiwa kwenye kigari chake anatuangalia …akiwa anatokea huko alipokuwa amelala…nikamuangalia mume wangu, alionekana kakasirika kakunja uso..
‘Kwanini umefanya hivyo mume wangu…unatakiwa ulale, hizo dawa zinahitajia wewe ulale, unakwenda wapi sasa…?’ nikamuuliza lakini hakunijibu, akawa anakiendesha kigari chake na kuelekea nje
‘Kasikia nini…?’ akauliza rafiki yangu
‘Sizani….’nikasema, nikiwa sina uhakika.
‘Basi ngoja nikaongee naye,..na wewe hakikisha hiyo taarifa unaificha asije kuiona, pili, nataka tuje tuongee mimi na wewe baadae…nataka.., nikusaidia kulimaliza hili jambo, nitahakikisha unaufahamu ukweli wote, na ushahidi unaoutaka, ila uniahidi jambo…’akasema
‘Jambo gani…?’ nikauliza na mara mume wangu akawa ananiita huko nje..
WAZO LA SIKU: Maisha yalivyo, inafikia muda inabidi ukope, ili kukidhi haja fulani, ni muhimu tukikopa tujue jinsi gani ya kuja kulipa deni la watu, wengine hukopa tu, akisema tutajua huko mbele kwa mbele, na ukianza kudaiwa, unakimbia, unajificha au unajibu jeuri. Tukumbuke kuwa deni ni deni, na deni haliishi mpaka ulipe au mwenyewe kwa ridhaa yake akusamehe. Tusipende kudhulumu tukidaiwa, deni halitaondoka hata ukiondoka hapa duniani,..utaenda kulikuta huko kwa hakimu wa mahakimu.
Docta aliposikia mimi naitwa, akasema
‘Ngoja mimi nikaongee naye kwanza…’akasema na nilitaka kumpinga maana mume wangu kaniita mimi, ni wajibu wangu kuitika wito wake kwanza, lakini docta akaniwahi na kukimbilia huko nje alipo mume wangu, ikabidi nisubirie tu.
Nikiwa nimebakia pale peke yangu, niliweza kuipitia ile taarifa ya rafiki yangu kwa makini, na mpaka nafika mwisho nilianza kubadilika, kuwa huenda wanayoongea wenzangu yana ukweli fulani. Kwenye hii taarifa rafiki yangu alijaribu kama kuficha jambo, na kujihami kwa namna fulani, japokuwa haionyeshi wazi wazi kuwa kweli anahusika ..
Kwa maelezo ya taarifa hiyo, Muosha magari anasema aliosha gari la mume wangu, na pia la mdogo wa mume wangu kuonyesha kuwa wote wawili walifika hapo siku hiyo, lakini docta anasema mdogo wa mume wangu alikuwa kwake wakiangalia mpira,..je muda gani alitoka hapo na kwenda huko…. nikjiuliza.
Hapo nikaona kuna muhimu wa kuonana na mdogo wa mume wangu kwa haraka iwezekekanavyo, lakini nisingeliweza kuondoka hapo, nikachukua simu na kumpigia huyo shemeji yangu, lakini simu haikupokelewa.
‘Nitampata tu….’nikasema na muda huo docta akaingia akisukuma kile kigari cha mume wangu, na mume wangu alikuwa kakaa kinyonge, akitikisa kichwa kama kukubali jambo fulani kwenye maongezi yao..na walipofika ndani docta akasema;
‘Tumemalizana na rafiki yangu, …mimi nataka kuondoka…’akasema
‘Sawa mimi nipo na mume wangu, sikusindikizi…’nikasema
‘Ni wajibu wako, lazima mleane kwa shida na raha…’akasema
Mume wangu akawa anakiendesha kigari chake peke yake na kuelekea chumbani, nikamuangalia docta, na docta akaniashiria nimfuate mume wangu, basi ikabidi niagane na docta, yeye akaondoka, na mimi nikamfuata mume wangu ndani.
‘Mbona unakuja huku, mgeni anabakia na nani, msindikize mgeni au..?’ akaniuliza
‘Anaondoka, nimeshaagana naye, kaondoka…’nikasema
‘Mimi nipo safi mbona, sasa hivi nataka nilale tu, nasikia kulala tu, nahisi macho mazito…’akasema
‘Uliamuka kabla dawa haijaisha nguvu yake…’nikasema
‘Niliota ndoto mbaya…’akasema
‘Ndoto gani…?’ nikamuuliza
‘Docta, ananiibia mke wangu…’akasema sasa akiniangalia huku anatabasamu kama utani vile
‘Hahaha, kama nikukuibia basi angelikuibia zamani, sio sasa, keshachelewa, na uzee huu anatakia nini tena kwangu, hizo ni ndoto za shetani usiziamini…kwanza yeye ana mke wake mnzuri..’nikasema
‘Mhh,..ni kweli lakini wewe ni mnzuri zaidi yake…, na .. na una mengi ambayo mke wake hana…’akasema
‘Kama yapi, …?’ nilimuuliza lakini nikiwa na tahadhari.
‘Mali, familia yako ina julikana…na mengine mengi..’akasema
‘Na wewe umenioa kwa hayo pia, au sio…?’ nikauliza
‘Ofcourse yes, uzuri wako, na hayo mengine vilinifanya nijisikie nina mke wa maana sana,..ndio hivyo, mitihani hii inanifanya nijutie kwa niliyoyafanya, …lakini nakuahidi mke wangu hayo yaliyopita sitarudia tena…’Nilitaka kumuuliza yapi kayafanya, lakini nikaogopa, haitakiwi, nikabakia kimia.
‘Sikiliza mke wangu, ngoja nipone, nina uhakika nikipona, na nguvu zangu zikirejea vyema, kila kitu kitakuwa sawa, niamini, kila kitu kitarejea kama kilivyokuwa awali…,nimeligundua kosa langu....’akasema
‘Hilo neno mume wangu…, utapona tu, usijali…’nikasema
‘Niahidi mke wangu, kuwa hutaniacha…’akasema hivyo na kunifanya nishtuke kidogo, ni kauli yenye utata, sikufahamu ni kwa muda huo au ana lengo gani, lakini sikuruhusiwa kuanzisha mijadala, na pia, sikupenda kusema uwongo
‘Mume wangu dawa itakuwa haifanyi kazi, tukiendelea kuongea, wewe lala kwanza, umeshaharibu kwa kuamuka mapema, sasa inabidi ulale tu…ukiamuka tutaongea, unasikia, usipuuze maagizo ya docta, ukifanya makosa hutapona na ndoto yako haitatimia..’nikasema
‘Ndoto…!’akasema kwa mshangao
‘Ndio za kuendeleza miradi yako, au sio…’nikasema
‘Haya bosi, ngoja nilale..kweli nasikia kulala, lakini sitaki niote hiyo ndoto tena, lakini naomba usiondoke hapa kitandani kabisa, nataka ukae hapa karibu yangu, nikiamuka tuongee, nataka niongee na wewe mambo mengi mazuri, ma-zzzrrr..’akasema
‘Haya lala…’nikasema nikiwa nimekaa karibu yake, na baada ya muda nikasikia akitoa ile sauti ya kuonyesha kuwa kweli kalala.
***************
Siku nyingine, nilikuwa nimekaa nyumbani, sebuleni, na mume wangu alikuwa amelala chumbani baada ya kupata dawa. Na nilipohakikisha amelala, nikaona nitoke kidogo nje, kitahadhari, maana akiamuka akaona sipo karibu yake, ni mtihani,..nikasema leo nataka nifanye jambo, angalau nitoke hata kufika madukani,.
‘Nani huyo tena…nikasema, niliposikia mtu anagonga geti la nje
Muda huo nilikuwa varandani nakagua kuwa kila kitu kipo sawa, kwa vile najua kuwa mfanyakazi wetu wa ndani yupo, atafungua geti sikuhangaika kutok nje, lakini haikuwa hivyo, mfanyakazi alikuwa hayupo karibu na huyo mtu akawa anaendelea kugonga,..
‘Kaenda wapi huyu binti…’nikawa naongea peke yangu, nikachungulia kupitia dirishani, na muda huo, huyo mtu akawa anafungua geti mwenyewe, kabla sijajiuliza ni nani, mara akatokea mfanyakazi wetu, kumbe alikuwa anafanya usafi sehemu za ndani.
‘Nani kagonga geti na sasa anafungua geti mwenyewe…?’ nikamuuliza
‘Hata sijui ni nani ..ngoja nikaangalie…’akasema na kukimbilia nje.
Haikupita muda, nikasikia watu wanaongea huko nje na vicheko…nikaingiwa na hamasa ya kumtambua huyo mtu ni nani, maana ni sauti ya kime, nikachungulia dirishani, alikuwa ni mdogo wa mume wangu.
Mdogo wa mume wangu mhh, kajileta…!!
Kwa haraka nikatoka nje, nilitaka nimuwahi, kwani sikutaka mtu yoyote kumsumbua mume wangu, japokuwa nafahamu kuwa mdogo wake huyo, akijua kaka yake kalala hawezi kumsumbua, kwani anafahamu utaratibu ulivyo,japokuwa sijaonana naye muda sasa, lakini moyoni nilikuwa na hamu sana ya kuongea na huyu mtu!
‘Hii ndio nafasi pekee…’nikajisemea kimoyo moyo nikitokeza kwenye mlango.
Sasa hivi nakuwa na tahadhari, sio kama zamani, mume wangu anaweza kunywa hizo dawa ghafla akaamuka, na akiamuka huwa hapendi kukaa ndani, anapenda kuzungushwa nje na kigari chake cha kukokotwa. Ndio maana nikaona nimuwahi mapema huyu mtu kwa tahadhari.
Nilihakikisha nimeusindika mlango nyuma yangu, na sasa nikawa naangaliana uso kwa uso na shemeji yangu huyu, alikuwa mlangoni alitaka kufungua,.. inaonekana ni kama vile hakutarajia kuniona hapo nyumbani, akabakia mdomo wazi akishindwa hata kuongea, nikatabasamu ili kumuondoa wasiwasi, na yeye kwa aibu akatizama chini..
‘Habari yako shemeji, mbona unaonekana kama umeona kitu cha kukuogofya, hukutarajia kuniona mimi hapa nyumbani nini, au una wasiwasi gani, naona unajaribu kunikwepa kinamna?’ nikamuuliza
‘Ni kweli, nilijua labda haupo, labda umetoka kwenda kazini kidogo, sasa kazi inakuwaje shemeji, …mmh, huu ni mtihani, lakini yana mwisho au sio, si kukwepi shemeji ni shughuli tu....’akasema.
‘Kuna nini kinaendelea kati yako wewe na mfanyakazi wangu?’ nikamuuliza, nilimuuliza hivyo nikiwa na maana yangu, japokuwa ulikuwa ni utani.
‘Hakuna kitu shemeji, hahaha, shemeji naye bwana, na mfanyakazi wako hakuna kitu kama hicho kabisa ...mimi nimekuja kwa ajili ya kumwangalia kaka, na kwa muda sasa sijafika, nilikuwa nimesafiri kidogo, na unajua nikiwepo basi inabidi nije, na ikibidi nikae hapa, ili nisaidie saidie,..na kiukweli mnisamehe sana, sijafika muda kumuona mgonjwa,....’akasema,
Nilimwangalia alivyokuwa akipata taabu ya kutaka kujieleza , na baadaye nikasema
‘Usijali shemeji nakutania tu, karibu, lakini kaka yako kalala na dawa anazotumia hatakiwi kusumbuliwa, unasikia sana…’nikasema.
‘Kama kalala basi …niwasalimie kidogo niondoke zangu, …nilijua nitakuta keshaamuka,..jana alinipigia simu kuwa nijitahidi tuonane…’akasema
‘Alitaka muonane mbona hajaniambia..?’ nikauliza kwa mshangao, hata yeye akaonekana kushangaa, na akasema
‘Kwakweli mimi sijui, ila alinipigia, simu, tukawa hatuelewani, mawasiliano, maana nilikuwa kwenye gari, akasema nijitahidi nionane naye…’akasema
‘Ok, labda kapitiwa kuniambia, hamna shida, ngoja tuongee kwanza
‘Ndio shemeji niambie…’ akasema
‘Unajua shemeji, wewe ni sawa na mdogo wangu, ....nakuona hivyo licha ya kuwa wewe ni shemeji yangu, ndio maana wakati wote nimekuwa nikihakikisha kuwa maisha yako yanakuwa bora, ili uweze kusimama kwa miguu yako mwenyewe, na natumai hayo yameshakamilika...na hapa ni nyumbani kwako, wakati wowote unaruhusiwa kufika, nilishangaa tu, kukuona kama unani kwepa, hasa pale hospitalini, nikajiuliza kuna nini...’nikasema.
‘Hapana sijakukwepa shemeji hizi hisia zako tu, kwanini nikukwepe..’akasema.
‘Hakuna tatizo kaka yako ana maendeleo mazuri tu, ila kuna mambo muhimu sana tunahitajika kumsaidia, …ndio najua mengi ni majukumu yangu, maana huyo ni mume wangu, au sio, ....’nikasema.
‘Ni kweli shemeji, ila kama kuna lolote la kusaidia wewe niambie tu …’akasema.
‘Usiwe na wasiwasi, sio jambo kubwa sana,..’nikasema, nikimuelekeza huyo shemeji yangu twende bustanini, kuna sehemu maalumu tumetengeneza ya kuongelea, upepo wake ni mwanana, kama upo ufukweni mwa bahari, na mume wangu hupendelea kuja kukaa hapo.
‘Tuletee vinywaji, na hakikisha kuwa mume wangu akiamuka unaniita mara moja...unasikia.’nikasema.
‘Nitafanya hivyo dada.....’akasema.
*********
‘Shemeji, nataka tuyafupishe mazungumzo yetu iwezekanavyo, kwani kaka yako akiamuka natakiwa niwe naye karibu, kwahiyo nakuomba nikikuuliza mambo fulani fulani ujitahidi kunijibu kwa ufasaha, bila ya kuogopa....’nikamwambia.
‘Uliza tu shemeji.’akasema.
‘Ninachotaka kukuuliza ni mambo ya kawaida tu usiwe na shaka...’nikasema.
‘Sawa nakusikiliza,...lakini kama ni kuhusu kaka, mimi sijui lolote...’akaanza kwa kujitetea.
‘Usijali,....wewe utaongea tu kile unachokifahamu, sio swala la kesi au swala la kulazimishana, kitu ambacho hukijui hukijui,…ila haya yote nayafanya kwa manufaa ya kaka yako…’nikasema
‘Ni kweli….’akasema
‘Mimi,sizani kama wewe unafurahia hiyo hali aliyokuwa nayo kaka yako, na sizani utataka hilo litokee tena, ina maana ni lazima na sisi kama tunamjali tuone tunamsaidiaje, na kabla ya hilo tujaribu kuona kama kuna sababu iliyosababisha hilo kutokea, ili lisije kutokea tena, umenielewa hapo....’nikasema.
‘Kwakweli shemeji mimi sifurahi kabisa hiyo hali, kaka na wewe ni watu muhimu sana kwangu, wazazi wetu kama unavyowafahamu, hawana mbele wala nyuma, wewe ndiye umeisaidia familia yetu kupitia kwa kaka,sasa naogopa sana kaka asije akaondoka..sijui itakuwaje, japokuwa nimeanza maisha lakini bila ya nyie bado najiona sina uhakika wa maisha,...’akasema.
‘Basi kama unafahamu hivyo ni vyema, tukamsaidia kaka yako, kwani japokuwa kiafya anaendelea vyema, lakini mpaka sasa sijajua ni nini kilichomfanya hadi afikie hapo, je ni jambo la dharura tu, au kuna jambo jingine ambalo huenda bado lipo, na kama lipo ni nini, ,..’nikasema na hapo akakaa kimia tu.
‘Unaposema hivyo shemeji unahisi kaka kapatwa na hiyo ajali kutokana na jambo fulani au, mimi nilijua kuwa ni ajali ya kawaida tu, ambayo anaweza kupatwa mtu yoyote’ akasema.
‘Ajali ni ajali ndio, lakini kuna ajali inakupa maulizo mengi kutegemea ilivyotokea, ndio maana nataka nikuulize wewe ambaye muda mwingi akirudi kazini, au…ikitokea dharura mnakuwa naye,…’nikasema.
‘Shemeji mimi sio kwamba mchana kutwa nakuwa naye, unafahamu hilo, kwani hata mimi ninakuwa kwenye mishe mishe zangu,... na mimi najaribu kutafuta jinsi ya kusimama mwenyewe... wakati mwingine huwa nafanya kazi za kaka, lakini sipendi mimi nifanye kazi kwenye ofisi yake, kama tulivyowahi kuongea..’akasema.
‘Ni kweli, sasa turejee kwa kaka yako, tumsaidie, kuna onekana kuna tatizo, na hueda tatizo hilo lipo nje…kuna kitu kinamsumbua, na huenda kakuitia kwa hilo, kaka yako hatakiwi awaze sana, ndio maana najitahidi kuchuja kila jambo, unanielewa, sasa hebu uwe muwazi kwangu, hajakuambia anakuitia nini, au huna fununu ya jambo fulani…’nikasema
‘Nijuavyo mimi , biashara za kaka, huko kazini zilifikia kubaya, hakuna wateja, ..na ikawa watu hawalipo madeni, kwahiyo na yeye akawa hawezi kulipa madeni, hilo likawa linamsumbua sana, na mara nyingi ananituma kwa wateja wake kufuatilia madeni, labda ndio hivyo…’akasema
‘Unaona vitu kama hivyo mimi nilikuwa sijui, haniambii,..’nikasema
‘Kaka huwa ni msiri sana, hata akiwa na shida hapendi kusema huwa anapambana kivyake, hata mimi nilimshauri akuambie akasema hawezi, atapambana kivyake, kwahiyo sijui, zaidi…ila nilisikia siku moja akilalamika kuwa watu wanaomdai, wanataka kufungua mashitaka…’akasema
‘Unawafahamu kwa orodha…?’ nikauliza
‘Kwa kichwa hapana, ila ukitaka ninaweza kukutafutia huko ofisini…’akasema
‘Hilo liache kwanza, je hakuna kitu kingine umesikia, akilalamika au…ni kwanini akatokea kunywa pombe sana…?’ nikamuliza
‘Shemeji mimi nijuavyo, na aliwahi kuniambia ni sababu ya mawazo, amekuwa kwenye wakati mgumu na nahisi anaona kama hana mtu wa kumliwaza vile, ni yeye na kazi yake, na anaogopa kusema kashindwa, ,….nahisi ni hivyo shemeji..madeni, na…sijui, kama kuna tatizo jingine mimi siwezi kufahamu…’akasema
‘Unavyosema hivyo..kumliwaza.., ni kama vile aliwahi kulalamika, kama unavyosema anahisi hana mtu wa kumsaidia, mimi si nipo mkewe jamani,je hujawahi kusikia akilalamika mbele yako, kuwa kuna tatizo analipata dhidi yangu?’ nikamuuliza.
‘Shemeji hapana, lakini mimi nimeishi na nyie, kwahiyo mengine nayafahamu, wakati mwingine nilikuwa natamani kuwa kama nyie wachapakazi, mkirudi nyumbani hamna muda wa kuongea ni kazi tu….’akasema
‘Naomba uniambie waziwazi, nitafurahi sana ukianiambia ukweli, kuwa labda katika maisha yetu uligundua kasoro fulani, maana wewe tumeishi nawe, ukisoma mpaka ukapata kazi, niambie ukweli shemeji,kuna jambo gani tunakosea, au mimi nimekosea mpaka namkwaza kaka yako?’ nikamuuliza.
‘Mhh, shemeji mimi sioni walakini ndio maana nasema natamani niwe kama nyie, lakini kwangu ukifanya hivyo mke ataanza kulalamika, unanielewa hapo, wake zetu sisi, kisomo kidogo, ukiwa nyumbani wanataka usifanye kitu, uwe unawasikiliza wao, ukishika simu ugomvi, uki..ndio hivyo,…mimi hata laptop naogopa kwenda nayo nyumbani….’akasema
‘Ina maana kumbe labda hata kaka yako yupo hivyo, kuwa labda alikuwa hapendi hali hiyo ya mimi kuwa na kazi hata nyumbani, lakini hata yeye alikuwa akifanya hivyo au sio…’nikasema
‘Kiukweli, nyie mnaishi kama wazungu, ..sizani kama kaka anaweza kulilalamikia hilo, mimi sijui kabisa…’akasema
‘Kwahiyo kwa uoni wako, kaka yako …hiyo ajali haijasababishwa na jambo fulani,, unavyohisi wewe…?’ nikamuuliza
‘Yaweza ikawa na sababu kwa jinsi nilivyosikia kuwa aliendesha kwa mwendo kasi, na kaka hana tabia hiyo ya kuendesha gari kwa mwendo kasi, ndio maana wengi wanahisi kulikuwa na jambo zito.., hata mimi mwenyewe nimejiuliza sana hilo swali, lakini ajali ni ajali tu shemeji…’akasema.
‘Kwahiyo wewe unahisi tatizo la kaka yako ni madeni na sio labda kuna mataizo ya kifamilia, labda, kitu kama hicho...?’ nikamuuliza.
‘Inawezekana kuna tatizo nje, mimi na wewe hatulijui, lakini kwa uoni wangu mdogo, nahisi kama alikuwa na msongo wa mawazo, kwanza madeni, pili nahisi alihitajia mtu wa karibu sana wa kuyaondoa hayo mawazo ya kazini, lakini wewe upo, sijui kwanini hakutaka kukushirikisha, na sijui zaidi shemeji…’akasema
‘Hapo sasa unaanza kusema ukweli…kuwa pamoja na yote hayo, nahisi ananiona kama sipo karibu naye sana, anaogopa kuniambia, ataonekana mdhaifu…’nikasema
‘Sawa sawa shemeji…’akasema
‘Kwahiyo akaanza kunywa, kuondoa mawazo…’nikasema
‘Sawa sawa shemeji…’akasema
‘Na ulevi, nisikiavyo, raha yake uwe na wenza, marafiki, wa kike na wa kiume mnakunywa mnacheka, au sio…’nikasema
‘Ndio hivyo hivyo…’akasema
‘Na kaka yako ni binadamu au sio, na ni mwanaume au sio, ni lazima akiwa anakunywa alikuwa na marafiki, anakunywa nao ..au sio…?’ nikauliza hapo akasita halafu akasema
‘Yawezekana…ndio anakuwa nao, ni kawaida hiyo…’akasema
‘Na marafiki wanaweza kuwa wa kike na kiume na wewe unawaona , sema ukweli wako, kumbuka, tunaongea ili kupata namna ya kumsaida kaka yako…’nikasema
‘Ni sawa shemeji, kwnye kunywa hivyo vipo, na nijuavyo kaka pia alikuwa na marafiki zake, na wakati mwingine ndio, wanakuwepo wanawake…’akasema
‘Na wengi ni wale wa mara kwa mara ..au sio, maana ni lazima mzoeane, huwezi ukawa na marafiki wa siku moja moja, au sio,…?’ nikauliza
‘Ni kweli shemeji, ni wale wale marafiki zake….’akasema
‘Sasa nataka tu kuliweka sawa, hao marafiki zake, nimeshawafahamu, yupo docta,..yupo wale wafanyakazi wenzake, wapo wale majirani wake wa kazini, na wanawake ni nani na nani…?’ nikauliza
‘Mhh…mara nyingi,..wapo, lakini anayekuwa karibu naye ni…unamfahamu shemeji, ni yule…yule mdada rafiki yako, na wanawake wengine ni wapenzi wa marafiki zake,…’akasema
‘Kuna kipindi analewa kupitiliza…au sio…?’ nikauliza
‘Ndio, hilo siwezi kukukatalia, hata yeye hawezi kulipinga…’akasema
‘Na kuna muda aliwahi kulala nje, kwasababu ya kulewa sana…’nikasema
‘Mhh..shemeji…lakini mimi namchukua na kumleta nyumbani…’akasema
‘Haijatokea nyie mkalala nje na mkaja karibu na asubuhi..au yeye akaja karibu na asubuhi..?’ nikamuuliza
‘Mmmh labda kukiwa na sherehe…’akasema
‘Lakini ilishatokea au sio..?; nikauliza
‘Kiukweli….eeh, ndio ilishatokea…’akasema
‘Na muda mwingine huyo mdada rafiki yangu alikuwepo…?’ nikauliza
‘Sio muda wote..inatokea tu, na mara nyingi huyo mdada anaondoka mapema..’akasema
‘Na ile siku mlichelewa, mkawa mumelewa mkaenda kulala kwa huyo rafiki yangu je,ilikuwaje..?’ nikamuuliza hapo akashtuka na kusema;
‘Shemeji, …siku zile, hahaha, nani alikuambia,..ndio..lakini sio kulala, kaka yeye aliondoka, unajua ilikuwaje, tulipotoka kule tukampitisha shemeji kwake, mara kukazuka maongezi, akatukaribisha kwake,..ujuavyo pombe hatukuangalia muda, wengine wakajikuta wamelala kwenye sofa…’akasema
‘Yeye ndiye aliwakaribisha, au sio…?’ nikauliza
‘Ndio, …na muda huo kaka kalewa, akawa naye anakubali haraka, …basi tukaingia kwake, tukaendelea kunywa, kuongea, wengine usingizi tena,…lakini kaka aliondoka…’akasema
‘Kaka yako aliondoka, wew ukabakia na rafiki yangu, mkalala naye hadi asubuhi si ndio hivyo…?’ nikauliza
‘Ilibidi mimi nibakie, kwa maaagizo ya kaka, kuhakikisha, kuna usalama, ndio sababu hiyo, sio vinginevyo shemeji, na asubuhi aliponiona huyo mdada akanifukuza…’akasema
‘Huyo mdada alilewa hajitambui, na wewe ukachukua nafasi hiyo kufanya ulichodhamiria siku nyingi ni kweli si kweli, usinidanganye nimeshafahamu kila kitu..’nikasema
‘Hahaha, shemeji bwana, hakuna kitu kama hicho, kaka angeniua, hapana..’nikasema
‘Kwanini kaka yako akuue…?’ nikauliza
‘Unajua tena shemeji, yule ni sawa na wewe, hatafurahia kama nitafanya jambo baya dhidi yake…’akasema
‘Na hiyo hali ya kwenda kulala kwake, sio mara moja ni zaidi ya mara moja au sio..?’ nikauliza
‘Mhh, kama mara mbili, au tatu, sikumbuki vyema…’akasema
‘Kaka yako hakuwahi kuingia kulala na rafiki yangu..?’ nikauliza hapo akashtuka na kusema
‘Ha-hapana shemeji…mimi sijui , sikuwahi kuona, ..unajua anamuheshimu sana yule mdada, sizani, mimi hapo siwezi kuwa na uhakika…’akasema
‘Mdada ana mtoto, na nikuulize tangia ajifungue uliwahi kwenda kumtembelea huyo mdada..?’ nikamuliza
‘Hapana shemeji, mimi na yule mdada hatuivani sana, inatokea siku na siku akiwa na shida zake ndio ananiona wa maana, vinginevyo, sina habari na yeye kabisa…’akasema , mara nikahisi sauti kama ya watu wanaongea, nikatega sikio, kukawa kimia, nikaanza kuingiwa na wasiwasi, mume wangu asije akawa kaamuka
‘Hebu kidogo…’nikasema na kusimama kusikiliza, nilikuwa sijamalizana na huyo mtu, nikasema
‘Sasa sikiliza shemeji…, mimi ninakupa wewe muda wa kuyatafakari haya kwa makini, nataka uniambie ukweli, kuhusu mahusiano ya mume wako na rafiki yangu, je kaka yako hana mwanamke mwingine yupo naye karibu..?’ nikamuliza
‘Mhh..mimi simfahamu…’akasema
‘Sasa nitaongea na wewe tena kesho, lakini sio hapa nyumbani, nataka tuyaongelee haya na mengine tukiwa wawili, nataka uniambie ukweli, unasikia, kwa manufaa ya kaka yako, unanisikia,....’nikasema.
‘Shemeji hamna tatizo kabisa , lakini yote nimeshakuambia, ..sizani kama kuna jambo ninalolifahamu …’akasema
‘Nimefurahia sana maongezi yako ya leo, hatujawahi kukaa na kuongea hivi, ukaniambia ukweli kutoka moyoni mwako,,..nimefurahi sana, na wakati wote ninakuona kuwa ni mtu mwema, unayejali, wale wanaokujali, nimefurahi sana...sasa ili kulihakiki hilo, nataka tena tuongee, kuhusu rafiki yangu, unajua mtoto wake anafanana sana na wewe…’nikasema.
‘Eti nini, anafanana na mimi, hapana shemeji, sio kweli, haiwezekani sio kweli….’ Akasema na kushtuka, na muda huo simu yake ikawa inaita lakini hapokei ni kama kachanganyikiwa fulani.
Na muda huo nikasikia sauti ya wazi, kuwa mfanyakazi wangu anaongea na mtu ndani, nikajua mume wangu ameshaamuka kwahiyo mimi kwa haraka nikawa nakimbilia huko ndani, na nilimuona shemeji akisikiliza simu na huku anatoka nje....
**************
Nilifika ndani na kukuta kupo kimia, na wakati nataka kwenda chumbani ndio nikasikia watu wakiongea nje, nilipochungulia nje kwa kupitia dirishani nilimuona yule msaidizi wangu akiwa anasukuma kile kigari cha mume wangu, na mume wangu akiwa kakaa na alikuwa kaegemeza kichwa huku kashika shavu, a macho kayafumba kama lasinzia, hiyo ilikuwa ni dalili, kuwa alikuwa na mawazo.
Kumbe mfanyakazi alimchukua mume wangu na kutoka naye nje wakati tunaongea na shemeji yangu,inaonekana mume wangu aliamuka akanikuta sipo na wakati huo mfanyakazi wangu alikuwa anafanya usafi, au….mume wangu alisikia yupo akamuita, na akamuambia amtoe nje
Niliwaangalia, na mfanyakazi alikuwa akikisukuma kigari huku na kule ndivyo anavyopenda mume wangu, kufanyiwa hivyo, hataki kukaa sehemu moja kwa muda mrefu.
Kwanza nikaingiwa na wasiwasi, nikijiuliza huyu mtu alitoka muda gani, isije ikawa,walifika hadi kule bustanini, wakasikia maongezi yetu na shemeji yangu,kitu ambacho muda wote nilikuwa nikikikwepa, nikaona nithibitishe hilo, nikafungua mlango na kutoka nje,....
Mume wangu alipoisi kuna mtu anakuja akafungua macho na aliponiona akajitahidi kutabasamu, lakini lilikuwa tabasamu la kujilazimisha, kwanza aliniangalia machioni, mimi nikatabasamu, yeye akabenua mdomo, ila ya dharau au kujifanya anajua jambo
‘Mume wangu samahani, nilikuwa na mgeni nikakuacha chumbani peke yako..’nikasem
‘Mdogo wangu kashaondoka, mbona hajanisalimia, nilitaka kuongea naye.....’ akasema
‘Ndio kapigiwa simu ya haraka, labda atarudi baadae lakini kwanini hukusema , kuwa umeamuka, nije, huyu mfanyakazi sio kazi yake hii, hii ni kazi yangu,..’ nikasema
‘Unajua upepo, na hali ya bustanini ni kama dawa kwangu nilipoamuka tu, nikaona haupo nikajua umetingwa na jambo, nikamuambia mfanyakaz anisaidie nitoke nje,..na wakati natoka ndio nikawaona mnaongea, nikaona nisiwasumbue, ….’akasema
‘Hutusumbui bwana…yule ni ndugu yako na mimi ni mke wako, wote tunawajibika kwako...’nikasema
‘Aaah, ni kweli, lakini na mimi ni binadamu, nakuonea huruma, na…..yawezekana na wewe ulikuwa unatafuta njia za kunisaidia nipone haraka, na mimi nataka kupona haraka, au sio…’akasema na kunifanya nihisi kuwa huenda alisikia jambo.
‘Mume wangu na wewe siku hizi una maneno, …’nikasema
‘Mke wangu hata mimi sijui yametoka wapi,..ila mengine uwe unaniuliza mimi mwenyewe nitakuambia kila kitu, usiogope kuniuliza mke wangu…nakupenda sana mke wangu usije kuniacha, ukiniacha na mimi nitaicha hii dunia ya mateso,..naumia mke wangu, kweli hujafa hujaumbika…’akasema kwa unyonge
‘Mume wangu kwanini unaongea hivyo…?’ nikauliza
‘Najua na wewe unajua, kuwa nimekosea sana, na kiukweli mke wangu, mengine tuyasahu tu, tusonge mbele, ukiwasikiliza sana wazazi wako tutaharibu kila kitu, kiukweli mimi najua nimekosea wapi, na mimi kwa hali kama hii, nimepata fundishi kuba sana, na kwahiyo naahidi sitarudia tena, najua kazini kupoje lakini najua jinsi gani ya kupainua tena, hata bila ya msaada wa baba yako…’akasema
‘Hayo usiyawazie sana mume wangu…muhimu ni wewe kupona, muhimu ni afya yako, ukiyawazia hayo hutapona, na kazi zipo tu, muhimu ni afya yako…’nikasema
‘Kupona kwangu ni pamoja na kufahamu kuwa wewe upo na mimi na kamwe hutaweza kuniacha…hata iweje ..lakini najua nipo kwenye kuti kavu, kwa hali kama hiyo nitawezaje kupona…, mawazo yataishaje, wakati najua kupona kwangu ni kuingia kwenye jela nyingine ya sintofahamu, najua yote hayo, baba yako, anasubiria tu, nipone, au sio…’akasema.
‘Sikiliza mume wangu…’nikasema
‘Nisikilize nini bwana,..hata ujifanye vipi najua, wewe na baba yako mpo kitu kimoja, najua..rafiki yako kaharibu kila kitu najua…lakini itasaidia nini kwa sasa, ila nikuambie ukweli, mimi nikiwa hivi miaka nenda rudi, na kama nitaendelea kuteseka hivi, aah, kwanini bwana niwasumbue watu…’akasema
‘Mume wangu hayo yametokea wapi, tulishaongea ukasema utajitahidi ili upone haraka…’’nikasema
‘Yaaah…nitapona haraka, …ili niingie kwenye kizima cha kesi, …unajua baba yako anatamani sana, ukaishi na watu kama docta, sio watu kama mimi, kwahiyo anatafuta kila namna, ndio maana alinitega, nimeliona hilo kwenye ndoto, na..mke wangu nasema hili kwako, kama ni hivyo, sawa, lakini utanikumbuka, labda, nikiwa huko kuzimu…’akasema na kuanza kusukuma kigari kuondoka.
‘Mume wangu…unaongea nini sasa..’nikasema lakini huyoo akasukuma kigari kuelekea ndani. Na muda huo nikahisi kichwa kinaniuma ni hiyo ni dalili mbaya kwangu…
NB: Kwa leo inatosha ....
WAZO LA LEO:Katika maisha yetu ya ndoa, na katika maisha yetu ya kila siku, tujifunze kuwa wakweli, kila mmoja amwamini mwenzake , awe mkweli kwa mwenzake....kwani, ukweli wakati wote, ni kinga ya uhasama,...japokuwa kuna wakati mwingine inatulazima kukwepa kusema ukweli kwa maana fulani, ili kukwepa madhara..tukihisi tunafanya hivyo kwa nia njema….lakini kama tukianza hivyo kusema uwongo, kidogo kidogo hujenga mazoea, na tutajikuta tunahasimiania, unafiki unatawala nafsi zetu..kwa vyovyote iwavyo, tujifunze kuwa wakweli kwa wenza wetu, ili kujenga uaminifu, upendo na furaha na kujenga familia zilizo bora