Kama mambo ni hivi, Ditopile Aachiwe!!!
Na. M. M. Mwanakijiji
Hivi majuzi nilikuwa namtambia rafiki yangu wa Kiganda kuwa Tanzania ukilinganisha na nchi nyingi za kiafrika na hata sehemu nyingine duniani ina mahakama huru zaidi na zinazoheshimika. Niliendelea kutamba kuwa kitendo kama kilichotokea huko Uganda ambapo askari waliingia kwenye maeneo ya mahakama na kuwakamata watu walioachiwa huru hakiwezi kutokea Tanzania. Kumbe nisichokijua kilikuwa ni kama 'usiku wa kiza'. Waswahili walisema "usimtukane mamba kabla hujavuka mto" na ndio hao hao waliosema "usitukane wakunga na uzazi ungalipo". Hata kabla ya wiki kwisha nikajikuta nimeumbuliwa na nchi yangu, kwani kile ambacho sikuwaza kinaweza kutokea Tanzania kimetokea na kuniacha nimepigwa na butwaa huku nimeyauma meno yangu kwa hasira. Jeshi la Polisi limeingia mahakamani kwa nguvu.
Mazingaombwe na wale wafanyao mazingaombwe! Siku ya Alhamisi kimefanyika kitendo kwenye Mahakama Kuu ambacho kama hakitakemewa na waliohusika kuchukuliwa hatua kali kinaashiria kubomoka kwa utawala wa sheria na utafutwaji wa haki katika mahakama za Tanzania. Na kitendo hicho kinatishia uhuru wa Mahakama, uhuru wa vyombo vya habari, na usawa wa raia wote mbele ya sheria.
Wakati polisi wanamfikisha mtuhumiwa wa kesi ya mauaji Bw. Ditopile Mzuzuri kwenye mahakama kuu jijini Dar-es-Salaam, bila sababu ya msingi waliamua kumpitisha mtuhumiwa huyo kuingia kwenye mahakama hiyo kwa kupitia mlango unaotumiwa na majaji. Kwa wale ambao hawajui taratibu za mahakama nyingi (siyo Tanzania peke yake hata sehemu nyingine duniani), majaji wanapokuja kazini au kwa shughuli mbalimbali mahakamani hapo kuna mlango ambao wao pekee wanapitia na mlango huo mara nyingi hautumiwi na watu wengine wakiwamo wafanyakazi wengine wa chombo hicho. Hata mawikili hawaruhusiwi kupita huko. Siyo tu kwa ajili ya heshima ya cheo chao bali pia kwa ajili ya usalama wao na uhuru wa chombo hicho
Lakini kwa mara ya kwanza katika historia ya Tanzania ambayo naweza kuikumbuka kwa haraka maaskari wa jeshi la Polisi walitumia ubavu (pamoja na kumpiga kikumbo mlinzi wa Mahakama hiyo) na kulazimisha mtuhumiwa huyo kuingizwa mahakamani hapo kwa kupitia mlango huo wa majaji. Kitendo hicho kama kilivyoripotiwa na vyombo mbalimbali vya habari kiliwashangaza watu wengi wakiwamo wafanyakazi wa Mahakama hiyo. Licha ya polisi kuingia kwa nguvu mahakamani hapo waandishi wa habari nao walishambuliwa na maafisa hao na baadhi yao vyombo vyao vya kazi kuharibiwa na polisi hao na wanafamilia ya Dito na hivyo wandishi kunyimwa nafasi ya kufanya kazi zao kama kawaida. Vitendo hivyo siyo tu vinatishia uhuru wa mahakama bali pia uhuru wa vyombo vya habari wa kutafuta, kupata na kutoa habari.
Mshangao wa kitendo hicho ulioneshwa wazi na Msajili wa Mahakama hiyo bw. Prophi Lyimo ambaye alinukuliwa akisema kuwa Kwa kweli tumekasirika sana, sijuwi walipewa nini, maana katika hali ya kawaida hawawezi kufanya hivyo. Haijawahi kutokea hapa, nimemwambia Tibaigana awabane polisi wake na wamueleze kwa nini wamefanya hivyo. Katika vyombo vya habari haijawekwa wazi kama askari waliompitisha Ditopile kupitia mlango huo walikuwa na silaha ama la. Kama walikuwa na silaha kitendo hicho kinakuwa na uzito ambao maneno ya karatasi hayatoshi kuelezea. Bila ya shaka kuna sababu iliyowafanya askari hao kufanya kitendo hicho na hapa nitashuku tu sababu hizo hadi zitakaposemwa hadharani.
Inawezekana kabisa kuwa maafisa wa ngazi za chini wa polisi walifanya kitendo hicho baada ya kupewa amri na mkubwa wao kumpitisha Mtuhumiwa huyo wa mauaji kupitia mlango huo wa majaji. Kama ni kweli, mkubwa huyo ni lazima ajulikane na hatua za kinidhamu (ikiwemo kufukuzwa kazi, kushushwa cheo n.k) zichukuliwe dhidi yake. Afisa yeyote wa jeshi la polisi ambaye hajui uzito wa kuingia kwenye chumba cha majaji kwa nguvu na kupitisha watuhumiwa huko wakati kuna milango iliyopo kwa ajili ya kazi hizo hastahili kuvaa nembo ya jeshi letu! Askari wa chini waliotekeleza amri hiyo ambayo si halali ni lazima nao wachukuliwe hatua kali. Maaskari hawa hawawezi kujitetea kuwa walikuwa wanafuata amri tu. Kutii amri ambayo siyo halali ni kosa!! Rais kwa mfano, hawezi akatoka nje pale Ikulu na kumuamuru askari ampigie mtu risasi kwa vile Rais amejisikia hivyo na askari huyo akafanya hivyo!! Siyo kila amri inayotolewa na mkubwa ni halali! Maafisa wetu ni lazima (kupitia tukio hili) wafundishwe wazi kuwa mkubwa akikuamuru kufanya jambo ambalo unajua au unahisi ni kinyume na sheria unayo haki ya kukataa kulitekeleza hata kama itatishia ajira yako au kumuudhi mkubwa huyo. Hadi pale utakapohakikishiwa usheria wa amri hiyo. Endapo maaskari hawawezi kukataa kutekeleza amri isiyo halali basi Watanzania tuna matatizo kwani viongozi wanaweza kuwaamuru mamluki hao kufanya lolote lile bila kujali matokeo yake, kwani bosi kasema.!! Hili katika Tanzania ya leo halikubaliki, tunalipinga, na tunalilaani kwa uzito wote unaostahili.
Inawezekana pia kuwa maafisa wa polisi walifanya kitendo hicho ili kuonesha ni nani anayeletwa mahakamani hapo na ni jinsi gani mtu huyo ni tofauti na washtakiwa wengine. Ni wazi kuwa kesi ya Ditopile ni mojawapo ya kesi chache zenye makosa makubwa ambayo kiongozi wa serikali anaweza kuhusishwa nacho, lakini kesi shitaka analokabiliwa nalo siyo ngeni kwenye mahakama zetu. Huko nyuma kuna viongozi walioshtakiwa kwa kuhujuma uchumi, ubadhirifu, wizi n.k lakini hili la kiongozi kutuhumiwa kumuua mtu ni jipya na hasa jinsi mauaji hayo yanavyodaiwa kufanyika. Mara zote ambapo Bw. Dito amekuwa akiletwa mahakamani kuanzia kule Kisutu hadi Mahakamani vimbwanga hufuatana naye. Hiki cha sasa kimepita hayo yote! Polisi hawana sababu yoyote ya kuionesha mahakamani uzito wa mtuhumiwa kwani Ditopile anajulikana na jina lake limetangaa. Lakini, waliofanya kitendo hicho inawezekana kabisa walitaka kutuma ujumbe kuwa Tutampeleka tunakotaka sisi, kwa wakati tunaotaka sisi, na hakuna anayeweza kutuzuia Kama hilo ndilo lilikuwa mawazoni mwa maafisa hawa basi nalo ni sababu ya kumwajibisha afisa aliyesimamia zoezi hilo, na kama mkuu wa polisi wa Kanda alikuwa anaujuzi wa kitendo hicho na akashindwa kukizuia na yeye hana budi kuchukuliwa hatua kali ikiwemo kuandika barua ya kujiuzulu. Kitendo hiki inawezekana kimechukua mistari michache kwenye vyombo vya habari lakini uzito wake unaweza kujaza maktaba!
Sababu nyingine ambayo naombea isiwe ya kweli inatokana na hiyo ya hapo juu. Maafisa wa polisi kutokana na amri waliyopewa au maelekezo waliyopewa waliamua kuitishia mahakama na hususan jaji au majaji ambayo wanaweza kujikuta wakisikiliza kesi hii. Hivi karibuni huko Uganda jambo kama hili limesababisha mgomo wa Majaji na wafanyakazi wa mahakama baada ya polisi kuingia mahakamani kwa mabavu na kuwakamata watu walioachiwa huru na mahakama hiyo ya Uganda. Hapo Tanzania , endapo jambo kama litavumiliwa au kujaribu kupuuzwa litajenga jaribio la chombo cha dola kuitisha mahakama ili isifanye kazi zake za kugawa haki kwa uhuru bila upendeleo. Katika mahakama zetu kuna watu wengi ambao wamewahi kushitakiwa kwa tuhuma nzito zaidi ya hiyo ya Ditopile, na hakuna siku ambapo washtakiwa waliingizwa kupitia mlango wa majaji, siyo wakati wa kesi ile ya uhaini au wa kesi ya Kiula na wenzake. Jaribio hili la kuitisha mahakama natumaini limeshindwa na halitatokea tena.
Hata kama mojawapo ya sababu hizo hapo juu ni ya kweli (ama zote) serikali ni lazima itamke mara moja kukikana kitendo hicho na kuahidi kuchukua hatua za kinidhamu siyo kuunda tume ya uchunguzi! Ingawa Msajili wa Mahakama ametamka kutofurahishwa kwake na kitendo hicho, Jaji Mkuu Bw. Barnabas Samatta ni lazima atamke na kukikemea kitendo hicho na aiambie serikali kuwa endapo jambo kama hilo au hata linalokaribiana na hilo kwa mbali litafanyika, waliohusika watatiwa mbaroni kwa kudharau mahakama na Mahakama yake haiwezi kukubali kuingiliwa na chombo kingine cha serikali hata kama kesi inamhusu mtu mashuhuri kiasi gani.
Zaidi ya yote, kwa vile kesi inaonekana kuwa na mvuto wa hisia nyingi hususan upande wa wanafamilia ya Ditopile ambao wamejaa jijini Dar-es-Salaam, Jaji Mkuu anaweza kuamuru kesi hiyo kuhamishiwa katika mahakama ya Kanda na kupelekwa mkoa mwingine kwenye matawi ya Mahakama hiyo ambapo inaweza kusikilizwa kwa uhuru bila kuvutia watu wenye hisia kali kwani siyo tu inatishia usalama wa maafisa wa mahakama bali pia raia wanaokuja mahakamani kwa kesi nyingine na watu wengine ambao kwa sababu moja ama nyingine wanaweza kujikuta wapo hapo mahakamani.
Vile vile, Jaji Mkuu ni lazima ahakikishe kuwa kama wale walioapishwa kulinda Katiba (maafisa wa Polisi) wameshindwa kazi hiyo, aamuru kuanzia sasa maafisa wa Magereza kumleta Mshitakiwa mahakama na kumuingiza mahakamani na kutoa ulinzi mahakamani hapo badala ya Polisi na ikibidi aombe Rais aidhinishe kikosi cha Polisi wa Jeshi kulinda mahakama hiyo kutoka kwa polisi wasiojua wajibu wao. Lililotekea mahakamani hapo jana si jambo dogo kwa kipimo chochote kile.
Ni matumaini ya wapenda demokrasia wote na wale wanaoelewa mtengano wa madaraka kuwa kitendo hicho (au kifananacho na hicho) hakitarudiwa tena, na endapo kitendo kama hicho kitarudiwa, basi Mahakama iamue kumuachia Ditopile huru kuliko kuvunja vunja na kusagasaga kama kwenye kinu uhuru wa mahakama zetu na hivyo kuharibu mchakato mzima wa utafutaji wa haki!