Mkuu wa Mkoa wa zamani, Ukiwaona Ditopile Mzuzuri (58),akiingia mahakamani jana.
Dito amlalamikia Kikwete
Na Tausi Ally
Mkuu wa Mkoa wa zamani, Ukiwaona Ditopile Mzuzuri (58), amelalamikia ziara za viongozi wa serikali kwenda kutoa rambirambi kwenye familia ya dereva wa daladala, marehemu Hassan Mbonde, anayedaiwa kuuawa naye kuwa ni sawa na kumuhukumu kabla ya mahakama kutoa hukumu yake.
Ingawa hakufika mwenyewe kuhani msiba huo, Rais Jakaya Kikwete alimtuma Katibu Mkuu Kiongozi, Philemon Luhanjo, ambaye pamoja na kutoa salamu maalum za rais kwa wafiwa, pia alitoa ubani wa Sh500,000 kwa familia ya marehemu.
Kupitia kwa wakili Nimrod Mkono, aliyejiunga na jopo la mawakili wanaomtetea, Ditopile aliiomba mahakama iwapige marufuku viongozi hao wa serikali kwenda kutoa rambirambi kiserikali kwenye familia hiyo.
Pia aliitaka mahakama kuvizuia vyombo vya habari kuandika na kutangaza habari za mteja wao nje ya mahakama kwa madai kuwa hali hiyo inaleta hisia mbaya katika jamii na inamtia wasiwasi kuwa hatatendewa haki.
Nimrod alitoa ombi hilo jana mbele ya Hakimu wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Michael Luguru, akidai kuwa mambo hayo yanajenga picha kuwa mteja wake tayari ana hatia kabla ya mahakama kumaliza kazi yake.Aliieleza mahakama kuwa endapo viongozi wa serikali wanataka kwenda kutoa rambirambi kwa familia ya marehemu, basi waende kwa siri na siyo hadharani kama wanavyofanya sasa.
Alihoji kuwa inakuwaje Makamu wa Rais anakwenda kutoa rambi rambi kwa wafiwa kwa niaba ya Rais pamoja na viongozi wengine kwa niaba ya serikali wakiwa na magari ya vimulimuli na hawafanyi hivyo kwa kwenda kumtembelea mteja wake kwa staili hiyo hiyo ya magari ya vimulimuli.Alidai kuwa wapo watu wengi waliouawa kwa kupigwa risasi lakini hakuna viongozi wa serikali wanaokwenda kutoa pole kwa familia zao kwa kutumia magari na vimulimuli vya serikali.
Hata hivyo, baada ya wakili huyo wa Ditopile kutoa malalamiko yake, Mwendesha Mashtaka, Mrakibu Mwandamizi wa Polisi, Charles Kenyela, alisimama na kuieleza mahakama kuwa Katiba ya Tanzania inatambua kuwa watu wote ni sawa mbele ya sheria na kwamba mahakama haifanyi kazi zake kwa kusikiliza mambo yanayofanyika mitaani au ya kisiasa, hivyo matukio hayo hayawezi kuingilia au kuishawishi iegemee upande mmoja.
Aliendelea kueleza kuwa mahakama haiwezi kuzuia viongozi wa serikali kwenda kusalimia ndugu au jamaa zao kwa kuwa nao ni binadamu wenye ndugu na marafiki na hakuna sheria inayozuia kujuliana hali na kwamba vyombo vya habari navyo vina uhuru wa kuripoti kila kinachotokea.Kwa upande wake, Hakimu Luguru alisema mahakama hiyo haina uwezo wa kutoa amri hiyo kama ilivyoombwa kwa kuwa kesi ya mauaji inasikilizwa na Mahakama Kuu.
Alisema kama anaona vyombo vya habari vinaripoti kinyume na matukio yanayojiri, basi awe huru kuchukua hatua za kisheria.Tangu tukio hilo viongozi mbalimbali wamekuwa wakienda nyumbani kwa marehemu kuhani msiba huo, akiwemo, Katibu Mkuu Kiongozi, Philemon Luhanjo aliyekwenda kwa niaba ya Rais Jakaya Kikwete na kutoa ubani wa Sh500,000.
Luhanjo pia alitoa ahadi kuwa Rais Kikwete akitoka safarini angekwenda mwenyewe kuhani msiba huo.Viongozi wengine waliokwenda kuhani msiba huo, ni Makamu wa Rais, Dk Ali Mohamed Shein ambaye pia aliahidi kuwatuma wasaidizi wake kupeleka ubani.
Wengine ni Meya wa Manispaa ya Kinondoni, Salum Londa, ambaye alitoa viroba 10 vya mchele na mafuta ya kula kwa kwa ajili ya kufanikisha kisomo cha hitma ya kumuombea marehemu iliyoandaliwa na kiongozi huyo Jumamosi iliyopita.Vile vile Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Abbas Kandoro, Meya wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, Adam Kimbisa, Meya wa Manispaa ya Ilala, Abuu Jumaa nao wamekwishafika kuhani msiba huo.
Kiongozi aliyefika kwenye msiba huo wakati wa mazishi na kutoa ubani wake wa Sh100,000 alikuwa ni Mwenyekiti wa Tanzania Labour Party (TLP), Augustine Mrema.Mahakamani jana, watu wengi zaidi walijitokeza katika kushuhudia jinsi kesi hiyo inavyoendeshwa kuliko waliojitokeza wakati Ditopile alifikishwa mahakamani hapo kwa mara ya kwanza Novemba 6.
Ditopile anadaiwa kuwa Novemba 4, majira ya saa 1:00 usiku katika eneo la njia panda ya Bagamoyo na Kawe wilayani Kinondoni, jijini Dar es Salaam, alimuua Hassan Mbonde.Mshtakiwa huyo anatetewa na mawakili maarufu watano wa jijini Dar es Salaam, ambao pamoja na Mkono ni Dk Ringo Tenga, Losan Mbwambo, Cuthbert Tenga na Samwel Mapande.