Mohamed Said
JF-Expert Member
- Nov 2, 2008
- 21,967
- 32,074
- Thread starter
- #21
Nilitegemea wataweka ahadi yao kuwa ikiwa hawatakuta madawa ya kulevya katika mizigo yangu watanirejeshea uhuru wangu wataniachia niende nyumbani. Haikuwa hivyo. Wakanirudisha ofisini kwao. Sasa wakaacha madawa ya kulevya wakahamia katika vitabu na “audio cassette” nilizokuwa nimepewa kama zawadi kule Tehran wakaniluliza kwa nini naingiza vitu vile khasa kanda za Khomeni na vitabu vyake nchini. Nikawauliza, “Kwani kanda na vitabu vya Khomeni haviruhusiwi kuingizwa Tanzania? Maana mimi hata nyumbani kwangu hii leo mkifika nina vitabu vya Khomeni na wanafalsafa wengine kama Karl Marx ambao nimesomeshwa pale Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam. Sasa hapo ikaja kejeli. “Ala wewe mtu wa Kariakoo lakini umefika hadi Chuo Kikuu!” Sikujibu kitu. Awali waliponitia mbaroni waliniuliza kwetu na nikawaeleza kuwa nimezaliwa Kariakoo.Mabesela,
In Shaa Allah nitaweka kidogo kidogo...
Hawakunipa jibu kuhusu kuingiza vitabu na cassette za Khomeni. Ikawa sasa kama vile wameishiwa maswali. Nikaona kuwa sasa ni zamu yangu nami kuwapiga maswali. Yule aliekuwa akinihoji nikamwambia, “Mimi wewe nakufahamu vizuri sana...'' Nilihisi amepata mfadhaiko kidogo akanambia,“Unanifananisha...'' Alikuwa anasema uongo lakini mie nikamkubalia. Hapo nikajua kuwa nishampata sasa hana nguvu tena ya kuuliza maswali. Kusema uongo ni dalili ya kujihami. Nikamrushia kombora lingine, “Sasa tuhuma za madawa ya kulevya zimekwisha tuko katika kwa nini naingiza vitabu vya Khomeni nchini?” Akanijibu kinyonge, “Tumeridhika huna madawa.” Kufika hapa tukawa tumemaliza mahojiano.
Wakati huo sasa ni usiku wa manane na nishapeleka SMS kwa sahib yangu mmoja bingwa wa mambo ya mtandao wa kompyuta kumjulisha kuwa nimekamatwa uwanja wa ndege kwa tuhuma za uongo za kuvusha mihadarati na yeye ile kuipata tu ule ujumbe wangu akaifahamisha dunia kuwa nimekamatwa uwanja wa ndege nikitokea mkutanoni Iran na nimebambikiziwa tuhuma za kuingiza nchini mihadarati. Waliponitia mbaroni tu walinionya kuhusu kutumia simu yangu ya mkononi lakini bahati nzuri hawakuninya’ganya. Aliyenipa onyo hili alikuwa mkuu wa kituo cha polisi cha uwanja wa ndege. Huyu rafiki yangu akawa kanisaidia sana maana hadi kumekucha wapenzi wangu wote ndani na nje ya nchi pamoja na vyombo vya habari vinavyonifahamu walikuwa na taarifa za kukamatwa kwangu. (Kwa kipindi takriban miaka ishirini nyuma kwa nyakati fofauti nimekuwa nifanya mahojiano na radio zote muhimu kama, BBC, VOA, Sauti ya Ujerumani, Sauti ya Iran nk.).
Nikawaomba wale watu wa Usalama waniachie basi nende zangu kulala nyumbani nirudi hapo kesho asubuhi kwa kuwa sikuwa nimebeba madawa ya kulevya. Wakaniambia, “Itabidi tukulaze hapa hadi asubuhi wakubwa wetu watupe amri ya kukuachia. Maana amri ya kukukamata wewe imetoka juu.”
Mwandishi Akiwa Katika Studio za Radio Iran Tehran
Idhaa ya Kiswahili