Magufuli atoa mpya
na Mwandishi Wetu
WAZIRI wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, John Magufuli, amezijia juu halmashauri nchini na kuzitaka kuacha mara moja kuvunja nyumba za wananchi zilizojengwa katika maeneo ya makazi ambayo hayajapimwa.
Alitoa agizo hilo jijini Dar es Salaam jana, alipokabidhi barua ya toleo kwa wakazi wa eneo la Hananasif katika hafla iliyofanyika katika viwanja vya zamani vya Shule ya Msingi Hananasif.
Hakuna sababu ya kuwabomolea (waliojenga maeneo yasiyopimwa), kinachotakiwa ni kuwatambua na kuwapa huduma muhimu
wananchi kuishi maeneo holela si tatizo lao, ni tatizo letu, kwani wananchi walivamia maeneo hayo kwa sababu serikali haikuwa na utaratibu wa kuwatengea maeneo maalumu ya kujenga tangu awali, alisema Magufuli.
Alisema Sheria namba 4 na 5 ya Ardhi ya mwaka 1999 katika kifungu cha 3 (G) inawatambua wananchi wanaoishi katika maeneo yasiyopimwa na kuwa endapo maeneo yao yanatakiwa yabomolewe, wanatakiwa walipwe fidia kwanza.
Aliwaonya wakurugenzi wa manispaa zote na kusema kuwa sheria hiyo inawalinda wanaokaa katika makazi yasiyopimwa na kuwataka wananchi kuwachukulia sheria wakurugenzi watakaowabolea nyumba zao kwa kuwashitaki katika mabaraza ya ardhi na vyombo vingine vya sheria.
Magufuli aliwatahadharisha wakurugenzi watakaokaidi agizo hilo na kuendelea kuwabomolea wakazi wa maeneo yasiyopimwa na kueleza kuwa watakaokaidi agizo hilo watajifunza kwa kuwekwa ndani.
Aidha, aliwataka wakurugenzi hao kuacha kumpelekea barua za mapendekezo ya kubadilisha matumizi ya ardhi ya maeneo ya wazi na kudai kwamba watakaofanya hivyo, atazituma barua zao moja kwa moja kwa Rais Jakaya Kikwete na kusisitiza kuwa hatobadilisha hati hizo kama wanavyotaka.
Hata hivyo, alitoa wito kwa halmashauri zote nchini kuwa na mkakati wa kujenga makazi bora badala ya kubomoa na kutambua makazi yaliyojengwa holela kwa kutoa huduma muhimu.
Kutokana na Sheria ya Ardhi namba 4 na 5 ya mwaka 1999, ardhi ina thamani, ila iliyopimwa ina thamani zaidi na ni mtaji unaoweza kutumika kuwapunguzia wananchi umaskini kwa kuitumia kama dhamana ya kuombea mikopo katika taasisi za fedha.
Nawasihi wakazi wa Hananasif ambao hamjakamilisha malipo ya barua zenu za toleo mkamilishe, ili mpate barua za toleo, alisema.
Aliwaagiza wakurugenzi wa wizara wanaohusika na upimaji, ambao waliambatana naye, pamoja na maofisa wa Manispaa ya Kinondoni, kuanza mchakato wa kutoa hatimiliki kwa wananchi watakaopata barua za toleo, ambao idadi yao ni 1,423 na kati ya hao waliokamilisha taratibu za malipo ni 250.
Alisema shughuli za urasimishaji maeneo umeanza katika maeneo ya Isamilo jijini Mwanza na Mailimoja mjini Dodoma na kuwa huo ni ushahidi kuwa serikali inatambua maeneo yaliyojengwa holela, na kwa sasa serikali imeanzisha mradi wa kuzikopesha halmashauri 19, ili ziweze kuwapimia wananchi maeneo yao.
Akizungumzia mafanikio ya mradi wa urasimishaji wa maeneo uliofanyika Hananasif, mkazi wa eneo hilo, Hamisi Kaniki, alisema kuwa mwanzoni ilikuwa vigumu kwa wakazi wa eneo hilo kujua faida za kurasimisha maeneo, lakini sasa wengi wametambua hilo.
Kaniki alimuomba Waziri Magufuli awasaidie kutatua tatizo la kuvamiwa au kuchukuliwa kwa maeneo ya wazi ya eneo hilo, jambo linalosababisha watoto wao waende kucheza katika viwanja vya Biafra Kinondoni ambako nako alidai kuwa wamezuiliwa.
Akijibu, Magufuli alisema serikali tayari imeshatoa agizo la watu wote waliojenga maeneo ya wazi kuyaachia na kuwa wajiandae kuyabomoa hata kama ni taasisi za serikali, haziruhusiwi kujenga au kuchukua maeneo ya wazi.
Source: Tanzania Daima
Mya take: Jk keshapelekewa mangapi na kachukuwa hatua gani kwa wahusika?
Enewei komaa nao Magufuli.