Meya Kinondoni azidi kusuguana na Magufuli
2007-02-23 09:20:54
Na Simon Mhina
Meya wa Manispaa ya Kinondoni Mstahiki Salum Londa, amesisitiza kwamba uamuzi wa Baraza la Madiwani kuhusu kubomoa mgahawa maarufu wa Rose Garden upo palepale.
Akizungumza na Nipashe jijini Dar es Salaam jana, Bw. Londa alisema binafsi anamheshimu sana Waziri John Magufuli.
Hata hivyo, alisisitiza kwamba kama ambavyo yeye (Waziri) yupo kwa mujibu wa sheria, pia kikao cha madiwani kilichobatilisha umiliki huo, nacho kimewekwa kwa mujibu wa sheria.
`Unajua Sheria ya Ardhi imetungwa na Bunge ninachotaka kukisema hapa jamani, tufanye kazi zetu kwa mujibu wa sheria... Utawala bora maana yake ni kila mtu afuate sheria, kwa hiyo msimamo wetu upo pale,` alisema Bw. Londa.
Meya huyo alisema hataki kuingia kwa undani juu ya sakata hilo, wala kulitolea maamuzi binafsi kwa vile uamuzi wa awali, haukuwa wa kwake binafsi kama Londa, bali ni uamuzi wa Baraza la Madiwani.
Jana Waziri Magufuli alikaririwa na vyombo vya habari akinukuu vifungu kadhaa vya Sheria ya Ardhi, vinavyompa mamlaka ya kubadili matumizi ya ardhi husika.
`Wizara ya ardhi ndiyo inayosimamia masuala ya ardhi nchi nzima, na sheria zilizopo zinampa waziri mamlaka kubadilisha matumizi ya ardhi hata kama ni ya maeneo ya wazi, na mimi kama waziri nikaamua nibadilishe matumizi ya ardhi ile,` alisema Waziri Magufuli alipozungumza na waandishi juzi.
Alikaririwa akiwataka madiwani hao, kuacha mpango wa kubomoa mgahawa huo, vinginevyo wanaweza kujikuta wakimlipa fidia kwa uharibifu wowote, kwa vile anamiliki eneo hilo kwa mujibu wa sheria. Magufuli alisema atakuwa shahidi wa mmiliki wa mgahawa huo kama atalifikisha sakata hilo mahakamani.
Hata hivyo, Bw. Londa alisisitiza kwamba anavyojua yeye, hakuna mtu ambaye yupo juu ya sheria, anayeweza kujiamulia mambo kwa matakwa yake binafsi.
`Magufuli ni waziri, mimi ni meya. Ukitulinganisha ni sawa na bahari na mto, yeye mwenzangu ni bahari mimi ni mto. Mto unaweza kukauka lakini bahari ikaendelea kuwepo, lakini ni lazima niseme kwamba tufuate utawala wa sheria kwa vile japo mito inaonekana midogo na maji machache, lakini ndiyo inayojaza bahari,` alisema.
Alisema madiwani watakutana kujadili kauli ya waziri, lakini akasisitiza kwamba msimamo wa Manispaa haujatenguliwa.
Mapema mwezi uliopita, madiwani wa Manispaa ya Kinondoni, chini ya Meya Londa, walitoa tamko la kutaka mgahawa wa Rose Garden ubomolewe kwa vile hauko kwenye eneo la biashara wala makazi, bali kwenye hifadhi ya barabara.
SOURCE: Nipashe