Magufuli awekwa kikaangoni tena
na Mwandishi Wetu
MGOGORO wa kiwanja ilipojengwa baa maarufu ya Rose Garden jijini Dar es Salaam, umeanza kubadilika na kuchukua sura inayoonyesha jitihada za baadhi ya wakubwa serikalini kuutumia kumkaanga Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, John Magufuli.
Mpango huo ambao tayari unaonekana kuanza kuiva umemfanya waziri huyo kujiandaa kukabiliana na kile ambacho watu wake wa karibu wanakielezea kuwa ni mashambulizi ya wazi wazi dhidi ya mwanasiasa huyo aliyepata umaarufu mkubwa enzi za Serikali ya Awamu ya Tatu. Vyanzo vya habari vya kuaminika kutoka Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi na Manispaa ya Kinondoni vimeieleza Tanzania Daima kwamba, Magufuli anawekwa katika wakati mgumu kwa sababu ya uamuzi wake wa kumlinda mmiliki wa baa hiyo.
Wakati tayari Manispaa ya Kinondoni inalitaja eneo hilo la Rose Garden kuwa la hifadhi ya barabara, Wizara ya Ardhi inaliona vinginevyo. Kauli aliyoitoa Magufuli mwanzoni mwa wiki hii, wakati akizungumza na waandishi wa habari akimtetea mmiliki wa baa hiyo, akisema ana hati halali iliyotolewa na Kamishna wa Ardhi, tayari imepokewa kwa hisia tofauti na watu mbalimbali walio na masilahi yanayokinzana juu ya umiliki wa kiwanja hicho.
Uchunguzi uliofanywa na Tanzania Daima unaonyesha kuwa, Magufuli alitoa kauli hiyo akitumia kumbukumbu zilizopo wizarani hapo ambazo zinaonyesha kuwa kiwanja hicho hakipo katika hifadhi ya barabara. Dokezo linalohusu eneo hilo ilipo Rose Garden lililosainiwa na Kamishna wa Ardhi, Albert Msangi, ambalo Tanzania Daima imepata nakala yake linaonyesha kuwa barabara inayopita hapo iko katika kundi la Barabara za Mikoa (Primary Distributor Road) na si Barabara Kuu za Kitaifa.
Kwa mujibu wa dokezo hilo, ambalo linazingatia Mpango Kabambe wa Jiji la Dar es Salaam wa mwaka 1979, upana wa barabara za mikoa unapaswa kuwa wa kati ya mita 30 hadi 40 na carriage ya kati ya mita saba hadi 10, viwango ambavyo vinakidhiwa na Rose Garden, na hivyo kuifanya kuwa nje ya eneo la hifadhi ya barabara.
Kulingana na viwango hivyo, upana wa barabara ambayo upo sambamba na Rose Garden, inayounga Barabara ya Ali Hassan Mwinyi na Barabara ya Mikocheni, unatakiwa kuwa kati ya mita 30 hadi mita 40 kwa kuwa ni Primary Distributor Road.
Kwa mantiki hiyo, upana wa barabara iliyopo kwenye eneo hilo la Rose Garden unakidhi viwango hivyo vya mita 30 kwa carriage way, inatakiwa iwe kati ya mita saba hadi 10, kwa maelezo hayo eneo la Rose Garden halipo katika road reserve kama inavyodhaniwa (angalia kiambatanisho kinachoonyesha upana wa barabara kulingana na G.N 157 ya mwaka 1997 ), eneo husika limegawiwa kwa matumizi ya cafes and restaurants, linasema dokezo hilo.
Mbali ya dokezo hilo, Tanzania Daima pia imebaini kuwapo kwa mawasiliano ya barua kati ya Ofisi ya Waziri Mkuu na Waziri Magufuli kuhusu suala hilo la Rose Garden. Moja ya barua ambayo gazeti hili limeiona, imeandikwa na Waziri Magufuli kwenda kwa waziri mkuu ikitoa ufafanuzi wa uhalali wa umiliki wa kiwanja hicho. Barua hiyo ya Agosti 14, 2006, yenye kumbukumbu namba LD 247419 iliyosainiwa na Magufuli mwenyewe, inasisitiza kuwa eneo hilo limegawiwa kwa matumizi ya migahawa.
Sehemu ya barua hiyo ambayo ni majibu ya barua aliyoandikiwa Magufuli na Katibu wa Waziri Mkuu, B. Olekuyan, ya Agosti 4, 2006, yenye kumbukumbu namba PM/P/1/567/38, inasomeka: Mheshimiwa Waziri Mkuu, kwa mujibu wa sheria Na. 167 ya mwaka 1967 inayohusu hifadhi ya barabara, tangazo la serikali G.N 157 la mwaka 1997 likisomwa kwa pamoja na kifungu cha 78 cha sheria ya mipango miji na vijiji.
..Sura 378 (The Town and Country Planning (Town Planning Space Standards) Regulation, 1997) na kwa kuzingatia mchoro wa mipango miji na. 1/518/369 wa eneo la Mikocheni ilipo barabara ambayo iko sambamba na Rose Garden inayoungana na Barabara ya Ali Hassan Mwinyi.
..Inaonyesha eneo la Rose Garden halipo katika hifadhi ya barabara (Road Reserve) kama ilivyodhaniwa. Hali kadhalika, eneo hilo limegawiwa kwa matumizi ya cafes and restaurants.
Barua hii inadhihirisha kuwa msimamo wa Waziri Magufuli kuhusu mgogoro wa Rose Garden hauwezi kubadilika, na kwa sababu mmiliki wake analindwa na sheria ambazo Magufuli alizitumia kujibu barua aliyoandikiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu. Katika kuthibitisha kuwa Magufuli amekwishatambua mpango wa watu wanaotaka kummaliza kwa kutumia sakata la mgogoro wa umiliki wa kiwanja cha Rose Garden, hivi karibuni, akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake alisema haogopi matokea ya uamuzi wake.
Magufuli, ambaye mara kadhaa amekumbana na misukosuko, ikiwamo kuokotwa bunduki nyumbani kwake, anaonekana kuzidi kuandamwa baada ya hivi karubini kuzushiwa kuwa amefariki dunia akiwa nchini Ujerumani ambako alikuwa akitibiwa.