Wakuu, huu ni Uungwana kweli?
Huko Marogoro mwenye nyumba kamfungia ndani saa 27 mpangaji kisa amekiuka notisi
Katika hali isiyokuwa ya kawaida, mmiliki wa nyumba Plot namba 149 BLOCK ‘A’ Kihonda Kilimanjaro, Dk. Lusako Mwakiruma ilioyopo Mtaa wa Kilimanjaro Manispaa ya Morogoro, amemfungia ndani mpangaji wake kwa saa 27 kisha kumtolea vitu vyake nje, kwa madai kuwa mpangaji huyo, Paschal Paulo alishindwa kupokea notisi ya kumtaka ahame kwenye nyumba hiyo ndani ya mwezi mmoja.
Sheria ya Ardhi, [Sura ya 113, Toleo la Mwaka 2019] Kifungu cha 101 kinamruhusu mwenye nyumba kusitisha mkataba wa pango endapo mpangaji atashindwa kulipa kodi ya pango kwa siku 30. Hata hivyo, kabla ya kusitisha mkataba huo, mwenye nyumba anapaswa kumpa mpangaji notisi ya siku 30, akimtaka alipe kodi anayodaiwa, na endapo mpangaji atashindwa kufanya hivyo, mkataba huo utasitishwa. Notisi hiyo haipaswi kuwa chini ya siku 30, ila inaweza kuwa zaidi ya hapo. Endapo siku za Notisi zitaisha bila mpangaji kulipa deni lote, mwenye nyumba atasitisha mkataba na atakuwa na haki ya kumuondoa mpangaji katika nyumba yake.
Utaratibu wa kumuondoa ni kama ufuatavyo;
- Endapo mpangaji atakua tayari kuondoka mwenyewe kwa amani, mwenye nyumba atasitisha mkataba na kumuamuru mpangaji aondoke.
- Endapo mpangaji atagoma kutoka kwa amani, mwenye nyumba atatakiwa kufungua shauri Mahakamani kuomba amri ya mahakama/Baraza kumfukuza mpangaji katika nyumba ile, na atatumia dalali wa Mahakama au dalali wa Baraza la Ardhi na kumuondoa mpangaji katika eneo hilo.
Sheria haijaweka aina ya Notisi kwamba ni lazima iwe barua ya karatasi, barua pepe, tangazo, au ujumbe mfupi wa maneno (SMS). Hivyo mwenye nyumba ameachiwa uhuru wa kuchagua aina ya Notisi itakayotumika pia kwa kuzingatia urahisi wa mpangaji wake kuipata. Aidha, Sheria imeelekeza taarifa gani lazima ziwepo kwenye Notisi hiyo, ikiwa ni pamoja na;
- Aina ya uvunjifu wa mkataba uliofanywa na mpangaji;
- Kiasi kinachopaswa kulipwa kutokana na uvunjifu wa mkataba huo;
- Kipindi, kisichopungua siku thelathini tangu tarehe ya kupokea notisi, ili kulipa kiasi hicho;
- Na kwamba iwapo mpangaji huyo hatalipa kiasi hicho ndani ya siku 30 tangu kutolewa kwa Notisi, mkataba utavunjwa.
Sheria pia inaelekeza kwamba endapo mpangaji amekataa kupokea Notisi, au hapatikani kwa urahisi, Notisi hiyo inaweza kubandikwa sehemu yoyote iliyokaribu na eneo hilo ama kutangazwa kwenye gazeti kwa kuzingatia aina ya umiliki wa eneo hilo.
Kwa kuzingatia hii taarifa ya Morogoro, kuna mkanganyiko, kuhusu upokeaji wa Notisi, na kama tatizo ni ulipaji kodi, au ubadilishaji wa matumizi hata hivyo; kwa kuzingatia kwamba mpangaji alikataa kuondoka, mwenye nyumba alitakiwa kufungua shauri mahakamani ili aweze kurudishiwa eneo lake kutoka kwa mpangaji.