Zaidi ya Wanachama 113 wa Chama cha Ukombozi wa Umma (CHAUMMA) Mkoa wa Morogoro wamekihama chama hicho na kujiunga na Chama cha Wananchi (CUF), wakieleza kutoridhishwa na namna viongozi wa chama hicho ngazi ya Taifa wanavyoendesha shughuli zake.
View attachment 3664592
Wanachama hao, ambao wameongozwa na aliyekuwa Mwenyekiti wa Vijana wa CHAUMMA Mkoa wa Morogoro, Emanuel Mpesa, wameeleza kuwa wameamua kuchukua hatua hiyo baada ya kupoteza imani na baadhi ya maamuzi yanayofanywa ndani ya chama hicho.
Akizungumza wakati wa kuwapokea wanachama hao, Mwenyekiti wa Kamati Maalumu ya Jumuiya ya Vijana CUF Taifa, Ibrahim Bakonzi, amesema kujiunga kwao na CUF ni hatua itakayoongeza nguvu ya chama hicho, hususan Mkoa wa Morogoro.
Kwa upande wao, Emanuel Mpesa pamoja na Nabi Prosper, aliyekuwa mgombea wa nafasi ya udiwani katika Uchaguzi wa mwaka 2025 kupitia CHAUMMA katika Kata ya Mwembesongo, wamesema sababu kubwa ya kuondoka katika chama hicho ni mwenendo wa maamuzi yanayotolewa na viongozi wa juu.
Aidha, Makamu Mwenyekiti wa CUF upande wa Zanzibar, Haroub Mohammed Shamis, amesema chama hicho kipo tayari kushiriki mazungumzo na vyama vingine vya siasa kwa ajili ya maridhiano, akisisitiza umuhimu wa kudumisha amani, umoja na mshikamano wa Watanzania.