Kwenu Watu Makini wa Jamii Forums:
Maudhui yafuatayo yanaaminika kuwa ya kweli kabisa:
1. Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (inayotambulika hivi sasa) ilitungwa na kikundi cha watu wachache, ambao – kwa mantiki na mtazamo wao – waliandika rasimu ya waraka huu takatifu bila hata kushirikisha kikundi kidogo kabisa cha Watanganyika. Waraka huu ulifanana kwa karibu sana na nyaraka nyingi za kisheria ambaazo zilikuwa zikitumika wakati wa utawala wa kikoloni (British Protectorate) wa Waingereza. Muundo, mfumo, na hata istilahi inayotumika kwenye Katiba na sheria mbali mbali, vyote hivi vinafanana kwa karibu sana na mfumo wa Kiingereza. Unaweza hata kuingia kwenye wavuti wa Google.com na kutafuta nyaraka za kisheria za Uingereza, na kubaini kwamba zinafanana SANA na hizi za Kitanzania.
2. Baada ya Muungano na Zanzibar, Katiba ikarekebishwa kuuwezesha Muungano kutambulika kisheria. Mpaka leo bado tunashangaa na kujiuliza iwapo vifungu vya Mkataba wa Muungano viliingizwa vyote kwenye Katiba hiyo mpya "iliyochakachuliwa". Inatia shaka, pia, kama Mkataba wa Muungano ni waraka ambao uko hai na umehifadhiwa mahala fulani – Pa siri? – mbali na macho ya umma! Ni ukweli usiopingika kwamba Raia wa Tanganyika hawakushauriwa katika kutunga Katiba ya Muungano! Anayebisha kuhusu hili aje na ushahidi usiopingika: Nani alikuwapo, mashauriano hayo yalifanyika wapi na lini? Nini kilikubalika? Hapo ndipo kitakapoeleweka.
3. Katiba zote mbili – ile ya Tanganyika na ile ya Muungano – ziliweka msingi wa mfumo na muundo wa jinsi ambavyo sisi, Watanganyika na baadaye Watanzania, tungetawaliwa. (Jaribuni kutofautisha kati ya "kutawala" na "kuongoza".) Katiba hizo pia ziliweka msingi wa Serikali yetu iliyoundwa kwa kushabihiana na Serikali ya Uingereza, mfumo wake wa kisiasa pia "ukikopa" kwa kiwango kikubwa maudhui ya siasa za Kimaksisti na Kimao, ambapo mfumo wa chama kimoja uliwekwa na Mwenyekiti wa Chama ndiye aliyekuwa mtawala wa juu na mtawala pekee. (Hakuwa "kiongozi"!)
4. Kwa kuwa vyanzo vya Katiba yetu na mfumo wa Serikali ni vya kikoloni, ambavyo vimewaweka madarakani Wakoloni Waafrika, na kwa kuwa sisi – wananchi – kamwe hatukushauriwa katika uundwaji wake, kwa nini …..
1. Tumeamua kujiweka rehani kwenye nguvu zile zile za serikali ya kikoloni, tukifikiria na kuamini kwamba tukishiriki – wakati huu – katika uundwaji wa Katiba Mpya, tutakuwa huru?
2. Ni jambo gani linalotuzuia kuutupilia mbali mfumo huu wa serikali batili na haramu na kuanzisha mfumo wa serikali tunayoitaka wa kipekee, pamoja na katiba (ambayo haitokani na Serikali)?
3. Tumekubali kudanganywa na kughilibiwa ili tuamini kwamba – hivi sasa – kwa kuweka saini zetu kwenye rasimu hii ya Katiba Mpya na hatimaye kuipigia kura ili ipite, ndiyo nauli yetu ya kwenda kwenye nchi iliyo huru, wakati ukweli ni mwingine?
Tafakari. Chukua hatua!