Suala la mikataba kuletwa Bungeni, alianza Maua Daftari
Parl Questions - Principal Question(s)
Honourable Kabwe Zuberi Zitto [ CHADEMA ]
Kigoma Kaskazini Constituency
Session Number Principal Question Number To the Ministry of Sector Date Asked 22 June 2006
Kwa kuwa, Serikali imekodisha Uwanja wa Ndege wa K.I.A kwa muda wa miaka thelathini (30) kwa gharama ya dola za Kimarekani 1000 kwa mwaka:-
(a) Je, Serikali ipo tayari kuuleta Mkataba wa makubaliano ya kukodisha uwanja huo hapa Bungeni ili Wabunge waweze kuufahamu?
(b) Je, Serikali ipo tayari kuupitia upya Mkataba huo ili nchi ifaidike na mapato ya uwanja huo ambao ulijengwa kwa gharama kubwa?
ANSWERS TO PRINCIPAL QUESTION # 61 SESSION # 4
Answer From Hon. Dr. Maua Abeid Daftari INFRASTRUCTURE DEVELOPMENT
NAIBU WAZIRI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Miundombinu, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Kabwe Zuberi Zitto, Mbunge wa Kigoma Kaskazini, kwa pamoja kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Uwanja wa Ndege wa Kilimanjaro (KIA) umekodishwa kwa Kampuni ya Kilimanjaro Airports Development Company (KADCO) kwa Mkataba wa miaka 25 na sio 30. Katika ukodishaji huo Serikali ni mmoja wa wabia na ina hisa asilimia 24. Katika Mkataba huo kipo kipengele 30.4 ambacho kinatufunga pande zote mbili zinazoingia Mkataba huo kutoa habari kwa mtu yeyote ambaye si mhusika wa moja kwa moja na utekelezaji wa Mkataba huo.
Mheshimiwa Spika, mkodishaji ameweza kufanya mambo mbalimbali ya kuboresha kiwanja hicho ikiwa ni
-kulipia mkopo uliochukuliwa na Serikali,
-kufanyia matengenezo magari ya zimamoto na ukarabati wa Kituo cha Zimamoto,
-ukarabati wa paa ambalo lilikuwa linavuja, upakaji rangi majengo ya abiria, ukarabati a vyumba vya kufikia abiria na chumba maarufu,
-ujenzi wa barabara ya kutoka BP Fuel Farm hadi DAHACO,
-ununuzi na kujenga mitambo mbalimbali ya kuongozea ndege, misaada kwa taasisi za kidini, shule na afya na elimu kwa wafanyakazi na uboreshaji wa shughuli za mazingira.
Jumla ya Shs.8,772,896,600/= zilitolewa na KADCO kwa kazi hizo.
Wizara yangu imeona umuhimu wa kuupitia upya mkataba huo kipengele kwa kipengele kazi ambayo ilianza na bado inaendelea, shughuli hii inafanywa na jopo la wataalamu kutoka Wizara zifuatazo:- Wizara ya Fedha, Wizara ya Katiba na Sheria, Wizara ya Miundombinu, Wizara ya Mipango, Uchumi na Uwezeshaji na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha na Kilimanjaro. Tunategemea baada ya pande mbili kufikia muafaka, marekebisho hayo yatafikishwa katika ngazi za juu Serikalini kwa maelekezo zaidi.