hata wabunge hawana haki ya kuiona bali ni wanene wachache tu wenye haki hiyo!
~+~+~+~+~+~+~+~+~+~+~+~+~+~+~+~+~+~+~+~+~+~+~+~+~+~+~
Mikataba ya madini kutopelekwa bungeni
na Peter Nyanje na Rachel Chizoza, Dodoma
SERIKALI imesema haitakuwa tayari kupeleka bungeni mikataba mbalimbali inayohusu madini, kwani kufanya hivyo ni kukiuka kanuni na taratibu za miktaba husika, Bunge limeelezwa.
Kauli hiyo ilitolewa jana na Waziri wa Nishati na Madini, Nazir Karamagi, alipojibu swali la Mbunge wa Wawi, Hamad Rashid Mohamed (CUF), aliyeuliza swali la nyongeza bungeni hapo kuwa, serikali inatumia kifungu gani kuwanyima wabunge nyaraka mbalimbali za kiserikali pamoja na mikataba.
Waziri Karamagi alisema serikali haijakataa kumpa mbunge nyaraka mbalimbali zinazohusu serikali, lakini kuhusu mikataba, serikali haitakuwa tayari kuleta mikataba hiyo na kujadiliwa bungeni kwani mikataba hiyo huwa ni siri, hivyo kufanya hivyo itakuwa ni kuanika hadharani mikataba hiyo kitendo ambacho alisema hakiruhusiwi kisheria.
Naye Mbunge wa Viti Maalum, Halima Mdee (CHADEMA) katika swali lake la nyongeza, alisema serikali inaingia mkataba kwa niaba ya wananchi kwa maovu ambayo wanataka, hivyo kwa nini serikali haioni haja ya kuwapa wabunge mikataba hiyo nao waione, na badala yake mikataba hiyo imekuwa siri kubwa serikalini.
Akijibu swali hilo, waziri huyo alisema suala la mkataba wa biashara ni tofauti na suala la maovu, hivyo mbunge anaruhusiwa kupewa kipengele ambacho anaona ana shaka nacho, lakini si mkataba mzima.
Kwa kweli serikali haiwezi kuleta mkataba mzima bungeni, ili kila mbunge aweze kuuona, kwani mkataba ni suala la kiushindani, hivyo ukileta bungeni na kuanza kujadili huyu kafanya hivi kapata hivi, utakuwa unatangaza hadharani mkataba huo ambao ni siri na hauruhusiwi kufanyiwa hivyo, alisema.
Katika swali la msingi, mbunge, Hamad Rashidi Mohamed, aliitaka serikali kulieleza Bunge kuwa ilipanga kupitia mikataba mingapi na ni ipi kwa majina.
Akijibu swali hilo, Naibu Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja, alisema serikali ilipanga kupitia mikataba yote mitano ambayo iliingia na kampuni kubwa za uchimbaji wa dhahabu.
Mikataba hiyo ni kati ya serikali na Kampuni ya Bulyanhulu Gold Mine Limited inayomiliki mgodi wa Bulyanhulu ulioko katika Wilaya ya Kahama, Pangea Minerals Limited inayomiliki mgodi wa Tulawaka ulioko wilayani Biharamulo, North Mara Mine, wilayani Tarime, Geita Gold Mine Limited na Resolute Tanzania Limited inayomiliki mgodi wa Golden Pride, wilayani Nzega.
Hata hivyo, alisema kazi ya kupitia mikataba yote ilikamilika Julai 2006 na majadiliano kati ya serikali na kampuni moja moja yanaendelea, ili kuhakikisha taifa linanufaika ipasavyo na maliasili yake, lakini marekebisho ya mfumo wa kodi yanakusudiwa kufanywa katika sekta ya madini.