Filosofia ya Rorya
JF-Expert Member
- Sep 20, 2021
- 3,211
- 3,611
|
Taswira zote kwa hisani ya:
Brand Resource Center
Mnamo Agosti 4 - 6, 2014 US ilikuwa na mkutano baina yake na baadhi ya viongozi wa Afrika kujaribu kufufua mkataba wa AGOA (African Growth and Opportunity Act) ambao kimsingi ni sera ya Marekani ya biashara na uwekezaji baina yake na Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara ambao unaruhusu takriban bidhaa 6,800 za mkataba wa AGOA kuingia katika soko la Marekani bila ushuru.
Tanzania ilipoteza fursa kubwa katika mkataba wa kwanza wa AGOA. Hii ni kweli kutokana na kuwa vyama vya ushirika na bodi za mazao ya pamba ambavyo vilikabidhiwa jukumu la kusimamia mapinduzi ya kilimo katika sekta hiyo ya mazao ya pamba vikiwemo viwanda vya nguo; vyote vimetafunwa na mchwa-watu na kufanya kilimo kudorora na jitihada za kupunguza umaskini kwa wakulima wa mazao hayo kuwa ni bure tu. Hata hivyo ni dhahiri kuwa Tanzania ilitakiwa kuwezesha watu na taasisi zilizohusika na uzalishaji wa bidhaa za AGOA kupitia programu zake za MKURABITA na MKUKUTA I na II ili kufanikisha mpango huo, mfano kiwanda cha A to Z (sekta binafsi) ambacho ndiyo alama pekee ya mafanikio ya Tanzania katika mkataba huo wa AGOA kilifanikiwa kutumia vizuri fursa hii ya AGOA kutokana na uratibu makini na usimamizi madhubuti wa uendeshaji wake na kupata mafanikio hayo hali ambayo pia serikali (sekta pekee ya umma) ingeweza kuvipa uwezo wa makusudi na upendeleo viwanda vyake vya nguo, bodi za mazao ya AGOA vikiwemo vyama vya ushirika vya mazao ya AGOA.
Mkataba huo wa pili wa AGOA ulitazamiwa kwisha Septemba 30, 2015 na Afrika na US katika mtaguso huo waliomba uendelezwaji wake kwa matarajio kwamba una manufaa kwa nchi husika za Afrika. Katika kuchombeza mahusiano haya inasadikika AGOA hadi 2014 ilileta fursa za ajira zaidi ya 1m kwa Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara na zaidi ya fursa 100,000 za ajira kwa US. Katika nchi zote husika za Afrika haijulikani Tanzania ina idadi gani ya fursa za ajira katika hizo 1m zilizokokotolewa ili kudhihirisha umuhimu wa AGOA kwa nchi yetu ambayo kilimo ndiyo uti wa mgongo wa uchumi wake na ambacho ndicho kimeajiri asilimia 80 ya watu wake wote. Hapa inaonekana takwimu za fursa za ajira za AGOA kwa US ni kubwa kuliko za nchi moja moja za Afrika katika mkataba huu.
Wawakilishi wa vyama vya Democrat na Republican kwa pamoja katika mtaguso huo walihimiza kuwa ni kwa maslahi ya US kujitokeza na kushindania fursa zinazojitokeza za masoko Afrika ili kuendeleza mahusiano ya biashara na uwekezaji kati ya US na Afrika na kuimarisha na kuendeleza AGOA. Wenzetu weupe huwa hawaingii katika mikataba ambayo wanajuwa wazi kuwa hawaendi kunufaika nayo kwa asilimia kubwa hata tukikesha kuomba ili waingie kichwa kichwa.
Mnamo tarehe 5 Agosti, 2014 mwakilishi wa masuala ya biashara Michael Froman pia alitangaza kusainiwa kwa makubaliano ya kupanua wigo wa kibiashara na uwekezaji kati ya US na wanachama 15 wa ECOWAS. Thamani ya biashara kati ya US na ECOWAS ilikadiriwa kufikia USD 23.3bn. Thamani ya bidhaa za US kwenda ECOWAS ilikadiriwa kufikia jumla ya USD 9.9bn mwaka 2014 wakati bidhaa za kutoka ECOWAS kuingia US ikiwa ni USD13.4bn. AGOA ilichukuwa asilimia moja tu ya bidhaa zote zilizoingia katika soko la US, huku bidhaa ghafi za petroli zikiongoza kwa asilimia takriban 86 zikiwa ni USD11.8bn ya jumla hiyo.
Maswali magumu nyuma ya pazia yasiyokuwa na majibu bayana:-
1. Je, US katika kuimarisha na kuendeleza AGOA itaweza kutekeleza makubaliano haya pasina kuyahusisha na sera ya kuridhia ushoga ambayo inapigania iingizwe kwenye haki za bianadamu na iliishaweka msimamo wake wazi? Sera ya ushoga iliasisiwa na Wademokrat ambao ndiyo wanatawala sasa Marekani.
2. Je, dhamira ya US kuimarisha na kuendeleza AGOA ni hofu yake dhidi ya kasi ya kutisha ya Uchina katika Afrika? Hasa baada ya sera ya US ya ulinzi na usalama kuonekana kupwaya sana katika kuisaidia kukamata Afrika na kujikuta sera hiyo ikiipa zaidi gharama kubwa na pengine chuki tu huku faida ikiwa ndogo au hakuna kabisa.
3. Je, viongozi wa Afrika walijipanga vipi na mtego au agenda yoyote ya siri waliyojuwa na wasiyojuwa ya US katika AGOA? Naamini kila jambo lina mazuri yake na mabaya yake hata kama unalipewa bure bila kulitolea jasho... Wakati mema yake yako wazi ni budi pia mabaya au mapungufu yake nayo yakawa wazi ili pia kutekeleza sera ya uwazi na ukweli na kuondoa uwezekano wa lawama za baadaye pale macho na akili vitapofunguka na kubaini kuwa mapungufu yake hayakufanyiwa kazi kuyatatua.
4. Je, kuna haja ya Tanzania na nchi zingine za AGOA kutafakari kuendeleza mkataba huu ambao tangia awamu yake ya kwanza hawakuwahi kufaidika nao kwa manufaa ya umma mzima? Je, wamerekebishaje makosa na mapungufu ya utekelezaji wa awamu ya kwanza ya mkataba huu ili kuona kama taifa litanufaika nao katika muendelezo wake huo uliojadiliwa huko Washington DC?
5. Je, viongozi wa kiroho wameendeleaje kufuatilia kwa karibu mahusiano haya ya Afrika na nchi ambayo tayari imeweka wazi msimamo wake wa kuhusisha misaada na mahusiano mengine na sera ya ushoga (sera yake ya mambo ya nje lazima itambue haki za mashoga)? Naamini viongozi wa dini wanaweza kuona mahali ambapo viongozi wa kisiasa wasione kwa sababu viongozi wa dini wamewekewa na MUNGU Roho wa unabii ndani yao katika kutenda kazi zao za kuhudumia jamii kwa njia ya ibada ili waweze kuona mbali, kutoa unabii na kushauri nini kifanyike ili kuiepusha jamii na sintojuwa inayoweza kuinyemelea. Ikumbukwe kuwa mikataba hii huwa inaathiri kwa matokeo chanya au hasi mapato ya watu na hatimaye matoleo ya waumini katika nyumba za ibada.
6. Mbali na Rais Mugabe wa Zimbabwe na Museveni wa Uganda (hawa kwa misimamo yao dhidi ya ushoga nawafananisha na Cornelio ambaye hakuwa ameokoka lakini sadaka zake zilikubaliwa na MUNGU) ambaye mahakama ya nchi yake ilitengua sheria iliyopitishwa kwa dharura kupinga ushoga; kuwa ijadiliwe upya kwa mapana na wadau wote washirikishwe kwanza; (misimamo ya Mugabe na Museveni ilionekana kupingwa na US ikiihusisha na uminyaji wa haki za binadamu ambazo naamini hazijaridhiwa na taasisi yoyote ya kimataifa na kwamba Uganda na Zimbabwe hazijawahi kutia saini mkataba huo ambao haujawahi kuwepo duniani hata kwa dakika moja) misimamo ya viongozi hawa wawili ilikuwa wazi toka mwanzo kabisa, sasa je, walijuwa kilichokuwa nyuma ya pazia ya AGOA? Japo Mugabe hakuhudhuria mtaguso huo. Je, viongozi wenzao walikuwa nyuma yao dhidi ya sera ya ushoga? Licha ya mahakama ya Uganda kutaka sheria hiyo iangaliwe upya (wakati huo), naamini kuwa mahakama hiyo iliyo huru kabisa haina dini na wala haifungamani na dini yoyote japo naamini kuwa inatambua misimamo ya dini zilizopo kuwa zinapingana na ushoga ikiwemo dini ya upagani ambayo naamini baadhi ya wafuasi wake hawakubaliani na ushoga pia.
7. Je, tunapokuja kwenye muktadha wa Afrika moja kupitia AU, huu mpango wa US wa AGOA kwa haraka haraka ulionekana kuligawa bara la Afrika kwa sababu ulijikita katika Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara tu hata kwa bidhaa za petroli ambazo zinapatikana pia kwa uwingi na ubora usio wa kutilia shaka huko Afrika Kaskazini mwa Jangwa la Sahara. Kwanini katika ule mkataba wa AGOA na ECOWAS kuhusu bidhaa ghafi za petroli Afrika Kaskazini mwa Jangwa la Sahara haikuhusishwa? Je, hali hii haiwezi kuleta hisia za kuwa Afrika bado inatumikishwa kwa mkakati ule ule wa kikoloni wa kuligawa na kwamba mkakati huu unaweza kudhoofisha AU? Mbona China yenyewe haijabagua kati ya Kusini na Kaskazini mwa Jangwa la Sahara? Na kwamba inachukulia Afrika kama moja? Tayari Rwanda ilionyesha wasiwasi wake kuwa upande mmoja wa US katika AGOA hautegemewi kuipa tu fursa ya kuchota utajiri wa Afrika. MUNGU ibariki Afrika, MUNGU ibariki Tanzania.
majwalaoriko@yahoo.co.uk