By Edo Kumwembe (Facebook page)
read this piece...nimeandika leo
Mwanaspoti
Kuanzia Okocha, Ramsey, sasa Davido
na edo kumwembe
KATIKA dimba la uwanja wa taifa wa Ufaransa,
maarufu kama Stade de France, Juni 28,
1998, Watanzania walikuwa wameganda
katika luninga zao wakishindwa kuamini kuwa
timu ya Afrika waliyokuwa wanaishabikia
katika kombe la dunia ilikuwa imekufa
mabao 4-1 kutoka kwa Denmark.
Ndio, kama ilivyo kwa Waafrika wengine,
Watanzania walikuwa wamejipa ushabiki wa
timu ya taifa ya Nigeria. Lakini Peter Moller
akaipatia Denmark bao la kwanza. Brian
Laudrup akaipatia bao la pili, Ebbe Sand
akaipatia la tatu, Thomas Helveg akaipatia la
nne. Dakika mbili baadaye, Tijani Babangida
akaipatia Nigeria bao la kufutia machozi.
Kwanini Watanzania tulikuwa mashabiki wa
Nigeria? Kwanza kabisa walikuwa
wametukosha katika fainali za kombe la
dunia mwaka 1994 nchini Marekani. Pili
wakatukosha kwa kutwaa medali ya dhahabu
ya Olimpiki pale Atlanta Georgia Marekani.
Hata baada ya kupigwa na Denmark
Watanzania wakaendelea kuwa mashabiki wa
Nigeria. Mpaka leo bado wapo mashabiki wa
Nigeria nchini. Mashabiki wa damu. Lakini
unadhani wanigeria wana tofauti kubwa
kisoka na sisi? Hapana.
Wanigeria wanajituma katika kuhaha kutafuta
maisha. Taifa lao lina watu zaidi ya milioni
170 kwa sasa. Kila Mnigeria anajituma kadri
anavyoweza. Huyu anatapeli, yule anacheza
soka, huyu anaimba, mwingine anaanzisha
dhehebu feki la dini. Ili mradi mkono uende
mdomoni.
Na ni kwa njia hii ndio Wanigeria
wametugeuza kuwa mashabiki wao. Vipaji vya
wachezaji wao ni hivi hivi vya wachezaji wetu.
Tofauti ni katika kutafuta maisha. Yakubu
Aiyegbeni ndiye Edward Chumilla.
Waliomuona Sunday Manara
hawamtofautishi sana na Jay Jay Okocha.
Peter Rufai alikuwa kipa wa kawaida asiyefikia
uwezo wa Mohamed Mwameja wala Riffat
Said. Hata mabao manne waliyofungwa na
Denmark alichangia kiasi kikubwa kufungisha.
Baada ya soka lao, Watanzania tulihamia
katika filamu zao. Mama zetu, dada zetu, na
watoto zetu wakahamia katika kupenda
filamu za Kinigeria. Ukweli ni kwamba
hawakuwa na jipya sana ambalo sisi
hatukuwa nalo.
Mastaa wao Nouah Ramsey, Desmond Elliot,
John Okafor, Ini Edo na wengineo wana
vipaji ambavyo Tanzania vilionekana tangu
zama za akina Bishanga na wengineo. Tatizo
ni uwezo wa Wanigeria kubuni vitu viwili
vitatu kama vile kuingiza mambo mengi ya
kishirikina ambayo tulikuja kuyaiga.
Hata hivyo maudhui yao ni yale yale ya
kawaida ambayo wacheza filamu wetu
wameyazoea. Mara nyingi unakuta mtoto wa
tajiri amempenda maskini. Hakuna jipya
sana. hakuna sehemu ambayo wanaweza
kuangusha ndege kama Hollywood
wanavyofanya na filamu zao za kusisimua.
Tatizo hapa wacheza Filamu wetu hawajitumi.
Wengi hawana vipaji wala elimu. Wanacheza
filamu kwa sababu walikuwa Mamiss,
wanamitindo au wamerudi kutoka katika
shindano la Big Brother. Vinginevyo
hatuangalii vipaji. Tunaangalia wauza sura.
Matokeo yake tumejikuta tumerudi kuwa
mashabiki wa Filamu za Kinigeria bila ya
sababu za msingi. Hakuna unachoweza
kufanya zaidi ya kucheka. Mcheza filamu yuko
bize na matajiri kuliko kujikita katika kazi
yake apate pesa za kuwa tajiri.
Lakini kama vile haitoshi, baada ya Wanigeria
kutuchukua kutoka katika soka na Filamu,
sasa wametuteka katika muziki. Nenda katika
baa maarufu popote Tanzania, au nenda
katika ukumbi maarufu wa Disko ukasikie
jinsi nyimbo za mwanamuziki Davido wa
Nigeria zinavyotuteka.
Wimbo wake wa Aye kwa sasa ni kama
nyimbo ya taifa ya Muziki. Kabla ya hapo
wimbo wake wa Skelewu ulikuwa gumzo
lililopitiliza. Lakini ukichunguza sana katika
nyimbo zake, hakuna cha ajabu ambacho
Watanzania hawawezi kufanya.
Wimbo wa Aye unamuonyesha akiwa
shambani. Lakini kama Diamond Platinumz
akipiga nyimbo inayomuonyesha akiwa
mashambani watu watapuuza. Hata yeye
mwenyewe hataki. Aliwahi kufanya wimbo
mmoja akiwa kijijini, lakini haukuvuma.
Na ndio maana sasa anafanya video za
kifahari Afrika Kusini ambapo anaonekana
akirekodiwa kutoka angani na vifaa vya
kisasa. Kwanini Davido anatuteka zaidi ya
Diamond? Kwanza ni kwa sababu ya kupenda
Unigeria ambao umetuingia.
Lakini pili wenzetu wamefanikiwa kujitangaza
kimataifa. Vipaji ni vile vile tu, lakini kama P
Square wanafanya wimbo na Ricky Ross huku
wewe unamtafuta Jackline Wooper na
kujaribu kumfanya kuwa mwanamuziki ili auze
sura katika wimbo wako wakati hana kipaji
chochote cha muziki.
Muziki wanaoufanya Wanigeria tunaweza
kuufanya. Mimi ni mmoja kati ya watu
wanaoamini hilo. Tatizo ni wanamuziki wetu
kukosa ubunifu, au Watanzania wenyewe
kuwa wepesi katika mapokeo....