Parabolic
JF-Expert Member
- Dec 3, 2013
- 2,922
- 3,252
***
Serikali, kupitia Baraza la Taifa la Usalama Barabarani, ilitoa siku 21 kwa wamiliki wa vyombo vya moto kuhakikisha wanaviingiza katika Mfumo wa Uratibu wa Ukaguzi (MIMIS) na kukamilisha taratibu zote za kisheria zinazohitajika.
Kwa mujibu wa taarifa, wamiliki wote wa vyombo vya moto wanatakiwa kusajili na kuingiza vyombo vyao katika mfumo huo kufikia Julai 31, 2026. Serikali ilieleza kuwa baada ya muda uliotolewa kumalizika, kutakuwa na operesheni maalumu ya kuchukua hatua dhidi ya wale watakaoshindwa kutekeleza agizo hilo kwa wakati.
Baadhi ya vituo vya uhakiki vimeanzishwa kwa ajili ya zoezi hilo, ambalo bado linaendelea. Binafsi, nimefanikiwa kufika Kituo cha Polisi Kawe ambacho ni kituo mojawapo katika Jiji la Dar es salaam, lakini nimelazimika kusubiri kwa zaidi ya saa saba ili kupata huduma.
Nilifika majira ya saa mbili asubuhi na nikaendelea kusubiri hadi saa tisa mchana, pamoja na wananchi wengine wengi waliokuwa wakisubiri huduma. Hali hii inasababisha wananchi kupoteza muda mwingi kwa ajili ya zoezi ambalo lingeweza kukamilika kwa haraka zaidi kama kungekuwa na maandalizi ya kutosha.
Ushauri wangu kwa Serikali ni kuongeza muda wa kujiunga na mfumo huo ili kuwapa fursa wananchi wengi zaidi kukamilisha zoezi la ukaguzi. Aidha, ni muhimu kuongeza idadi ya vituo vya ukaguzi ili kurahisisha upatikanaji wa huduma na kupunguza msongamano endapo Serikali inaona zoezi hili lina umuhimu mkubwa.
Lakini watu wengi bado hawana taarifa kuhusu kujiunga na mfumo huu, zimechelewa kuwafikia wananchi. Wapo watu wengi walengwa ambao bado hawana taarifa kuhusu zoezi hilo, hususan kuhusu muda wa mwisho uliowekwa.
Hivyo, nashauri Serikali iongeze juhudi za kutoa elimu na kusambaza taarifa kwa wananchi kupitia njia mbalimbali za mawasiliano ili kuwafikia watu wengi zaidi, badala ya kusubiri muda wa mwisho ufike kisha kuanza kuwatoza faini wale ambao hawakupata taarifa kwa wakati.