Date::8/20/2008
Wabunge washauri serikali ya Mapinduzi Z'bar ifutwe
Tausi Mbowe, Dodoma
Mwananchi
MJADALA wa Muungano umeingia katika sura mpya baada ya wabunge kuibua madai ya kutaka iundwe serikali moja ya Muungano badala ya mfumo wa sasa wa serikali mbili.
Kauli hiyo ya wabunge imetolewa wakati tayari Muungano umekuwa ukitikiswa kwa nguvu kutokana na hoja ya Zanzibar si nchi au la.
Wakichangia makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano), kwa nyakati tofauti wabunge hao, wengi wao wakiwa wanatoka Bara walisema, dawa pekee ya Muungano huo ni kuundwa kwa serikali moja ya Jamhuri ya Muungano, ingawa dawa hiyo ni chungu.
Dawa pekee ya Muungano ni kuelekea katika serikali moja ya Jamhuri ya Muungano, ingawa dawa hiyo ni chungu lakini hii ndio italeta Utanzania wa kweli, badala ya kuwa na serikali mbili au tatu, alisema Mbunge wa Mchinga (CCM), Mudhihir Mudhihir.
Mudhihir alisema, mtafaruku unaoendelea sasa kutokea bungeni, ni mazoea na tamaa za utawala kwa baadhi ya viongozi na kulazimisha kulumbana kwa kugombea majina au serikali kila upande, jambo ambalo halina mantiki kwa sababu majina hayo (Tanganyika na Zanzibar) hakuna anayejua maana yake.
Mjadala huo ulionekana wazi kuwagawa wabunge kwa misingi ya utaifa, ambapo Wazanzibari walionyesha wazi kutaka kuundwa kwa serikali tatu, huku Watanganyika wakitaka serikali moja.
Wabunge wa CCM na CUF, wanaotoka katika visiwa vya Zanzibar waliungana katika hoja ya kuwa na serikali tatu.
Awali, Mbunge wa Kongwa, Job Nugai (CCM), alisema ni matarajio yake kuwa na serikali moja ambayo Rais wa Zanzibar atakuwa Makamu wa Rais, itakuwa ndiyo jibu la matatizo ya Muungano na si kuwa na serikali tatu.
Hoja hiyo iliungwa mkono na Mbunge Nkasi, Ponsian Nyami (CCM) na kutahadharisha kuwa iwapo Muungano utavunjika, sababu itakuwa chokochoko za Wazanzibari ambao wameshindwa kuwa wawazi kuhusu mustakabali wa Muungano.
Mbunge wa Kilwa Kaskazini, Samson Mpanda (CCM), alitahadharisha kwamba, Wazanzibari wana kitu wanachokitaka kupitia hoja hiyo na kuwataka wawe wazi badala ya kufanya mambo chini kwa chini kwa kisingizio cha kutaka kuundwa kwa serikali tatu ya Tanganyika.
Mbunge wa Nzega, Lucas Selelii (CCM), aliwaonya watu wanaotaka kuvunja Muungano akisema kuwa, ni hatari kwa kuwa utarudisha nyuma maendeleo ya taifa hili.
Selelii alisema, hasara ya kuvunja Muungano ni kubwa zaidi inavyofikiriwa na kuwataka Watanzania kusonga mbele kwa kuwa na serikali moja badala ya tatu.
Wakati Wabunge kutoka Tanzania Bara, wakitaka kuundwa kwa serikali moja, wabunge kutoka visiwani ambao wote waliosimama kuchangia hoja hiyo walitaka kuundwa kwa serikali ya Tanganyika ili kuwe na serikali tatu.
Mbunge wa viti maalumu, Maulida Komu (Chadema), alisema haungi mkono hoja kwa sababu inamtesa moyoni kutokana na usiri mkubwa uliopo katika hoja hiyo.
Komu ambaye alionyesha kushangazwa na kitendo cha Rais wa Jamhuri ya Muungano kuingia wa kwanza wakati wa sherehe za Mapinduzi ya Zanzibar na Rais wa Zanzibar kuwa wa mwisho.
Alisema hizo ni kasoro za Muungano na kutaka zirekebishwe haraka
kwa kuwa Rais wa Jamhuri ndiye Rais wa Tanzania Bara na Visiwani.
Awali, Mbunge wa Magomeni, Mohamed Amour Chomboh (CCM), alionya watu wanaovaa ngozi ya kondoo wakati ni chui, akimaanisha baadhi ya wabunge waliokuwa wakitoa kauli za kukebehi kama Zanzibar si nchi wakati ina bendera na wimbo wake wa taifa.
Naye Mbunge wa Konde, Dk Ally Taarabu Ally (CUF), alisema umefikia wakati kwa serikali kuwashirikisha wananchi ili kupata suluhisho sahihi la Muungano.
Kauli hiyo pia iliungwa mkono na Kamati ya Bunge ya Katiba, Sheria na Utawala ambayo iliishauri serikali kuchukua changamoto zote zilizojitokeza kuhusu Muungano na kuzipatia ufumbuzi wa kudumu kwa kuwashirikisha wananchi.
Akizungumza kwa niaba ya Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mbunge wa viti maalumu, Pindi Chana, alisema wakati umefika kwa serikali kuanzisha mjadala wa kitaifa kwa lengo la kuwashirikisha wananchi kujadili suala hilo.
Naye msemaji mkuu wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Riziki Omar Juma, alisema muundo na mfumo wa Muungano ndio unaosababisha matatizo hayo, kwa kuwa Katiba ya Jamhuri ya Muungano na sheria
nyingine zimeshindwa kuzingatia na kutambua maana, dhamira na matakwa halisi ya Muungano huo kupitia hati za awali za Muungano.