bandari ikiwa huru inamaanisha z'bar itakosa robo tatu ya mapato ya kodi. si utaua nchi.
credit crunch bado unaongelea mambo ya misaada...
angalia mkoa wa kinondoni una watu sawasawa na z'bar lakini angalia z'bar ilivyokuwa na viongozi wengi...
mwanza ni kubwa na idadi ya watu ni mara mbili na uchumi wake ni mkubwa kuliko wa z'bar. ni uongozi wenu ndio unaharibu z'bar na sio bara. z'bzr needs efficient management, na sio "hapa pangu".
Mafuta yaongeza mgogoro wa Muungano
Na Salma Said, Zanzibar
KUNA dalili kwamba mzimu wa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere kuhusu Zanzibar, unaanza kuumomonyoa Muundo wa Serikali ya Muungano, baada ya wawakilishi wa CCM na CUF kuungana na kudai kuna upungufu mwingi katika mambo yaliyokubaliwa katika hati ya Muungano mwaka 1964.
Madai hayo yalitolewa jana wakati wajumbe wa Baraza la wawakilishi walipokuwa wakichangia mjadala baada ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ), kuwasilisha taarifa yake juu ya mapendekezo ya uendeshaji wa kazi ya utafutaji na uchimbaji mafuta na gesi asilia katika visiwa hivyo.
Kikao hicho kilichoongozwa na Ali Mzee Ali kilielezea mengi kutoka kwa wajumbe kuhusiana na kutoridhishwa na ushauri wa Mshauri Mwelekezi juu ya utafutaji wa mafuta na gesi asilia.
Mwakilishi wa Jimbo la Mkanyageni (CUF) Haji Faki Shaali alisema, hakuna haja ya SMZ kukubali kulifanya suala la mafuta na gesi asilia, kuwa chini ya Muungano.
Akitolea mfano Muungano wa nchi za Kifalme za Emirates (UAE), Shaali alisema, kila nchi katika muungano huo inatumia rasilimali zake bila kuingiliwa na nyingine.
Naye mwakilishi wa jimbo la Amani (CCM), Ali Denge Makame alisema kutokana na Tanzania Bara kuwa na rasilimali nyingi, ni busara mafuta na gesi asilia iliyoko Zanzibar, vikaachiwa SMZ kama ilivyo tanzanite, dhahabu na madini kwa Tanzania bara.
Aliwashauri wawakilishi wenzake waafiki mpango wa kukataa pendekezo la kutumiwa kwa maeneo ya bahari kuu na Serikali ya Muungano kutokana na eneo hilo kuwa la Zanzibar na lina vyanzo vingi vya nishati.
Kiongozi wa upinzani katika Baraza la wawakilishi Abubakar Khamis Bakari, alisema suala la mafuta liliingizwa kinyemelela kwa hila za Rais Nyerere katika mambo ya Muungano.
Bakari alisema, chini ya mfumo wa chama kushika hatamu, Serikali ya Muungano chini ya uongozi wa Hayati Nyerere, ilitumbukizwa suala la mafuta na gesi bila ridhaa ya SMZ licha ya kuwa hatua kadhaa zilichukuliwa kutaka suala hilo litolewe.
Mwaka 1984 mimi nilikuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali. Nilipoona dalili chafu, niliwaendea wakubwa wangu Rais marehemu Idris Abdul Wakil na Waziri Kiongozi wake Maalim Seif Sharif Hamad kuwaeleza kuna tatizo na wao wakaniambia niende Tanganyika kwa majadiliano zaidi, alisema.
Alisema alipofika Tanganyika, alikutana na Waziri Mkuu Dk Salim Ahmed Salim na Mwanasheria Mkuu wa serikali wakati huo akiwa Jaji Joseph Warioba na kwenda nao hadi Msasani nyumbani kwa Mwalimu Nyerere kujadili suala hilo kwa undani.
Khamis alizidi kuliambia Baraza la Wawakilishi kuwa, Nyerere alikubali kuwa jambo hilo limeingizwa kinyemela na litashughulikiwa kisheria lakini jambo la kushangaza hadi leo hii limebaki bila kutolewa uamuzi.
Mwakilishi huyo alimtahadharisha Waziri wa Maji, Ujenzi, Nishati na Ardhi, Mansoor Yusuf Himid kwamba, asikubali kuahidiwa urais na kuanza kuwageuka wawakilishi wenzake na ikiwa atafanya hivyo, atahukumiwa na umma wa Wazanzibari.
Akichangia mjadala huo Mwakilishi wa Jimbo la Magomeni (CCM) Salmin Awadh Salmin, aliitaka SMZ kufanya haraka kuunda chombo cha Udhibiti na Usimamizi wa nishati ya Mafuta na Gesi Asilia bila kuzubaa na kusubiri kwani wakati wake umeshafika kufanya hivyo.
SMZ iunde ZPDC yake haraka haraka kama ilivyofanya wakati wa kuunda Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa serikali na Elimu ya Juu na hilo halina haja ya kusubiri ushauri wa mtaalam mwelekezi Alisema mwakilishi huyo huku akipongezwa na pande mbili za vyama hivyo.
Salmin alisema, hata suala la uvuvi katika bahari kuu ni la muungano lakini Serikali ya Muungano inaendesha kazi hizo bila kuishirikisha SMZ.
Mwakilishi wa Chambani (CUF) Abass Juma Muhunzi alisema, utata wa mafuta na gesi asilia ni matokeo ya kuchezewa na kufinyangwafinyangwa kwa mkataba wenye masuala 11 ya muungano mwaka 1964 na kuongezwa mambo mengine bila idhini ya Wazanzibari.
Muhunzi alisema Zanzibar imepoteza sauti katika medani za Kimataifa na sasa inadidimia kiuchumi na hata taasisi za kimataifa na kampuni kubwa ziko Bara.
Kwa upande wake mwakilishi wa Jimbo la Gando (CUF) Said Ali Mbarouk, alisema huenda sheria ya mafuta kutajwa kuwa itafanya kazi Tanzania Bara na Tanzania Visiwani, imekusudiwa katika visiwa vya SongoSongo, Mafia na Ukerewe na si Zanzibar.
Awali akiahirisha kikao hicho jana mchana, Spika wa Baraza la Wawakilishi Pandu Ameir Kificho, aliwataka wawakilishi kujadili hoja hiyo bila jazba kwa lengo la kujenga na kutazama maslahi ya umma.
Spika huyo na Waziri Kiongozi wa SMZ Shamsi Vuia Nahodha, hawakuhudhuria kikao cha majadilano hayo kilichoanza saa 11 jioni hadi saa 1.45 usiku.
Kesho wawakilishi hao wanatarajia kuendelea na mjadala huo wakijadili ripoti ya Mshauri Mwelekezi na maoni ya serikali yaliowasilishwa katika kikao hicho.