Date::4/15/2009
Waziri Himid:
Elias Msuya
Suala la mafuta limekuwa likijadiliwa kwa muda mrefu. Hoja inayogonga vichwa vya watu ni kama mafuta hayo yanufaishe pande zote za Muungano (Bara na Visiwani) au yabaki kuwa ya visiwani Zanzibar pekee.
Hivi karibuni Waziri wa maji ,ujenzi nishati na ardhi wa Zanzibar Mansoor Yusuf Himid akilihutubia Baraza la wawakilishi alilizungumzia suala hilo. Kwa kuanza Waziri Himid anaanza kueleza jitihada za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuanza uchimbaji wa mafuta hayo,
"Tangu Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuzuia kazi ya Utafutaji Mafuta na Gesi asilia kwa Kampuni ya Antrim ya Canada mwaka 1997 licha ya kutolewa Leseni na TPDC kwa kazi hiyo katika eneo la Zanzibar, eneo la utafiti ambalo linahusisha maeneo ya Zanzibar kama yalivyoelezewa katika Katiba ya Zanzibar 1984, Sura ya Kwanza kifungu 2.(1), kumekuwa na juhudi kadhaa za Kidiplomasia na Kisiasa katika kulipatia ufumbuzi suala hilo.
Kibali cha utafiti kwa eneo la visiwa vya Zanzibar na bahari iliyozunguka visiwa hivyo kilitolewa kwa TPDC katika mwaka 1997.
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,TPDC na Kampuni ya Antrim ziliingia katika mkataba wa uchimbaji (Production Sharing Agreement) tarehe 29 Januari 1997 kwa mkataba ambao ulitengenezwa na Wizara ya Nishati na Madini (SMT).
Antrim kwa mujibu wa mkataba huo walitakiwa kuanza kazi za kukusanya taarifa za kitaalamu za mtetemo kwa kuhusisha eneo la kilomita 100 kisiwani Pemba, kilomita 100 kisiwani Unguja na kilomita 200 kwa eneo la baharini kwa gharama ya Dola za Kimarekani Milioni 3.5 kwa miaka miwili ya mwanzo kuanzia Aprili 2002 mpaka Aprili 2004.
Kwa kipindi cha miaka miwili mengine inayofuata kuanzia Aprili 2004 mpaka April 2006 walitakiwa wachimbe kisima cha utafiti wa mafuta kwa maeneo ya Kaskazini Pemba kwa gharama ya Dola za Kimarekani Milioni 4.
Kwa mujibu wa ramani ya eneo la utafiti huo (Antrim Block) vilihusisha Visiwa vyote vya Zanzibar na Bahari yake bila ya ridhaa na ushauri wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Kwa nini mafuta yalitolewa kwenye orodha ya mambo ya Muungano? Waziri Himid anasema,
"Baada ya serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuzuia Kampuni hiyo kuanza utafiti huo kwa maeneo hayo, hatimae suala hili likawa ajenda mojawapo ya kikao cha kwanza cha kujadili kero za Muungano baina ya Waziri Mkuu na Waziri Kiongozi.
Ndani ya Kikao hicho, msimamo wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ukawa ni kuliondoa suala la Mafuta na Gesi asilia kutoka katika Orodha ya Mambo ya Muungano au kuyafanya madini yote kwa jumla kuwa ni ya Muungano.
Hata hivyo, katika vikao vilivyofuata, pande mbili hizi zikakubaliana kutafuta Mshauri Mwelekezi atakayezishauri Serikali zote mbili juu ya namna bora ya kugawana rasilimali hiyo. Kampuni ya AUPEC ya Uingereza ikashinda zabuni ya kufanya kazi hiyo.
Mshauri huyo alipewa hadidu za rejea zilizoridhiwa na pande zote mbili kama muongozo wa kukamilisha kazi hiyo, na Kampuni hiyo ilianza kazi tarehe 20 Juni 2007"
Pamoja na kumpata Mshauri huyo, bado ameonesha mapungufu kadhaa ambayo yamejitokeza katika utekelezaji wa kazi hii ya utafutaji na uchimbaji wa Mafuta na Gesi asilia ndani ya Jamhuri ya Muungano Tanzania, mambo ambayo zaidi yanaiathiri Zanzibar kimapato. Himid anaeleza,
"Japo kuwa TPDC (Tanzania Petroleum Development Corporation) lilianzishwa kwa tamko la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tarehe 26 May 1969 na Sheria ya Makampuni ya Umma ya 1969 ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kurekebishwa na Sheria mpya ya mwaka 1992 inayotumika hivi sasa huko T/Bara na ambayo ilianzishwa kwa ina sura na tafsiri ya chombo cha Muungano kinachosimamia utoaji wa leseni za utafutaji na uchimbaji wa mafuta na gesi asilia katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ushirikishwaji wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar hususan kwa masuala yanayohusiana na mafuta na gesi asilia haupo. Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inawakilishwa na mjumbe mmoja tu kutoka Wizara ya Maji, Ujenzi, Nishati na Ardhi ndani ya bodi ya TPDC." anasema
Akielezea jinsi Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itakavyopoteza mapato kwa kuundwa kwa Taasisi mbili yaani Wizara ya Mafuta ya Muungano na TPDC, Waziri Himid anasema,
"Katika Ripoti hii Mshauri Elekezi anapendekeza kuundwa kwa Wizara itakayoshughulikia Mafuta chini ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania. Hii maana yake ni kwamba Wizara hiyo itakuwa na Makao Makuu yake Tanzania Bara kama zilivyo Wizara nyengine za Muungano.
Vyombo hivyo viwili pia ndivyo vitakavyokuwa na mamlaka ya kutoa leseni kwa makampuni mbali mbali yatakayojihusisha na uchimbaji wa mafuta na gesi asilia.
Zaidi ya hayo, suala hili la kuundwa kwa Taasisi mbili hizi na kuwa na sura ya Kimuungano zitainyima Zanzibar Mapato ya Mrahaba "Royalties" ambayo kwa mujibu wa taratibu yatatakiwa kulipwa katika taasisi inayosimamia usajili na utoaji wa leseni ambayo itakuwa ni Wizara ya Mafuta na TPDC.
Akieleza athari ambazo Zanzibar itazipata kutokana na kutopata kodi za mapato, kwa kutoshirikishi kikamilifu kwenye usimamizi wa mafuta hayo, Himid anasema,
"Kodi ya Mapato inayolipwa na Watu Binafsi na Mashirika ni suala la Muungano na linasimamiwa na Sheria ya kodi ya Mapato ya mwaka 2004. Kwa hali ya sasa hivi kwa mujibu wa Sheria hii, Mapato yanayotokana na kodi ya Mapato kwa upande mmoja wa Muungano yanapokusanywa huwa yanabakia katika sehemu ile ya Muungano .
Hivi sasa, kwa upande wa Mashirika kodi ya mapato kwa kampuni husika huwa inalipwa pale kampuni iliposajiliwa na yalipo Makao Makuu yake.
Kutokana na Mapendekezo ya Mshauri Elekezi ya kuundwa kwa Wizara ya Mafuta na TPDC kupewa mamlaka ya kusajili, kutoa leseni na usimamizi wa utafutaji na uchimbaji wa mafuta na gesi asilia, Kampuni zote za uchimbaji wa mafuta zitasajiliwa na vyombo hivyo viwili na mapato yote ya kodi ya mapato kwa makampuni italipwa Tanzania Bara na hivyo kutokuchangia chochote katika Mfuko wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Kodi nyengine ya Mapato ambayo itakosekana kwa upande wa Zanzibar ikiwa Makampuni yatakuwa yanapewa leseni na kusajiliwa Tanzania Bara ni Kodi ya ufundi stadi (SDL) ambayo huwa inalipwa kila mwezi kwa mujibu wa asilimia ya mishahara ya wafanyakazi. Mfano wa Taasisi hizo ni BOT, JWTZ, Jeshi la Polisi, Usalama wa Taifa" anasema.
Akieleza jinsi suala la mafuta lilivyoingizwa kwenye katiba, Waziri himid anasema,
"Suala la mafuta liliingizwa katika Katiba mwaka 1984 baada ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitisha Sheria ya Mafuta ya mwaka 1980 inayosimamia Utafiti na Uchimbaji wa Mafuta na Gesi Asilia.
Hata hivyo ikumbukwe kwamba katika Mkataba wa muda wa Muungano wa Jamhuri ya Tanganyika na Jamhuri ya Watu wa Zanzibar 1964, haikuhusisha kabisa suala la mafuta katika vipengele kumi na moja vya kushirikiana vya makubaliano hayo kama ifuatavyo:-
Katiba na Serikali ya Jamhuri ya Muungano, Bunge na Serikali na vilivyotajwa kuwa na mamlaka ya mwisho juu ya mambo yote yahusuyo Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Mambo ya Nchi za Nje, Ulinzi, Polisi, Mamlaka juu ya mambo yanayohusika na hali ya hatari, Uraia, Uhamiaji, Mikopo na Biashara ya Nje, Utumishi katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kodi ya mapato inayolipwa na watu binafsi na mashirika,ushuru wa forodha na ushuru wa bidhaa zinazotengenezwa nchini na kusimamiwa na Idara ya forodha, Bandari, mambo yanayohusu usafiri wa Anga, Posta na simu.
Ni dhahiri kuwa suala la Mafuta na Gesi Asilia halikuwemo kabisa katika makubaliano ya Muungano ya mwanzo (matters within the first schedule to the Union Constitution)." anasema Waziri Himid.
Tuma maoni kwa Mhariri