Mwanasheria Mkuu amchambua Lowassa
2008-03-03 08:41:37
Na Mwinyi Sadallah, Zanzibar
Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar, Bw. Idd Pandu Hassan, amesema Bw. Edward Lowassa hastahili kuitwa Waziri Mkuu Mstaafu kwa vile hakufikisha kipindi cha miaka mitano, ambapo angestahili kuitwa mstaafu.
Aliyasema hayo katika mahojiano maalum na Nipashe juu ya nafasi ya wastaafu wanaoondoka kwa sababu mbali mbali, ikiwemo tuhuma za ubadhirifu.
Mwanasheria Mkuu alisema kwa mujibu wa sheria za viongozi wastaafu hutakiwa kutumikia serikali kwa miaka mitano na sio chini ya hapo, ili uweze kunufaika na mafao yote ya wastaafu.
Bw. Pandu alisema sheria hiyo haina tofauti na ile ya watumishi serikalini, kwa vile huwezi kuitwa mstaafu hadi ufike umri wa miaka 55 hadi 60 na hapo ndipo pia unastahili kulipwa mafao yako.
``Huwezi kumwita Bw. Lowassa kuwa ni Waziri Mkuu Mstaafu au Waziri Mkuu aliyefukuzwa kwa vile alijiuzulu mwenyewe na hasa unaweza kumwita `aliyekuwa Waziri Mkuu`, basi,`` alisema.
Hata hivyo, alisema mtu anaweza kumuitwa waziri mkuu mstafu kwa lugha ya kisiasa tu ili kuendeleza umoja na mshikamano, kama ilivyotokea kwa viongozi wengine waliondoka madarakani kwa matatizo.
Alisema wapo viongozi wanaoitwa wastaafu katika lugha ya kisiasa, lakini hawana sifa za kuitwa hivyo na kutoa mfano wa aliyekuwa Waziri Kiongozi wa Zanzibar, Bw. Seif Sharif Hamad.
Alisema Bw. Hamad hana sifa ya kuitwa Waziri Kiongozi Mstaafu kwa vile hakutumikia kipindi cha miaka mitano, lakini amekuwa akinufaika na kulipwa mafao yake baada ya kufikiwa muafaka wa mwaka 2001, ili kujenga umoja na mshikamano.
Alisema viongozi wengine wamekuwa wakiitwa wastaafu kwa lengo la kuleta umoja na mshikamano katika taifa, kama vile Mzee Aboud Jumbe Mwinyi na Mzee Ramadhan Haji Faki ambaye aliwahi kuwa Waziri Kiongozi.
Bw. Pandu alisema viongozi hao hawakuondoka kwa utaratibu wa kustaafu, lakini kwa kuzingatia umoja na mshikamano wa taifa ndio maana wanaitwa viongozi wastaafu na kulipwa mafao yao kama kawaida.
Hata hivyo, alisema Bw. Lowassa atabakia kama kiongozi aliyejiuzulu mwenyewe kwa vile Bunge halikupiga kura ya kutokuwa na imani naye.
Bw. Hamad alifukuzwa katika CCM kutokana na kwenda kinyume na maadili ya chama, chini ya aliyekuwa Mwenyekiti wa chama hicho, marehemu Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere.
Aidha, Rais Mstaafu, Bw. Jumbe alijiuzulu yeye na Waziri Kiongozi wake kutokana na kilichoitwa machafuko ya kisiasa Zanzibar.
Tangu Bw. Lowassa atangaze kujiuzulu kumekuwepo mjadala mkubwa juu ya kuendelea kuitwa Waziri Mkuu Mstaafu, au Waziri Mkuu wa zamani.
Bw. Lowassa ambaye ni Mbunge wa Monduli alijiuzulu kutokana na kashfa ya kampuni iliyopewa zabuni ya umeme wa dharura, Richmond.
Wakati huo huo, Simon Mhina anaripoti kwamba Mwenyekiti wa TLP, Bw. Augustine Mrema amemshauri aliyekuwa Waziri Mkuu, Bw. Edward Lowassa, aachane na CCM na atafute chama kingine.
Akizungumza na Nipashe ofisini wake jijini Dar es Salaam Mwanasiasa huyo alisema kama kweli Bw. Lowassa anasema kutoka moyoni mwake kwamba ameonewa na hahusiki na ufisadi, basi awatose CCM.
``Inaonekana kwamba Lowassa hakutaka kujiuzulu, kwa mujibu wa kauli zake ndani na nje ya bunge anaonyesha wazi kwamba amedhalilishwa ameonewa, inaonekana huyu bwana anayo agenda na siri nzito moyoni. Mimi sio Mungu sijui ukweli halisi, lakini atauthibitishia ulimwengu kwamba hana kosa, iwapo ataachana na chama kilichomsingizia,`` alisema Bw. Mrema.
Kiongozi huyo alikuwa anazungumzia hatua ya Bw. Lowassa kutangaza rasmi kwamba ameufunga majadala wa yeye kujiuzulu baada ya kuamua kuwajibika kutokana na kuhusishwa na kashfa ya Richmond.
Alisema kama kweli Lowassa akiwa Waziri mkuu wanchi anadhani kasingiziwa, basi nchi inayo matatizo makubwa.
Bw. Mrema alimuonya Bw. Lowassa asifikiri kwamba yaliyomfika yatawatoka wananchi vichwani na kusahau.
``Nimesikia watu wakisema huu sio mwisho wa Lowassa. Mimi nasema alichofanya hakitasahaulika, kwa hiyo njia ya kujisafisha sio kuzungumza mitaani achukue hatua ya kuonyesha kukerwa na kusingiziwa huko, yaani kuihama CCM, kama kweli anasingiziwa,`` alisema.
Alisema iwapo atakihama CCM atapata uwanja wa kutoboa siri zote za chuki zilizojengeka katika serikali.
``Lowassa ndani ya CCM ajihesabu amekwisha, amejizolea sifa mbaya sana, na bila kuchukua uamuzi wa kijasiri ataingia kaburini na lawama,`` alisema.
Alipoulizwa kwamba atakuwa tayari kumpokea Bw. Lowassa ndani ya TLP, Bw. Mrema alisema iwapo ataamua kujiunga atahojiwa kwanza.
``Akija kwetu tutamhoji kiundani, maana kupitia kwake tutafanikiwa kuwabaini mafisadi wengi zaidi, na kama atakuwa tayari kuwataja na mahali wanapoweka pesa zao, tutamsamehe, huu ndio mkakati wangu, hata nilipokuwa Waziri wa Mambo ya Ndani majambazi ambao walikuwa wanasalimu amri na kurejesha silaha, nilikuwa nawasamehe, halafu nawatumia kuwafichua wenzao waliojificha. Mtindo huu nataka kuutumia pia kwa Lowassa,`` alisema Bw. Mrema.
Alisema licha ya kwamba amelaumiwa vya kutosha, Bw. Lowassa anaweza kupunguza kwa kiasi kikubwa lawama hizo, iwapo atawasaidia watanzania kuwafichua mafisadi ndani ya serikali.
Alisema ni ukweli ulio wazi kwamba kuna mambo mengi yanayofanana na Richmond, ambayo bila shaka Bw. Lowassa anayafahamu na hawezi kulipua bomu akiwa bado ndani ya CCM.
SOURCE: NIPASHE