Posted Date::3/31/2008
CUF wadai Rais Kikwete anachezea amani ya Zanzibar
Muhibu Said, Dar na Salma Said, Zanzibar
Mwananchi
BAADHI ya wajumbe wa baraza la wawakilishi wa Chama cha Wananchi Zanzibar, wamedai kuwa Rais Jakaya Kikwete anachezea amani ya visiwani hapa.
Kauli hiyo, waliitoa jana kwa nyakati tofauti wakati wakitoa maoni yao kuhusiana na tamko la mwafaka wa kiasiasa lilitolewa katika Kikao cha Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya Chama Cha Mapinduzi (NEC) kilichomalizika juzi katika Kijiji cha Butiama mkoani Mara.
Mwakilishi wa Viti Maalum (CUF), Zakia Omar alisema hakuna dhamira ya kweli katika kuutatua mgogoro wa kisiasa visiwani Zanzibar kutokana na tamko hilo la CCM.
Alisema kuna maamuzi mengi tu ambayo serikali ya CCM imekuwa ikiyachukua bila hata ya kuwashirikisha wananchi, na inakuwaje hili la mwafaka, washirikishwe wananchi.
Maamuzi mengi yameamuliwa bila ya kutushirikisha sisi wananchi leo wanatwambia kupigwe kura ya maoni... mimi naona kama wana-'bytime' tu," alisema mwakilishi huyo.
Alitaja baadhi ya maamuzi yaliyowafikiwa bila ya kuwashirikisha wananchi kuwa ni kujiuzulu kwa aliyekuwa Rais wa Zanzibar, Aboud Jumbe Mwinyi bila ya kuchukuliwa maoni ya mtu yeyote.
Mwakilishi huyo, alisema kwa mujibu wa hati ya muungano, Rais wa Zanzibar, anakuwa Makamu Mwenyekiti wa CCM, lakini kufuatia mabadiliko ya 11 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano, wamepitisha vifungu na kumuondolea madaraka bila ya kuwapo kura ya maoni pamoja na maamuzi mengi yakiwemo yale ya kupeleka majeshi ya Tanzania katika vita vya Somalia na Comoro.
Kwa upande wake, Mansour Ali Yusuf, alisema inaonekana kana kwamba mbinu hiyo ya kutaka kupata kura ya maoni, ni mchakato wa kuhakikisha kwamba, watu wachache wateule wanaendelea kuiongoza Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) , wakisaidiwa na Serikali ya Muungano, iliyotumika ni mbinu ya kuwadanganya wananchi kuwa suala hilo ni gumu na haliwezi kupatiwa uamuzi wa haraka bila ya kuwepo kura ya maoni.
Naye Yussuf, alisema sio kweli kama Kikwete hawezi kutafuta suluhu isipokuwa anachofanya ni kuwalinda wahafidhina ambao kama watapata nafasi wangependa watawale milele.
Baadhi ya wananchi jana walikuwa katika mijadala mikali katika kila sehemu ambapo baadhi yao walisema sasa Rais Kikwete anataka kucheza na amani kwa kuwaachia viongozi wa Zanzibar kufanya maaamuzi ya kihuni.
Kilichoamuliwa Butiama, ni uhuni na sasa wanataka kutuchagulia nchi. Maana hatutakubali... wanataka yale yaliyotokea Kenya sasa yaje Zanzibar,? alisema mzee mmoja wa makamu katika Soko la Darajani.
Mapema wajumbe wote wa Baraza la Wawakilishi wa CUF, jana asubuhi, walitoka nje ya kikao cha Baraza hilo wakati kikiendelea, kuitikia wito wa chama hicho wa kuhudhuria kikao cha dharura.
Kabla ya kuchukua uamuzi huo, wajumbe hao awali waliingia ndani ya kikao cha Baraza la Wawakilishi kama kawaida na kusikiliza maswali na majibu, lakini kabla mchakato huo kumalizika, walianza kutoka nje mmoja baada ya mwingine.
Wajumbe hao walitoka nje wakati Waziri wa Maji, Ujenzi, Nishati ya Ardhi Mansour Yussuf Himid akiwasilisha muswada wa Sheria ya Kusajili Wahandisi, Wasanifu na Wakadiriaji Majengo.
Mnadhimu wa Baraza la Wawakilishi wa Kambi ya Upinzani, Soud Yussuf Mgeni aliwaongoza wajumbe wenzake kutoka nje ya kikao hicho, huku akisema wamelazimika kufanya hivyo, kutokana na unyeti wa jambo lenyewe ambalo linahusisha amani katika nchi.
Mgeni alithibitisha wajumbe hao kuondoka barazani na kwamba, walikwenda Makao Makuu ya chama hicho Mtendeni kwa kikao cha dharura ambacho pamoja na mambo mengine kitajadili kilichojitokeza Butiama.
Tumetoka kwenye Baraza tunakwenda kwenye kikao muhimu tulichoitwa na chama chetu, sisi tunawawakilisha wananchi, kwa hiyo, lazima la leo lifanywe leo hakuna kusubiri, alisema.
Mnadhimu huyo, alisema wamechukua uamuzi wa kutoka nje ya kikao cha baraza bila ya kumuarifu Spika , lakini taarifa zaidi atazipata atakapoangalia upande wanaokaa wawakilishi wa Kambi ya Upinzani.
Spika hatujamuarifu rasmi, lakini bila ya shaka atafahamu tu baadaye kwa sababu akitupa jicho ataona hakuna mtu upande wetu kwa hivyo?atajua...atajua tu,? alisema Mgeni haraka haraka huku akiingia ndani ya gari dogo na kwenda Mtendeni.
Spika wa Baraza hilo, Pandu Ameir Kificho alisema hajapokea taarifa zozote kuhusiana na wajumbe wa kambi ya upinzani kuondoka ghafla katika kikao hicho.
Sina taarifa ya kuondoka kwao, ingawa niliwaona wakiingia na baadaye kutoka wote, sina tafsiri juu ya kitendo hicho..., alisema Spika.
Hata hivyo, baada ya kuwasilishwa muswada wa Waziri Himid, Mwenyekiti wa Kamati, aliwataka CUF kuwasilisha maoni ya kambi yao kana kwamba hajaona upande wake wa kushoto kama kulikuwa hakuna mtu, jambo lililozua vicheko kwa wajumbe walioketi upande wa kulia ambao ni wa CCM.
Mheshimiwa njoo uwasilishe maoni ya kambi ya upinzani, aliwachekesha wajumbe wa CCM.
Wakati huo huo; Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Chama cha Wananchi (CUF), imewaita wabunge na wawakilishi wake, katika kikao cha dharura kitakachofanyika leo jijini Dar es Salaam kujadili tamko hilo la CCM.
Mbali na kikao hicho, CUF pia inatarajia kutoa tamko lake rasmi leo asubuhi kueleza msimamo wake kuhusu tamko hilo la NEC ya CCM.
NEC katika tamko lake lililosomwa na Makamu Mwenyekiti wa CCM Taifa, Pius Msekwa kwa wajumbe wa halmashauri hiyo na waandishi wa habari baada ya kumalizika kwa kikao chake cha siku mbili kijijini Butiama mkoani Mara juzi usiku, ilisema imeyakubali mapendekezo yaliyomo katika taarifa ya mazungumzo ya mwafaka.
Hata hivyo, ikasema imeazimia kuwa ikiwa makubaliano hayo yatakubaliwa, yataleta mabadiliko makubwa katika mfumo wa utawala wa Zanzibar na kwamba, kwa kuliangalia jambo hilo, ni lazima wananchi wote wa Zanzibar watapaswa kuliamua kwa njia ya kura ya maoni.
Kutokana na hali hiyo, NEC ilisema imeiagiza Kamati ya Mwafaka ya CCM kurejea tena katika mazungumzo na wenzao wa CUF ili kuliamua jambo hilo.
Kutokana na hali hiyo, Katibu wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya CUF Taifa, Said Miraji aliliambia gazeti hili jijini Dar es Salaam jana kuwa, wamelazimika kuitisha kikao cha dharura kati ya kamati yake na wabunge na wawakilishi wote wa chama hicho.
Miraji ambaye pia ni Mkurugenzi wa Blue Gurad Taifa, alisema kikao hicho, kitafanyika leo Makao Makuu ya chama hicho, Buguruni, jijini saa 11:00 jioni na ajenda kuu itahusu kujadili tamko hilo la kikao cha NEC na hatua ambazo wabunge na wawakilishi wataona kuwa zinafaa kuchukua kuhusiana nalo.
"Hapo hakuna jambo la kuficha, kila kitu sasa ni wazi," alisema Miraji.
Kabla ya kikao hicho, Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Shariff Hamad, atakutana na waandishi wa habari Makao Makuu ya chama hicho, leo asubuhi.
Mkurugenzi wa Haki za Binadamu na Mahusiano na Umma wa CUF Zanzibar, Salim Bimani, aliliambia gazeti hili jana kuwa, katika mkutano huo, Maalim Seif ambaye atakuwa na Makamu Mwenyekiti wake, Machano Khamis Machano, anatarajiwa kutoa kutoa tamko kuhusu msimamo wa chama hicho kuhusiana na la NEC CCM kuhusu mwafaka.
"Kubwa litakalozungumzwa na Katibu Mkuu, ni kutoa tamko kuhusu msimamo wa chama kama alivyoahidi katika mkutano hadhara katika Uwanja wa Garagara, Mtoni Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja juzi kuhusu tamko la NEC Butiama," alisisitiza Bimani.