CUF waja juu
2008-05-20 16:32:06
Na Sharon Sauwa, Mikocheni
Baada ya Rais wa Zanzibar Bwana Amani Karume kutoa masharti ya kukutana na hasimu wake, Maalim Seif Sharif Hamad, chama cha CUF kimekuja juu kikidai kwamba kauli za kiongozi huyo ni kejeli tupu na kwamba piga ua galagaza, hakitamtambua kama rais halali wa visiwa hivyo.
Naibu Mkurugenzi wa Mawasiliano na Habari wa chama hicho,
Bw. Salum Bimani, ameliambia Alasiri leo asubuhi kuwa, kauli ya Rais Karume kutaka CUF wamtambue kwanza ndiyo akae nao kuzungumzia mgogoro wa kisiasa unaokikabili kisiwa hicho, inaonyesha hana nia ya kumaliza mgogoro huo.
Mwanasiasa huyo amedai kuwa wanao ushahidi ambao unaonyesha Bw. Karume hakushinda katika uchaguzi wa mwaka 2000 na ule wa 2005 na hivyo hata siku moja hawatamtambua kama ni rais.
``Kauli zake hizo ni za kejeli, si za kujenga na hata siku moja hatutamtambua kuwa ni rais kwa sababu vigezo vya kufanya hivyo tunavyo...mwaka 2000 hakushinda wala 2005 hakushinda pia,`` akasema Bw. Bimani.
``Salmin (Rais Mstaafu wa Zanzibar), naye alileta kibri na sasa yuko huko nje, anasikika wapi sasa hivi?, muache huyo Karume naye amalize kipindi chake, historia ndiyo itakayomhukumu,`` akasema Bw. Bimani.
Amesema itafika wakati Zanzibar itakuja kupata rais ambaye atawaunganisha Wapemba na Waunguja na kuwa kitu kimoja.
Ameongeza kuwa wao hawana tatizo la kukutana na
rais Karume lakini si kwa masharti aliyoweka yeye.
Jana rais Karume alisema atakuwa tayari kukutana na Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad, kuzungumzia mpasuko wa kisiasa Zanzibar kwa sharti la kumtambua kuwa yeye ni rais halali wa visiwa hivyo.
Alisema kimsingi yeye amekuwa mstari wa mbele kukaribisha maelewano ili kuendeleza umoja wa kitaifa na ndio maana CCM ikaingia katika mazungumzo ya kutafuta muafaka wa kuondoa tatizo hilo.
Alisema iwapo chama hicho kitatangaza rasmi hadharani kumtambua kama rais halali wa Zanzibar yeye hana tatizo la kukutana nao kuzungumza.
* SOURCE:
Alasiri