Wazanzibari wazidi kuwaka
Na Salma Said, Zanzibar
," alisema ALIYEKUWA Katibu Mkuu wa kwanza wa Baraza la Mapinduzi, Mzee Salim Rashid, amesema kauli ya Naibu Waziri Kiongozi, Ali Juma Shamhuna, kwamba Zanzibar ni nchi ni msimamo wa Wazanzibari wote.
Akizungumza na gazeti hili katika mahojiano maalumu nyumbani kwake Mtaa wa Vuga, Mkoa wa Mjini Magharibi, Mzee Rashid alisema, yaliyosemwa na wawakilishi na Shamhuna sio maneno yao binafsi, bali ni msimamo wa Wazanzibari kwa ujumla wao.
�Hili sio suala la Shamhuna au Serikali, ni suala la Wazanzibari wote na wawakilishi wanaosemea hilo kwenye Baraza la Wawakilishi wanawakilisha maoni ya wananchi, kwa hiyo Shamhuna hakukosea wala sio maneno yake ni maneno ya Wazanzibari wote,� alisema Mzee Rashid ambaye ana uzoefu mkubwa wa uongozi katika siasa za Tanzania.
Alisema, ipo haja ya mjadala huo kuachwa ukazungumzwa kwa upana wake badala ya kuamuliwa kwa mabavu kama ilivyofanywa awali na kuleta athari kubwa katika siasa za Tanzania.
Mzee aliwaonya wanaojaribu kuzima mjadala huo kufahamu kwamba, suala hilo ni zito na haliwezi kumalizwa kwa wepesi kwa kuwa hivi sasa, Wazanzibari wanalizungumzia na wana hamu ya kutaka kusikia kauli nzito inayotoka kwa viongozi wakuu juu ya ufumbuzi wake.
Kuhusu suala hilo kutolewa uamuzi na Chama Cha Mapinduzi (CCM), Mzee Rashid alisema si sahihi kwa kuwa maamuzi yatakuwa ni ya CCM na si ya kikatiba. Alimsifu Waziri Mkuu Mizengo Pinda kwa kuibua suala hilo sasa ambapo Wazanzibari wana hamu ya kuunganishwa.
�Jambo hili ni historia kubwa. Pinda kaondoa fitina kwani kwa zaidi ya miaka 50 Wazanzibari walikuwa wanahitaji kuunganishwa isiwezekane, lakini hili sasa limewaunganisha, Alhamdulilah,� alishukuru Mzee huyo.
Alisema Muungano si suala la CCM peke yao, bali wananchi wote wa Tanganyika na Zanzibar, hivyo suala hilo haliwezi kupatiwa ufumbuzi kwa kutumia Katiba ya Muungano kwa sababu lilitengenezwa katika maamuzi ya kisiasa.
Kwa mujibu wa Mzee Rashid kinachoweza kutumika kulipatia ufumbuzi suala hilo ni Hati ya Makubaliano ya Muungano badala ya Katiba ya Muungano.
Alishauri kwamba, endapo kuna haja ya kutumia sheria na Katiba katika kulitafutia ufumbuzi suala hilo, mahala panapopaswa kupelekwa suala hilo ni katika Mahakama ya Kimataifa ya Haki (International Court Of Justice, The Hague) kwa sababu zilizoungana zilikuwa nchi mbili hivyo ni suala la kimataifa.
Akizungumzia maoni ya hivi karibuni yaliyotolewa na mwanasiasa mwenzake, Peter Kisumo, kuhusu Zanzibar, alisema Kisumo ameonyesha dharau kwa Zanzibar, kwani hakupaswa kulinganisha timu ya mpira na Zanzibar ambayo ni nchi.
�Ni dharau kubwa sana ameonyesha Kisumo kwa nchi yetu na pia amemdhalilisha hata Rais Karume, huwezi kufananisha timu ya mpira na Zanzibar, wala huwezi kufananisha wimbo wa taifa na kwaya. Si vizuri kabisa, amekosea na ni maneno ya ... si
maneno ya akiliMzee Rashid na akaongeza:
"Mimi Kisumo ni rafiki yangu kipenzi namualika awe mgeni wangu
aje Zanzibar kusikiliza maoni ya Wazanzibari juu ya suala hili linavyoendelea, hapo ndio atajua kinachoendelea hapa visiwani."
Alisema kauli ya Kisumo imetolewa kana kwamba anahutubia mkutano wa TANU Biharamulo, kwamba kinachosemwa hicho ndicho kinachotendeka, lakini wakati huu ni mwingine na mfumo wa vyama vingi ndio unaochukua nafasi ya demokrasia.
�Wapo wanaojisahau wakadhani bado kuna chama kimoja, Kisumo hana uzoefu wala ujuzi wa kuzungumzia mambo ya kimataifa au kitaifa ... maneno yake ni kama anahutubia mkutano wa TANU chini ya mfumo wa chama kimoja,� alisema na akaongeza:
�Mimi siamini kama mjadala huu unaweza kumalizwa kwa CCM kutoa tamko au kukataza viongozi wasizungumze, hapana babu, huu mjadala uendelee, wao wanadhani chama kikisema Zanzibar si nchi ndio mambo yatakwisha?�
Akizungumzia kauli ya Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Dk Asha-Rose Migiro, mwanasiasa huyo mkongwe alisema hana mamlaka yoyote ya Umoja huo, hivyo kauli yake haina uzito unaostahili, kwani alipaswa kuutaka mjadala huu uendelee na si kunyamazishwa na kukumbusha kwamba, Umoja wa Mataifa haujafuta kiti cha Zanzibar, kwani hakuna maombi ya Zanzibar wala Tanzania juu ya kufutwa kwa kiti hicho.
Alishauri kuitishwa kura za maoni kuhusu suala hilo na kwamba hata kama watakaoulizwa na wanaCCM wawe Wazanzibari na Wabara ili kupata uwiano wa maoni kabla ya kuamua kulipeleka suala hilo Mahakama ya Kimataifa ikitokea kura zinawiana.
Mzee Salim Rashid, ambaye amepata misukosuko kadhaa kwa kutetea masilahi ya Zanzibar, alikuwa ni Katibu wa kwanza wa Baraza la Mapinduzi baada ya Zanzibar kupata uhuru, aliwahi pia kuwa Naibu Waziri wa Fedha katika Serikali ya Muungano, balozi wa nchi mbalimbali ambaye hadi kustaafu kwake mwaka 1972 alikuwa Balozi wa Tanzania nchini Ethiopia