Hati ya Muungano ilivyokuwa inavurugwa tangu 1964
Na Nizar K Visram
Wakati Tanganyika ilipopata Uhuru mwaka 1961 uwezo wa kutawala uligawanywa baina ya Gavana Jenerali na Waziri Mkuu. Hiyo ndiyo katiba ya Uhuru tuliorithi kutoka kwa wakoloni. Mfumo huo uligeuka na kuwa Jamhuru mnamo 1962. Tukapitisha katiba mpya ambayo ilimpa Rais uwezo wote aliokuwa nayo Gavana na Waziri Mkuu.
Chini ya katiba hiyo Rais akawa mkuu wa nchi, mkuu wa serikali, jamadari mkuu wa majeshi na akawa na uwezo wa kuzuia sheria yoyote inayopitishwa na bunge kwa kukataa kuisaini. Rais akapewa uwezo wa kuteua makamo wake na mawazi. Akapewa uwezo wa kuongoza baraza la mawaziri ambao waliwajibika kwake.
Katika katiba ya Uhuru mawaziri walikuwa wanawajibika kwa bunge. Katiba ya Jamhuri ukaondoa uwezo huo wa Bunge na mawaziri wakawa wanawajibika kwa Rais. Bunge likapokonywa meno na likawa kibogoyo, kwa vile likawa halina uwezo wa kusimamia serikali. Kwa kweli Rais akawa na uwezo hata wa kulivunja bunge na kuitisha uchaguzi mpya.
Tanganyika ilirithi Bunge lenye wajumbe 71 waliochaguliwa, wote kutoka chama cha TANU, na kumi walioteuliwa. Katika kutunga katiba ya jamhuri, kilichofanyika ni kuwa bunge likajipa uwezo wa kujibadili na kuwa baraza la kutunga katiba (constituent assembly). Ni baraza hili ndilo lililopitisha katiba ya jamhuri
Ni katika mazingira haya ndipo Hati ya Muungano (Articles of Union) ikasainiwa baina ya Jamhuri ya Wananchi wa Zanzibar na Jamhuri ya Tanganyika. Hati hiyo ilisainiwa na Rais Mwalimu Nyerere kwa niaba ya Tanganyika na Rais Sheikh Karume kwa niaba ya Zanzibar. Na ndipo ikazaliwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Tuliambiwa kuwa kuundwa kwa muungano huo ni matokeo ya karne nyingi ya mahusiano ya kihistoria baina ya wananchi wa bara na visiwani.
Pamoja na hayo ukweli ni kuwa Hati ilisainiwa bila ya mjadala miongoni mwa wananchi na hata miongoni mwa wanachama wa chama tawala. Ni matokeo ya maamuzi ya viongozi yaliyowashitukiza wananchi. Hata chama cha Umma Party kilichoshirikiana na chama cha Afro-Shirazi katika kuleta Mapinduzi na kuendesha serikali, hakikushauriwa kabla ya kusainiwa Hati.
Labda ni kutokana na hulka ya muungno wenyewe. Licha ya hiyo sababu ya mahusiano ya kihistoria, kuna sababu zingine ambazo zimekuwa zikijitokeza hivi karibuni. Haya yameanza kueleweka zaidi baada ya tafiti kufanyika na baada ya kufichuliwa kwa nyaraka za siri za watawala wa Marekani. Nyaraka hizi zinazungumzia kuundwa kwa Muungano kutokana na vita baridi baina ya Marekani na kambi ya Kisoshalisti iliyoongozwa na Muungano wa Kisovieti (USSR)
Kenya, Uganda na Tanganyika zilipata uhuru wake wa kisiasa kwa kupitia mazungumzo na wakoloni. Hakujakuwa na mapigano au vurugu, kinyume cha Zanzibar ambako mapinduzi yaliashiria kushika hatamu kwa viongozi wa mrengo wa kushoto kama akina Abdulrahman Babu wa Umma Party na wenzake wa Afro-Shirazi Party.
Marekani na Uingereza zilipata mshituko mkubwa kuhusu mapinduzi haya ya kimaendeleo. Mara moja ujumbe ulitumwa kutoa kwa waziri wa mambo ya nje wa Marekani mjini Washinton, Dean Rusk, kwenda kwa mabalozi wake mjini Nairobi, Kampala na Dar es Salaam. Mabalozi hao waliagizwa wazungumze na Marais Kenyatta, Obote na Nyerere ili wamuelimishe Sheikh Karume kuhusu hatari anayokabiliwa katika ushirikiano wake na Umma Party
Haya yanathibitishwa na Amrit Wilson ambaye ni mwandishi wa kitabu cha US Foreign Policy: The Creation of Tanzania (sera ya mambo ya nje ya Marekani na kuundwa kwa Muungano wa Tanzania). Yeye alimhoji aliyekuwa balozi mdogo wa Marekani huko Zanzibar wakati wa mapinduzi, Bw Franc Carlucci ambaye alikubali kuwa serikali yake ilimshawishi Mwalimu Nyerere kuhusu kuundwa kwa Muungano. Carlucci baadaye akaja kuwa mkuu wa shirika la kijasusi la CIA.
Naye mwandishi Susan Crouch, katika kitabu chake kiitwacho Western Response to Tanzanian Socialism 1967-1983 (nchi za magharibi zilivyopambana na Ujamaa wa Tanzania) anaeleza jinsi CIA ilivyofanya juu chini ili kuunda mazingira ya Muungano kwa kuchochea wasiwasi miongoni mwa viongozi wa Afrika Mashariki kuwa Zanzibar ilikuwa inamezwa na ukomunisti.
Ni wasiwasi huu ndio uliowaingia viongozi wa Tanzania wakati ule, wasiwasi dhidi ya Umma Party. Lakini pia Karume alikuwa na tatizo ndani ya ASP yenywe. Baada ya kushindwa kwa mara nyingine kuunda serikali kufuatia uchaguzi mwengine wa Julai 1963, viongozi wenzake walianza kumkosoa na kukosa imani naye.
Hawa ni akina Othman Shariff waliotaka kuchukua nafasi yake. Pia kulikuweko na akina Abdallah Kassim Hanga, Abdulaziz Ali Twala na Hassan Nassor Moyo ambao walielekea kushirikiana na Umma Party ikiongozwa na akina Babu, Ali Sultan, Ali Mahfoudh, Salim Rashid na Badawi Qullatein. Karume kwa hiyo alipokabiliwa na ushauri wa kuunda Muungano alikubali mara moja. Hamu yake iliongezeka hasa baada ya motisha alizopewa na CIA kama ilivyoelezwa katika nyaraka zake.
Ndipo Hati ya Muungano ilipotiwa saini na marais Nyerere na Karume. Hati hiyo ikaorodhesha mambo kumi na moja ambayo ni ya muungano. Muundo wa serikali ukawa na makamo wa rais wawili, mmoja kutoka bara na mwingine kutoka Zanzibar ambaye ndiye Rais wa Zanzibar.
Baada ya kutiwa saini Hati hiyo ilitakiwa iridhiwe na bunge la Tanganyika na Baraza la Mapinduzi la Zanzibar.Inasemekana huko Zanzibar jambo hili halikufanyika. Hii inathibitishwa na watu kadha waliokuwa na madaraka wakati ule. Wa kwanza ni Bw Salim Said Rashid aliyekuwa katibu wa kwanza wa Baraza la Mapinduzi.
Pia Mwanasheria Mkuu wa mwanzo baada ya Mapinduzi, Bw Wolfgng Dourado, naye anathibitisha kuwa Hati haikuridhiwa na Baraza. Mwengine ni Abubakar Khamis Bakary aliyewahi kuwa Mwanasheria Mkuu na waziri wa sheria na katiba. Yeye alipitia vitabu vyote vya sheria na kumbukumbu kuanzia 1964 na hakuona popote Hati hiyo kuridhiwa na Baraza la Mapinduzi.
Kwa hiyo baada ya Hati kusainiwa na marais wawili ikaridhiwa na bunge la Tanganyika lenye wabunge kutoka TANU. Kisha katiba ya Tanganyika ikarekebishwa na ikawa katiba ya muda ya Muungano iliyopitishwa na bunge la TANU. Katiba mpya ikapitishwa kama vile ni katiba ya zamani inarekebishwa tu.
Katiba ya kudumu ilitakiwa ipitishwe baada ya kuundwa kwa baraza la katiba (constituent assembly). Ilitakiwa ipitishwe katika muda wa mwaka mmoja lakini ilichukua hadi 1977. Na hilo baraza la katiba ambalo kwa kawaida huwa linashirikisha jamii nzima halikuundwa.
Tunachosema hapa ni kuwa hakukuwa na mjadala wa kitaifa wakati wa kutia saini Hati ya Muungano, wakati wa kupitisha Katiba ya Muungano ya mpito na hata pale Katiba ya kudumu ilipopitiswa. Hakukuwa na mijadala ya kitaifa na kakukuwa na baraza la katiba.
Katiba ya muda nayo ilifanyiwa marekebisho kadha.Moja ni kuhusu kuongezwa kwa mambo ya muungano, yaani kupunguza mamlaka ya serikali ya Zanzibar. Hii ni kinyume cha Hati ya Muungano. Rekebisho lingine la 1975 ni kupunguza mamlaka ya Bunge na kuongezea mamlaka Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya TANU.
Matokeo yake ni kuwa chama (NEC) ndicho chenye mamlaka kamili katika mambo yote ya kisiasa na kitaifa. Kilichokuwa kikifanyika kabla sasa kikapewa nguvu ya kikatiba, kwani kabla ya hapo chama tayari kilikuwa kinatawala katiba. Kwa mfano Azimio la Arusha utekelezaji wake ulipitishwa na NEC na kuridhiwa na bunge. Kwa hiyo chama kikawa na uwezo wa kutawala dola moja kwa moja bila kupitia bunge.
Chama kikazidi kupata nguvu baada ya kifo cha Rais wa Zanzibar, Mzee Karume na nafasi yake iliposhikwa na Aboud Jumbe. Yeye huyu alirahisisha njia ya kuunganisha vyama vya TANU na ASP na kuundwa kwa CCM mnamo 1977. Kamati ya kuunda katiba mpya ya chama ni hiyo hiyo iliyopewa kazi ya kupendekeza katiba ya Muungano.
Ikawasilisha muswada wa katiba ya Muungano kwa NEC ambayo ilikaa katika kikao cha siri cha siku moja. Baada ya hapo mswada huo ukapelekwa katika Bunge likikaa kama Baraza la Katiba. Bunge lilipitisha katiba baada ya kukaa kwa muda wa saa tatu na wabunge saba kuchangia. Kabla ya hapo Waziri Mkuu aliwakumbusha wabunge kuwa uwezo wao ni mdogo kwa vile mswada huo ulipitishwa na chama ambacho ndicho kinachoshika hatamu.
Hivi ndivyo ilivyopitishwa katiba ya kudumu ya 1977, bila ya mjadala au mashauriano ya kitaifa kama ilivyotakiwa na Hati ya Muungano. Kwa mujibu wa Hati hiyo NEC haikuwa na mamlaka ya kupitisha katiba.
Mnamo January 1982 NEC ilipendekeza mabadiliko ya katiba ambayo kwa mara ya kwanza yaliwasilishwa kwa wananchi wayajadili kwa muda wa mwaka mmoja. Wananchi walitekeleza wajibu na haki yao hiyo kwa bidii zote. Mapendekezo ya wengi yalikuwa ni kupunguzwa kwa mamlaka ya Rais na kuongezwa kwa mamlaka ya Bunge. Ikapendekezwa kuwa katiba iwe na kifungu cha haki za kimsingi (bill of rights).
Huko Zanzibar watu wakadai uhuru zaidi katika kujiamulia mambo yao pamoja na kupitia upya Hati ya Muungano. Mjadala ukapamba moto. Baada ya miezi minane mjadala ukafungwa ghafla na NEC ikatangaza kuwa hali ya hewa ya kisiasa imechafuka Ilisemekana Rais Jumbe alitiwa hanjam mpaka akalazimishwa kujiuzulu. Yeye na Waziri Kiongozi wake walishutumiwa kuwa ndio waliochafua hali hiyo huko visiwani
Kilichofanyika ni kuwa Jumbe alitayarisha waraka aliokusudia kuuwasilisha kwa Rais Nyerere akiomba kuitishwa kwa mahakama maalum ya katiba ili kungalia iwapo katiba iliyopo ilikiuka Hati ya Muungano. Kabla ya waraka huo kuwasilishwa ulipotea na ukaibuka kwenye meza ya Mwalimu ambaye aliifikisha katika kikao cha NEC ili ijadiliwe.
Inasemekana katika mdalala mkali uliofuata, mmoja kati ya wapinzani wakali wa Rais Jumbe alikuwa Maalim Seif Sharif Hamad pamoja na washiriki wenzake. Jumbe akajiuzulu na Ali Hassan Mwinyi akateuliwa na NEC kugombea urais wa Zanzibar. Maalim Seif akateuliwa kuwa Waziri Kiongozi
Nini hasa kilichochafua hali ya hewa? Katiba ilitakiwa iongoze mgao wa madaraka baina ya serikali ya Zanzibar na ya Muungano. Katiba hiyo nayo ilitakiwa iwe inaongozwa na Hati. Hii haikufanyika hasa pale mambo ya ndani ya Zanzibar yalipopunguzwa na mambo ya Muungano yalipoongezwa. Ndani ya Zanzibar jambo hili lilipingwa hata miongoni mwa viongozi. Kupitishwa kwa katiba ya Muungano ya 1977 na kuvunjwa kwa ASP na nafasi yake kuchukuliwa na CCM huko visiwani, kulisaidia katika kufunika upinzani huu mpaka pale mjadala ulipofunguliwa na NEC. Chini ya Sheikh Karume kuvunjwa kwa ASP ilibaki kuwa ndoto ya wale waliotaka kuimarisha Muungano.
Jumbe alisaidia kuvunjwa kwa ASP na kuundwa kwa CCM, chama ambacho mwishowe kilimvua madaraka. Haya yasingetokea kama kila upande ungelikuwa na chama chake kama ilivyokuwa hapo awali. Baada ya hapo uongozi mpya wa Zanzibar haukudiriki tena kuzungumzia masuala haya. Kilichobaki sasa ni kuzungumzia kero tu baina ya Waziri Mkuu na Waziri Kiongozi.
Mwaka 1992 katiba ikabadilishwa tena ili kuanzisha mfumo wa vyama vingi. Wakati huo huo kulifanyika mabadiliko ya kimsingi, kinyume cha Hati ya Muungano. Hati ilisema kuwa iwapo rais anatoka bara basi Rais wa Zanzibar atakuwa makamo wake. Badala yake makamo wa rais sasa akawa ni mgombea mwenza.
Suala likaibuka kuhusu wadhifa na nafasi ya Rais wa Zanzibar katika Muungano. Kilichofanyika ni kumfanya Rais huyo awe sehemu ya baraza la mawaziri la Muungano. Rais wa Zanzibar anatokana na katiba ya Zanzibar na siyo ya Muungano. Kwa hivyo kwa yeye kukaa katika kebineti ya Muungano ni kitu kisichoeleweka.
Matatizo ya katiba ya Muungano yamejitokeza katika sura kadha. Kwa mfano pale Zanzibar ilipojiunga na jumuiya kimataifa ya kiislamu (OIC) kulizuka mtafaruki mkubwa baina ya uongozi wa bara na Zanzibar.
Halafu tena mnamo 1993 kikaja kikundi cha wabunge wa CCM waliojiita G55 ambao walidai mfumo wa serikali tatu. Mwalimu aliingilia kati na kuwakemea G55 akiwaambia hawangeweza kutetea sera hiyo wakati wakiwa ndani ya CCM. Kutetea serikali tatu ni kwenda kinyume cha Hati ya Muungano na kwa hiyo ni kosa la usaliti. Hakuna aliyeuliza mbona Hati yenyewe imekuwa ikichezewa na watawala tangu 1964? Kwa mara nyingine suala la serikali ya Tanganyika likazimwa na halikusikika tena mpaka hivi karibuni.
Baada ya kufariki kwa Mwalimu suala hilo likajitokeza kwa nguvu zaidi. Mfano mmoja ni ile kesi iliyofunguliwa mnamo 2003 na Wazanzibari kumi wakidai kuwa Muungano ulikuwa batili. Wamtaka Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar awasilishe Hati ya Muungano. Aliiambia mahakama kuwa hajawahi kuiona! Ikasemekana kuwa haipo.
Kesi hiyo imefifia lakini suala la Hati ya Muungano litaibuka tena. Kule Uingereza wamekuwa na Muungano kwa karne kadha lakini mahakama ya huko mnamo 1953 ilitoa amri kuwa bunge la Uingereza halikuwa na uwezo wa kuvuruga hati ya muungano (Act of Union) baina ya England na Scotland kwa vile hati hiyo iko juu (supreme) ya vyombo vyote vya utawala.
Nasi tunahitaji mahakama inayothubutu kusema hivyo kuhusu Hati yetu ya Muungano wa
Tanzania.nizarvisram@ctvsatcom.ne. Kwa makala zaidi na picha, tembelea;
http://mjengwa.blogspot.com