Na Asha Bani
PROFESA Mwesiga Baregu, ni mwanasiasa na mchumi mwenye shahada mbalimbali za elimu ya juu nchini na nchi za nje, ambaye amejitoa mhanga katika kugombea ubunge wa Afrika Mashariki.
Profesa Baregu, ni mgombea wa nafasi hiyo kwa tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), ambacho kilimpitisha kutokana na kumuona anafaa na kwamba hakuna mgombea katika vyama vingine vya sisa ambaye anafanana au kuwa na elimu na umaarufu kama alionao Profesa Baregu katika masuala ya siasa na uchumi.
Hata hivyo kuna sababu ya kuhoji kwa nini Profesa Baregu agombee ubunge wa Afrika Mashariki? Katika mahojiano yake na Tanzania Daima, Profesa Baregu anabainisha kuwa ana sababu nyingi zilizomfanya agombee nafasi hii na akishinda atahakikisha Tanzania inangara na kupeperusha bendera katika Afrika Mashariki.
Sifa nilizonazo katika elimu, katika uwezo wa kufahamu jambo na kulitatua, nina uhakika hakuna mgombea katika chama chochote ambaye anasifa kama hii, hivyo nina uwezo wa kuongoza, alisema Profesa Baregu.
Anasema mbali na kuwa na elimu, atahakikisha anakuwa na nguvu katika muungano huo na kuiwezesha Tanzania kuwika katika medani ya uchumi na biashara, ambapo uchumi wa Tanzania utapanda na kutambulika kuliko ilivyokuwa hivi sasa, ukilinganisha na nchi za Afrika Mashariki.
Ikiwa tulifanikiwa na kuupa nguvu muungano wa Tanganyika na Zanzibar hadi ulipo hapa sasa na kuitwa Tanzania, na hadi leo unaendelea kuwapo ingawa kuna migogoro ya hapa na pale, lakini Mwalimu Nyerere alijitahidi kuuimarisha na viongozi wetu wanajitahidi kuuimarisha ili usije kuvunjika, ndivyo itakavyokuwa EAC, alisema.
Anasema atahakikisha muungano hautaweza kuvunjika tena kama ilivyotokea awali, mwaka 1977, ambapo muungano huo ulidumu kwa muda wa miaka 10 tangu kuanzishwa.
Kuvunjika kwa Muungano wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Tanzania tayari tumejifunza mengi na vya kutosha, na kama kulikuwa na udhaifu au upungufu katika nchi yetu kwa sasa, nitakuwa katika mstari wa mbele kukabili na kuyasawazisha matatizo hayo ili umoja huo usiweze kuvunjika tena, na kinachotakiwa ni kuwa imara kwa umoja huo, alisema Baregu.
Tunaweza kuwa viongozi wa EAC endapo tukijiamini na kuacha kuwa wafuasi, na mimi ni mtaalamu pekee wa kusuluhisha migogoro na ninawahakikishia Tanzania itakuwa makao makuu ya usuluhishi, kwa kuwa ni nchi ya amani na yenye utulivu, anasema Baregu.
Baregu anasema atakuwa kama silaha na chachu ya kuleta maendeleo katika jumuiya hiyo, kwa kuwa anapenda kupata mawazo ya watu kutoka sehemu mbalimbali ili kufanikisha malengo yake aliyojiwekea katika kuimarisha umoja huo.
Baregu anasema kugombea nafasi hiyo ni sawa na kujitoa mhanga, kwa kuwa Bunge la Chama Cha Mapinduzi (CCM) limepitisha wagombea 24.
Katika wagombea 24, kambi ya upinzani kupitia CHADEMA kuna mgombea mmoja ambaye ni yeye Baregu, na Chama cha United Democratic (UDP), kinawakilishwa na Fortunatus Masha.
Uchaguzi huo unatarajiwa kufanyika Novemba 2, ndani ya Bunge ili kumpata mwakilishi wa Bunge la Afrika Mashariki.
Profesa Baregu anasema endapo akichaguliwa katika nafasi hiyo atahakikisha anafanya maajabu, kwa kuhakikisha anaunganisha Tanzania, Kenya na Uganda kuwa kitu kimoja katika masuala mbalimbali yakiwamo ya kijamii na kiuchumi.
Profesa Baregu alizaliwa Februari 23, mwaka 1944, katika Kijiji cha Maruku, mkoani Kagera, ameoa na hadi sasa ana watoto saba.
Ana shahada mbalimbali alizozipata katika vyuo vya hapa nchini na nje ya nchi, hasa shahada za uchumi na mambo ya siasa.
Mwaka 1964 alipata elimu ya juu katika Chuo cha Makerere nchini Uganda, ambapo alisoma na kupata Shahada ya Ukutubi. Anasema chuo hicho ni maarufu zaidi kwa kutoa viongozi hapa nchini kama Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.
Mwaka 1998-2002, alisoma katika Chuo cha Senior Reseach Fellow - Afrika Kusini, na kozi kama hiyo pia aliisoma akiwa nchini Zimbabwe.
Kuanzia mwaka 1988 hadi 1994, alikuwa profesa katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam katika masuala ya Sayansi ya Siasa. Mwaka 1982 -1988, alikuwa Senior Lecturer in Political Science katika chuo kikuu hicho hicho cha Dar es Salaam.
Mwaka 1992-1994, alikuwa member Committee of vice-Chancellors and Principal, wa Tanzania.
Mwaka huo huo alikuwa mhariri katika kitengo cha mambo ya Sayansi ya Siasa katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
Mwaka 1989-1991, alikuwa mratibu nchini Afrika Kusini, na alikuwa msuluhishi katika migogoro ya kisiasa nchini humo.
Mwaka 1989-1991, alikuwa mratibu katika uchunguzi wa masuala ya miradi katika Idara ya Sayansi na Siasa nchini Namibia. Aidha, anasema kuwa mratibu wa mambo ya siasa na katika kamati ya kusuluhisha
migogoro mara kwa mara katika Afrika, kumemfanya awe mzoefu wa kufanya maamuzi katika mchakato wa mtandao wa siasa.
Mwaka 1988 -1991, alikuwa Mhariri Mkuu wa jarida la The Dar Graduate, ambalo lilikuwa linaandaliwa na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, kwa wakati huo na ni mtunzi mzuri wa vitabu mbalimbali vinavyoelezea masuala ya siasa na uchumi.
Aliwahi kuwa na nyadhifa mbalimbali katika chuo kikuu na ni mtu ambaye walikuwa wanamthamini sana hasa kwa kazi zake katika chuo hicho na chuo chochote, na ndivyo ilivyo hadi sasa mchango wake kwa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ni mkubwa.