hawa hasa ndio serikali ya mapinduzi wanavyoendesha nchi, wameondoa ubaguzi wa mwarab na kuleta usawa.
ona jinsi walivyowaadilifu, sasa kama uliwahi kuwapo zanzibar hutoshangaa nini kinaendelea.
MAPINDUZI DAIMA
http://www.freemedia.co.tz/daima/2007/7/26/habari4.php
Wawakilishi wambana Shamuhuna
na Mwandishi Wetu, Zanzibar
WAJUMBE wa Baraza la Wawakilishi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na wale wa Chama cha Wananchi (CUF), wamembana Naibu Waziri Kiongozi na Waziri wa Habari, Ali Juma Shamuhuna kwa kuvitumia vibaya vyombo vya habari vya umma dhidi ya wapinzani.
Aidha, baadhi ya wajumbe wamesema wizara yake inachangia baadhi ya waandishi wa vyombo vya serikali kuwa ombaomba kutokana kutolipwa posho zao na kupatiwa maslahi duni.
Walitoa mfano tangu kuanza kikao cha bajeti ya serikali katika mwaka wa fedha 2007/08 mwezi uliopita, mawaziri vivuli wamekuwa wakikatiwa hotuba zao katika Televisheni Zanzibar na Radio Zanzibar, mara wanaponyanyuka kwa ajili ya kuwasilisha hotuba zao.
Mwakilishi wa Muyuni, Ramadhan Nyonje Pandu (CCM), alisema wizara hiyo imekuwa haiwatendei haki wafanyakazi wake katika vyombo vya habari, kwa vile waandishi wa habari wanaofuatilia shughuli za baraza hilo hawajalipwa posho tangu Januari, mwaka huu.
Kiongozi wa upinzani katika baraza hilo, Abubakar Khamis Bakar, alisema kwamba mwenendo wa utendaji wa vyombo vya habari vya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), si wa kuridhisha katika uimarishaji umoja wa kitaifa, demokrasia na misingi ya utawala bora.
Alisema kwamba yeye binafsi atakuwa mgumu kupitisha bajeti ya wizara hiyo hadi atakapopata maelezo ya kutosha juu ya sababu za vyombo hivyo vya umma kutotenda haki.
Naye Mwakilishi wa Jimbo la Mji Mkongwe, Fatma Fereji (CUF), alisema kwamba pamoja na vyombo hivyo kutakiwa katika muafaka wa CCM na CUF wa mwaka 2001 kutenda haki, hali bado haijabadilika hadi hivi sasa.
Alisema kwamba ni jambo la kushangaza kuwa, tangu kikao cha bajeti kianze, vyombo hivyo vimekuwa havionyeshi hotuba za mawaziri vivuli na hukata matangazo baada ya mawaziri wa serikali kuwasilisha bajeti zao.
Alisema kwamba waziri lazima atoe maelezo ya kutosha kwa nini vyombo hivyo vinashindwa kubadilika, hasa kwa kuzingatia waziri anayeviongoza ni miongoni mwa waliokuwa makamishana wa tume ya kusimamia muafaka huo wa CCM na CUF.
Mwakilishi wa CUF kutoka Jimbo la Mtambwe, Salim Abdallah Hamad, alisema uhuru wa vyombo vya habari bado haujapatikana Zanzibar na ndiyo maana vyombo hivyo huripoti matukio kinyume cha yalivyotokea.
Mwakilishi wa Jimbo la Kwamtipura, Hamza Hassan (CCM), aliitaka Wizara ya Habari, Utamaduni na Michezo Zanzibar, iwarejeshe wafanyakazi walioondoshwa, hasa kutoka TVZ na kupelekwa katika idara nyingine.
Aidha, alisema kwamba imefika wakati Serikali ya Zanzibar ihakikishe viongozi wanawashirikisha waandishi wanapofanya ziara za nje kama anavyofanya Rais Jakaya Kikwete.
Mwakilishi huyo alisema kwamba ni jambo la kushangaza serikali imesema mwelekeo wake ni kutonunua magari ya mitumba, lakini hivi sasa wafanyakazi katika sekta ya habari wanafanya kazi katika mazingira magumu kutokana na magari yaliyonunuliwa hivi karibuni kuharibika yakiwa yamenunuliwa katika muda mfupi.