Huko Kibera, ambako ni maarufu sana kwa jina la mtaa wa mabanda jijini Nairobi, kukatika umeme ni jambo la kawaida. Miriam Achieng Kenyatta, mwenye umri wa miaka 23, huwa anasoma akitumia taa ndogo na mishumaa. Kwa kuwa hakuwa na uwezo wa kulipia madarasa ya Kichina, alibadilisha nyumba yake ndogo kuwa mazingira halisi ya lugha hiyo: kwa kubadilisha majina ya watu kwenye simu yake na kuyaandika kwa Kichina, kurudia maneno kutoka kwenye tamthilia za Kichina, kutafuta watu wa kuzungumza nao kupitia app za simu, na kujiunga na vyumba vya mazungumzo vya Kichina. Ndani ya miezi sita, aliweza kuelewa tamthilia ya Kichina ya dakika 40 bila kuhitaji maneno ya tafsiri kwenye skrini.
Mwezi Aprili, alifika ngazi ya fainali nchini Kenya katika shindano la 25 la Umahiri wa Lugha ya Kichina lijulikanalo kama "Daraja la Kichina". Akiwa amevalia joho jekundu, alipiga ngoma iliyochorwa picha ya dragon na kusoma shairi la "Wimbo wa Upepo Mkuu", shairi la kale la miaka 2,000 lililotungwa na Liu Bang. Alishinda shindano hilo la ngazi la Kenya na kupata nafasi kati ya washiriki 15 bora wa fainali ya dunia nchini China.
Alisoma rasmi katika Taasisi ya Confucius ya Chuo Kikuu cha Nairobi kwa miezi mitatu pekee kabla ya kuacha masomo kwa sababu hakuweza kulipa ada ya mtihani ya shilingi 2,000. Kujifunza mwenyewe na kufanya mazoezi na klabu ya ngoma ya taasisi hiyo kulibadilisha hali yake. Mkufunzi wa klabu hiyo alipendekeza arudishwe chuoni, hatua iliyomfanya kuwa mshiriki muhimu, kupewa mafunzo maalum, na kusamehewa ada.
Wakati wa mafunzo makali, alikataa kukaa bwenini na badala yake alikuwa akirudi nyumbani kila siku, iwe jua au mvua, ili kumtunza mdogo wake wa kiume. Anaishi Kibera, eneo ambalo wazazi wake walihamia miaka 25 iliyopita wakitokea Kisumu kutafuta elimu bora. Familia hiyo ya watu sita iliishi katika nyumba ndogo ya udongo na mabati yenye ukubwa wa mita za mraba 15. Mama yake, Hellen Juma Bonyo, hajawahi kununua nguo mpya tangu watoto wake wazaliwe, alikuwa akijishughulisha na biashara ya karanga na sabuni kuanzia saa 11 alfajiri hadi baada ya saa 3 usiku. Fedha zilikuwa tatizo sugu; gharama za chuo kikuu zilifikia shilingi 130,000 kwa mwaka. Ndugu na marafiki walitoa msaada kadiri walivyoweza, na babu yake mwenye umri wa miaka 92 aliandaa harambee iliyochangisha shilingi 40,000.
Bonyo hakuwahi kuhitimu shule ya upili na mara nyingi aliwaambia watoto wake, "Msiposoma sasa, mtaishia kuwa kama mimi." Hajawahi kujutia uamuzi wa kuishi Nairobi: "Kwa sababu tuliishi Nairobi, binti yangu aliingia chuo kikuu, akajifunza Kichina, na kuwa mtu wa kwanza katika familia yetu kupanda ndege."
Wakati Kenyatta alipopiga simu kutoa habari za ushindi wake, Bonyo alikuwa akiuza karanga. Alifunga kwa siku tatu ili kumwombea binti yake kabla ya safari hiyo. Akiwa China, Kenyatta alipanda Ukuta Mkuu wa China, alitembelea Kasri la Kale “Palace Museum”, na kujifunza kuhusu kampeni ya China ya kupunguza umaskini. Akiwa ameketi kwenye basi, alikumbuka sana nyumbani: "Barabara ya kawaida nchini China inaonekana kama barabara kuu jijini Nairobi. Niliwaza, kwa nini nyumbani kwetu kusiwe na barabara pana kila mahali? Natumai Kibera inaweza kuwa hivi siku moja."
Alisema umaskini ulimsukuma kufanya kazi kwa bidii, na sasa anatumai kutumia yale anayojifunza ili kuwapa fursa bora zaidi watu wenye ndoto huko Kibera. Mama yake anaamini kuwa ujuzi wa binti yake wa lugha ya Kichina utamwezesha kuwa na maisha mepesi zaidi.
Kenyatta, ambaye ni mwanafunzi wa uhandisi, amepata udhamini wa masomo ya Kichina kwa miezi 18 katika Chuo Kikuu cha Ualimu cha Tianjin baada ya kuhitimu, na kisha anapanga kuomba nafasi ya masomo ya shahada ya uzamili nchini China. Wadogo zake wawili wa katikati sasa wanasoma shule ya bweni wakiishi hukohuko, na wazazi wake wamerudi Kisumu. Yeye anaishi Kibera na mdogo wake wa mwisho; husafiri kwenda darasani, humpikia chakula, na kumfundisha Kiingereza mtandaoni.
Alipoulizwa kuelezea siku yake bora, aliwaza kwa muda: "Siku ya kawaida kabisa. Naamka bila kuwa na wasiwasi kuhusu wapi nitapata kifungua kinywa, au kama kunywa chai kutamaanisha sitapata chakula cha mchana. Sitahitaji tena kuuliza kwamba, 'Tutafanyaje?'"