Hii dunia ina vitu vya ajabu sana na vya kushangaza. Kuna historia baadhi unaweza unaweza kushangazwa nazo mojawapo ikiwa hii niliyopata kusimuliwa.
Msitu wa Nyumbanitu una historia nyingi za kushangaza. Msitu huu upo katika Wilaya ya Wanging'ombe mkoa wa Njombe. Msitu huu nimepata kusimuliwa kuwa endapo mwanamke atakuwa kwenye siku zake basi hatoruhusiwa kuingia katika msitu huo, Ikiwa atakaidi basi akiingia kwenye huo msitu ndio utakuwa mwisho wake wa kuonekana maana atapotea mazima.
Nadhani hili jambo mnaona linavyostaajibisha. Najiuliza huu msitu una nguvu na miujiza gani mpaka uweze kuwatendea hivyo dada zetu.
Msitu wa Nyumbanitu una historia nyingi za kushangaza. Msitu huu upo katika Wilaya ya Wanging'ombe mkoa wa Njombe. Msitu huu nimepata kusimuliwa kuwa endapo mwanamke atakuwa kwenye siku zake basi hatoruhusiwa kuingia katika msitu huo, Ikiwa atakaidi basi akiingia kwenye huo msitu ndio utakuwa mwisho wake wa kuonekana maana atapotea mazima.
Nadhani hili jambo mnaona linavyostaajibisha. Najiuliza huu msitu una nguvu na miujiza gani mpaka uweze kuwatendea hivyo dada zetu.
- Tunachokijua
- Nyumbanitu na msitu unaopatikana katika kijiji cha Mlevela, kata ya Mdandu, Wilaya ya Wanging'ombe, ni kilomita 15 kutoka Njombe mjini.
Jina "Nyumbanitu" ni muunganiko wa maneno mawili; nyumba na nitu. Neno "Nitu" manaa yake ni Giza au Nyeusi. Hivyo Nyumbanitu maana yake ni nyumba yenye giza au nyumba nyeusi.
Maajabu yake
Nyumbanitu si nyumba, kama lilivyo neno lenyewe, bali ni msitu mdogo, wenye ukubwa wa hekta moja na nusu (1.5) tu, lakini una mambo ya kustaajabisha.
Kuna watu ambao huenda Nyumbanitu kuomba mizimu iwape baraka katika mambo yao. Kuna ambao huenda kuchuma dawa, wengine huenda kujifunza mila na desturi za mahali hapo ambazo pengine zinahusiana na ushirikina n.k.
Maajabu ya msitu huo ni kuku weusi wenye midomo myekundu ambao wahifadhi wanasema hawazeeki, hawafugwi na wala hawaliwi.
Kuku hao huonekana kwa wingi wakati wa mavuno na inapofika masika, hawaonekani tena.
Mfano wa kuku wanaopatikana kwenye msitu huo
Pia, inasemekana huwa kuna ng’ombe na kondoo ambao huingia kwa msimu na rangi ya wanyama wanaongia kwenye msitu huo ni nyeusi. Inadaiwa kuwa mtu anayeiba kuku hawa anaweza kugeuka kuwa kichaa.
Septemba 2022, Serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii iliutangaza rasmi msitu huu kuwa miongoni mwa vivutio muhimu vya utalii na utamaduni Tanzania.
Wanawake wenye hedhi kuingia kwenye msitu huo
Kabla ya kuingia kwenye msitu huo, waangalizi wa msitu hutoa tangazo la kuwataka wanawake walio katika siku zao, yaani kwenye hedhi, kutothubutu kuingia.
“Ni mwiko na ikiwa utajidanganya kufanya hivyo, basi miaka yako yote utabaki hivyo hivyo, hakuna dawa ya kutibu”
Maneno haya yanathibitishwa na mwandishi mmoja wa gazeti la Mwananchi aliyetembelea msitu huo kupitia andiko lililochapishwa na gazeti hilo Agosti 28, 2016.
Aidha, Septemba 26, 2020, Mtumiaji wa JamiiForums aliwahi pia kuweka andiko lenye ujumbe unaofanana na huu. Alisema;
Si ruhusa Kwa wanawake walio katika siku zao, yaani kwenye hedhi kuingia ndani ya msitu huo. Ni mwiko kabisa, na ikiwa mwanamke atajidanganya kufanya hivyo, basi miaka yake yote atabaki akitokwa na damu ya hedhi bila ukomo na hakuna dawa ya kumtibu.
Wanawake wajawazito pia hawaruhusiwi kuingia. Marufuku hii imeandikwa kwenye ubao maalumu nje kabisa ya msitu huo mdogo. Ili kuhakikisha kuwa wageni (watalii) hawakiuki marufuku hiyo, mwenyeji huirudia marufuku hiyo kwa mdomo ili kutilia mkazo.
Sharti lingine kabla ya kuingia msituni humo ni kuvua viatu, kofia na vilemba. Baada ya kufuata taratibu zote, mwenyeji huomba ruhusa ya kuingia msituni kwa kuongea maneno ya kibena.
Mtu yeyote anayepuuzia masharti haya hupatwa na kitu kibaya, ikiwemo kupotelea msituni humo
Julius Msigwa, mwongozaji wa watu wanaotembelea msitu huo akifanya mahojiano na Gazeti la Mwananchi anasema simulizi za ajabu za msitu huu na kuwapo kwa imani za kishirikina, ziliwafanya baadhi ya waumini wa Kikristo wanaojulikana kama walokole vijiji vya jirani kuamua kuingia ili kufanya maombi.
“Hili si tukio la siku nyingi, hawa watu walitaka kuja kukemea mashetani ndani ya msitu. Siku ya maombi yao, walokole hao walijikusanya na kuanza safari hadi msituni. Walipofika waliamua kuingia bila kukutana na mwenyeji yoyote wala kufuata mila na desturi za kuingia msituni ili kutoka salama.
“Walikuja moja kwa moja hadi kwenye mti huu, walianza kukemea na kuvuruga utaratibu wa hivi vifaa vya matambiko,” anasema.
Julius anasema watu hao waliendelea na maombi kwa siku nzima, ilipoisha wakataka kuanza safari ya kutoka ndani ya msitu.
Julius anasema hakukuwa na njia ya kuwawezesha kutoka ndani ya msitu.
“Walijikuta wakiendelea kupiga kelele, wakizunguka msitu mzima lakini hakukuwa na msaada kwa wao kutoka"
"Watu waliokuwa wakipita nje ya msitu walisikia kelele, hata hivyo hawakuwa na msaada wowote kwani hata wao hawawezi kuingia bila kufuata taratibu"
Ushahidi wa madai ya kufanya hedhi isikome
JamiiForums haijapata uthibitisho wa moja kwa moja kutoka kwa mwanamke aliyewahi kupatwa na tatizo hili, lakini imezungumza na Mpokezi wa Wageni na Kiongozi wa Kimila katika Msitu wa Nyumbanitu, Julias Vangamel, anaelezea:
Nyumbanitu ni Msitu wa Mila, sehemu zote zenye Misitu ya Kimila kuna taratibu na miiko yake, hivyo ni kweli kuwa sehemu ya miiko iliyopo ni kuwa Mwanamke hatakiwi kuingia akiwa katika siku zake za hedhi.
Mila zikishawekwa lazima zisuatwe kwa kuwa tofauti na hapo kutakuwa na madhara yake.
Mwanamke akiingia kwenye pango lililopo katika Msitu wa Nyumbanitu akiwa kwenye mzunguko wake wa hedhi anaweza kujikuta anaendelea kuwa hivyo siku zote, yaani mzunguko wa hedhi ambao hauna ukomo.
Madhara ya aina hiyo yamewahi kutokea miaka ya nyuma, ndio maana likawekwa hilo angalizo, kwa miaka ya hivi karibuni haijawahi kutokea.
Wanawake wakifika hapa kwa ajili ya kuingia pangoni wanajulishwa masharti ya kimila ikiwemo hilo na wanalizingatia.
Uthibitisho huu hautofautiani na maelezo yaliyofafanuliwa awali kutoka kwenye vyanzo mbalimbali, yote kwa pamoja yakiweka ukweli wa msingi wa madai haya.
Aidha, Vangamel ameiambia JamiiForums kuwa Agosti 7, 2023, Wanafunzi zaidi ya 200 kutoka shule mbalimbali walitembelea msitu huo kwa ajili ya kujifunza mambo mbalimbali.