Kwa kweli tuliokuwa wapenzi wa muziki enzi hizo ,uwezo wa Juma kilaza uikuwa mzuri tu. Na kwa kumtendea haki hakustahili kupewa jina la kigezo cha umbumbumbu. Lakini katika wanamuziki bora kumi Tanzania ya wakati huo 1970_1975 .mifano ya bending zilizovuma wakati huo ni AtomicJB , Jamhuri JB, Tabora JB, Jamhuri JB, nk
,Kuniaminisha kuwa Kilaza alikuwa mbumbumbu ni sawa na kusema leo kwa kuwa diamond ana wapenzi kuliko kiba basi Ali Kiba apewe jina lisiloenda na hadhi yake wakati magwiji wa muziki wanakiri kuwa Kiba ana Sauti bora kuliko diamond . Tofauti ni kuwa diamond anajituma zaidi ya mwenzie. Mwenzie hahangaiki kutoa nyimbo SAA zote. Kiba anafanya Kazi at leisure muziki anafanya kama burudani .Na enzi hizo kilaza alikuwa ameajiriwa railway na ninasikia alikuwa na cheti cha ufundi FTC. Sasa Kilaza hakutegemea Muziki ili apate mlo wa siku,, wakati Mubaraka alikuwa amefukuzwa kidato cha tatu na marehemu Elinawinga kwa kuona hasomi anatoroka usiku pale Mzumbe sekondari kwenda kupiga Muziki. Kwa hiyo Mubaraka muziki ilikuwa ndio maisha.ndio tofauti ya hao magwiji wa enzi hizo .MUZIKI UKIWA NYUZI BIN NYUZI.hakukuwa na macomputer kuboost uwezo wa MTU .msiomjua Kilaza hapo ndio kifupi cha heshima kubwa tu ambayo Leo tuliomhusudu tunasikitika akipewa reference isiyo stahiki yake.
Japo nimechelewa kujiunga na thread hii. Nmeona vema kushirki kwa kuuunga mkono hoja ya Jonas Kigweza inayopinga imani kwamba Juma Kilaza alikuwa ni mwanamuziki mwenye uwezo mdogo saaana aliyetamba kuwa mahiri katika upigaji wa gitaa la solo na kuja kubwaga vibaya na Mbaraka Mwishehe Mwaruka katika mashindano. Habari hii haina ukweli hata kidogo, na inahitaji uafafanuzi ili kuiweka sawa.
Kama alivyoandika Jonas sisi tuliokuwepo wakati huo ndio tunajua vizuri habari za muziki zama hizo. Mimi nilikuwa Morogoro kipindi bendi za Morogoro Jazz na Cuban Marimba zikiwa zinavuma, na kwa mapenzi ya muziki niliyokuwa nayo nilkuwa sihudhurii kwenye kumbi za muziki pekee bali hata kwenye mazoezi yao na kuona jinsi wanavyotunga nyimbo. Makao ya Morogoro jazz (eneo la mazoezi lilikuwa karibu na ukumbi wa Social Hall la Morogoro) Na Cuban Marimba walikuwa wakitumia chumba kimoja katika Social hall iliyokuwa Kichangani (baadae walihama).
Ni ukweli usiopingika kwamba Mbaraka alikuwa na uwezo mkubwa wa kutunga, kuimba, kupiga magitaa yote, na hata filimbi ikiwa ni pamoja na Hawaian gitaa ambalo halikudumu sana katika muziki wa kitanzania. Hata hivyo chombo alichopendelea zaidi ni solo gitaa
Kuhusu Juma Kilaza naye alikuwa na uwezo wa kupiga magitaa yote, kutunga na kuimba. Isipokuwa si kweli kwamba alikuwa akipiga gitaa la solo kwenye kumbi na hata wakati wa kurekodi Kericho ama radio Tanzania (wapiga gitaa wa solo wa kutegemewa walikuwa wakibadilika mara kwa mara – Waziri Nyange, Joachim Ufuta na wengineo) lakini mpiga gitaa wa solo wa muda mrefu zaidi katika miaka ya 1970 alikuwa ni Dr. Joachim Ufuta. Kilaza alikuwa kiongozi, mwimbaji na mtunzi mkuu wa Cuban Marimba. Izingatiwe kwamba bendi hizi mbili zilikuwa na ushindani na ushabiki mkubwa sana unaofanana na Yanga na Simba.
Najaribu kufikiria kama kweli wangeamua kuweka mashindano kati ya bendi hizo zama hizo sijui ingekuwaje maana kwa uhasama uliokuwepo nadhani hata mashindano yenyewe yangeshindikana. Ila kuna nyakati maalum bendi hizi zilikuwa zikiombwa kutumbuiza pamoja haswa wakati sherehe za kitaifa na hata hivyo ilikuwa kash kash kweli huku Kilaza akisema moto wa Ambiyansey….na kuamsha mashabiki ambao kweli walikuwa wakiwasha moto ,na huku Mbaraka akisema Moto wako washa nje hapa maji yatazima, yaani walikuwa wakipigana vijembe hata ndani ya ukumbi.
Kwa ufupi Kilaza alikuwa gwiji wa muziki na hadi leo bado nyimbo zake zinatamba, utakumbuka wimbo wa
maisha ya sasa uliokuwa ukitumiwa na Kikundi cha Kaole kufungua kipindi cha mchezo wao wa kuigiza ITV. Wimbo huo aliutunga, kuimba na kuerekodi akiwa na bendi yake mwenyewe aliyoiunda baada ya kujitenga kutoka Cuban Marimba mwaka 1973. Kilaza alianza kupiga gitaa la solo baadae kabisa akiwa TK Lumpopo baada ya Joachim Ufuta kuhama bendi na wakati alipounda bendi yake nyingine
Magola International huko Kenya. Jambo jingine la kuliweka sawa ni kwamba Kilaza ana sifa moja iliyotukuka yeye ni sehemu ya wanamuziki wachache sana nchini waliokuwa wakitunga nyimbo zao wenyewe bila kuiga, tena kwa mtindo wa mashairi(guni) na Kiswahili safi, hakupiga Kopi na wala alikuwa hapigi nyimbo za bendi nyingine kama ilivyokuwa kawaida enzi hizo haswa kwa kuiga nyimbo za Kongo. Hebu ona sehemu ya utunzi huu wa Juma Kilaza (mwaka 1968).
Kwako ni kwako wewe mtoto
Hata ikiwa pango ni kwako
Kwako ni kule mwana utokako
Wazee wako kule waliko
Na huko ndiko masikani kwako …….
Hivyo kwa nguvu zote naunga mkono haja ya kuweka suala hili sawa ili kumtendea haki Kilaza ambaye alifanya kazi nzuri ya uimbaji na kuinua lugha ya Kiswahili, licha ya kutoa wanamuziki wengine waliokuja kuwa mahiri sana ikiwa ni pamoja na Chiriku Hemed Maneti aliyedumu naye Cuban Marimba na TK Lumpopo kwa zaidi ya miaka mitatu. Mambo mengine yamewekwa sawa vizuri sana na Jonas.