TANZIA Mwanasheria Mkuu wa Kwanza Mzalendo na Jaji Mstaafu Mark Bomani afariki dunia

TANZIA Mwanasheria Mkuu wa Kwanza Mzalendo na Jaji Mstaafu Mark Bomani afariki dunia

..gazeti la the citizen wameandika kwamba Mark Bomani amefariki akiwa na miaka 88.

..kama huo ndio umri wake sahihi basi atakuwa amezaliwa mwaka 1932.
Hao ndio wako sahihi. Hata kuzaliwa kwake si Pemba bali Sizaki, Bunda, Lake Province (sasa mkoa wa Mara).
 
Amejumuika Kuwafariji Wapendwa Wetu Leo

FB_IMG_15999864557019194.jpg
FB_IMG_15999864509014103.jpg
FB_IMG_15999864467016483.jpg
 
Huyo mjane ni dada yake na akina mwapachu aisee wanafanana mno Rip mzee bomani
 
*Mh. JAJI MARK BOMANI: _"AG"_ WA KWANZA MZALENDO NCHINI AFARIKI DUNIA!!!*

_MZEE WA ATIKALI_ ✍️✍️✍️

1. *Usuli*

Mh.Jaji mstaafu MARK DANHI BOMANI, mmoja wa viongozi waliolifanyia Taifa letu mambo mengi na aliyekuwa akijua mambo lukuki ya nchi yetu ambayo _Bongolanders_ wengi hawayajui, ameaga dunia jana usiku tarehe 10.9.2020 akiwa na umri wa miaka 88 kutokana na maradhi.

Je, Mh. BOMANI, mmoja wa Watanzania waliokuwa wakiheshimika sana nchini, alitokea wapi na mchango wake kwa Taifa ni upi?.

2. *MARK BOMANI Azaliwa*

MARK DANHI BOMANI alizaliwa siku ya Jumamosi, tarehe 2.1.1932 huko Uchashi, Bunda, mkoani Mara. BOMANI ni mmoja wa watoto wa Mzee BOMANI ambapo wengine ni Daniel, Paul, Emma, Francis, Martha, Yona, Washington, Fibe & Neema.

3. *Safari ya Elimu ya BOMANI*

3.1 *Shule ya Msingi*

BOMANI alisoma shule ya msingi Mwamanyili, Nassa ambapo baba yake mzazi ndiye alikuwa mwalimu wake.

3.2 *Shule ya Kati*

Mwaka 1945, serikali ya kikoloni ilijenga shule ya wavulana ya Bwiru na kuwataka wanafunzi wakafanye mtihani. Mzee BOMANI, baba yake MARK, alimuomba jirani yao, Mzee SHITEBO, ampeleke MARK kwa baiskeli kwenda kufanya mtihani huo na MARK akafanya mtihani na kuwa mmoja wa wanafunzi wa mwanzo 30 waliochaguliwa kujiunga na _"Bwiru Boys"_. Jina la BOMANI ndilo lililokuwa la kwanza kwenye orodha ya waliochaguliwa ikimaanisha yeye ndiye aliyepata alama za juu kuliko wote. Akiwa shuleni hapo, talanta ya uongozi ambayo BOMANI alijaliwa na Mola wake ilianza kujionesha kwani alikuwa mmoja wa ma-"Prefects".

Mwaka 1950, BOMANI alifanya mtihani wa darasa la 10. Kwavile alikuwa _Kipanga_ aliweza _kupasua pepa_ na kuwa mmoja wa wanafunzi wawili (2) tu kati ya wanafunzi 30 wa "Bwiru Boys" waliofaulu na kuchaguliwa kujiunga na _"Tabora School_, shule iliyokuwa bora na maarufu kuliko zote Tanganyika enzi hizo.

3.3 *Elimu ya Sekondari*

BOMANI alipojiunga na _"Tabora School"_ kwaajili ya elimu ya sekondari, alikutana na vijana hodari na _"vipanga"_ kama yeye. Darasa lao ndilo linahesabika kuwa na _"vipanga"_ kuliko madarasa yote katika historia ya shule hiyo. Katika darasa hilo, Mh. EDWIN MTEI, aliyekuwa mwanafunzi bora nchini mwaka wao _"Tanganyika One"_, ndiye aliyekuwa akiongoza darasani.

BOMANI akiwa shuleni hapo alikuwa _"Senior Prefect"_ wa bweni.

Walipofanya mtihani wa mwisho wa kumaliza shule, _"vipanga"_ 7 wa darasa hilo walichaguliwa kwenda _"Makerere college"_, Uganda ambao ni EDWIN MTEI, MARK BOMANI, GEOFREY MMARI, J.PENDAEL, ROWLAND MWANJISI, O. MWAMBUNGU & G. SIMITI.

3.4 *Makerere College*

Chuoni Makerere, BOMANI alisomea Uchumi na Siasa. Alipokuwa _"First year"_, MWAI KIBAKI alikuwa _"Third year"_. MWAI KIBAKI _alipasua pepa_ na kubakishwa chuoni hapo kama _"Tutorial Assistant"_ hivyo akamfundisha BOMANI. Akiwa Makerere, BOMANI talanta yake ya uongozi ilizidi kujitanabaisha kwani alikuwa Rais wa Umoja wa Wanafunzi (Makerere Students Guild).

Baada ya kuhitimu vizuri masomo yake Makerere, BOMANI alikwenda Uingereza kusomea Sheria.

3.5 *Uingereza*

BOMANI alienda London, Uingereza kusomea Sheria kwenye Chuo cha "London University". Akiwa huko, akakutana na CHARLES NJONJO ( aliyekuja kuwa AG wa Kenya-1963) na alikutana tena na MWAI KIBAKI (aliyekuja kuwa Rais wa Kenya) aliyekwenda kusomea _"Masters"_ ya uchumi (London School of Economics).

4 *BOMANI Akutana na KAMBONA*

Akiwa Uingereza, BOMANI alikutana na OSCAR KAMBONA aliyekwenda huko pia kusomea Sheria.

5. *BOMANI Awa _"Best Man"_ Harusi ya KAMBONA*

Tarehe 19.11.1960, Bw. OSCAR KAMBONA alifunga ndoa ya kukata na shoka na Bi. FLORA URIYO huko Uingereza. Bi FLORA alikuwa ni binti mrembo aliyewahi kuwa _"Miss Tanganyika"_. BOMANI ndiye alikuwa mpambe wa KAMBONA _"Best Man"_. Mwalimu NYERERE, aliyekuwa Uingereza kuhimiza uhuru wa Tanganyika, ndiye aliyemtoa Bi. FLORA siku ya harusi pale St. Paul's Cathedral. Harusi hiyo ilikuwa ya kipekee na iliandikwa sana kwenye magazeti ya Uingereza.

6 *BOMANI Arejea Nchini*

BOMANI alihitimu vizuri masomo yake ya Sheria ikiwa ni pamoja na mafunzo Lincoln's Inn na kurejea nchini mwaka 1962.

7. *BOMANI Awa Mtanganyika wa 3 Kuwa Wakili*

BOMANI aliporudi nchini aliapishwa kuwa Wakili tarehe 21.1.1962. BOMANI akawa Mtanganyika wa tatu kuwa Wakili baada ya HUMPHREY MKONDYA na JUMA MAWALLA.

8. *Bw. BOMANI Aanza Kazi ya Uwakili*

Mara tu baada ya kuapishwa, Bw. BOMANI alifanya kazi ya uwakili wa kujitegemea mjini Mwanza lakini baadaye akaitwa kufanya kazi serikalini.

9. *Mh. BOMANI Ateuliwa Deputy AG*

Rais NYERERE alimteua BOMANI kuwa Naibu Mwanasheria Mkuu wa Tanganyika mwaka 1963, huku "AG" akiwa Mzungu, ROWLAND BROWN.

10. *Familia ya BOMANI Yaweka Rekodi ya Kuwa na Viongozi 2 Wakubwa*

Mwaka huo wa 1963, Rais NYERERE alimteua Mh. PAUL BOMANI kuwa Waziri wa Fedha. Hivyo, kwa Mh. MARK kuwa _"Deputy AG"_ maana yake familia ya BOMANI ilikuwa ndiyo yenye ndugu wenye nyadhifa za juu kabisa serikalini.

11. *Mh. BOMANI Ashiriki Kutayarishaji Nyaraka za Muungano*

Kazi kubwa kabisa ya mwanzo aliyoifanya Mh. BOMANI akiwa _"Deputy AG"_ ilikuwa ni kusaidiana na _"AG"_ Bw. BROWN kutayarisha nyaraka zote za kisheria za Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, kazi aliyoitekeleza kwa weledi wa hali ya juu.

12. *Mh. BOMANI Ateuliwa kuwa AG wa TZ*

Mwaka 1965, Mh. BOMANI aliteuliwa na Rais NYERERE kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali "AG", akiwa na miaka 33 tu na bado _"Bachelor"_. Hivyo, Mh. BOMANI akawa Mzalendo wa kwanza nchini kushika cheo hicho.

13. *Rais NYERERE Amwagiza _AG_ BOMANI Akatafute Jaji Mkuu Nje*

Baada ya nchi yetu kupata uhuru ilikuwa ni dhahiri kwamba hatukuwa na Wanasheria wa kutosha. Hii ni kwasasabu Chuo pekee Afrika Mashariki enzi hizo, Makerere college _"The Havard of Africa"_ ilikuwa haifundishi fani hiyo. Waliotaka kusomea Sheria ilibidi kwenda India au UK. Aidha, Udsm ndio kwanza ilikuwa imeanzishwa (25.10.1961).

Hivyo, Mwalimu akamtuma _AG_ BOMANI aende nje ya nchi kutafuta Jaji Mkuu, baadhi ya Majaji na Mahakimu, kama Mh. BOMANI alivyowahi kuelezea--:

_*"Mpaka wakati huo, Jaji Mkuu alikuwa Mzungu (Sir Ralph Windham). Aidha, Majaji wote walikuwa Wazungu na Mahakimu wengi walikuwa wazungu na Wahindi wachache. Mwalimu akanipa kazi ya kwenda nje kuwatafuta. Nilikwenda Nigeria, Sierra Leone na West Indies"*_.

14. *_AG_ BOMANI Afanikiwa Kumuibua JAJI MKUU*

Ziara hiyo ya _AG_ BOMANI ilikuwa ni ya mafanikio makubwa kwani alifanikiwa kumpata mtu aliyekuwa na sifa za Jaji Mkuu, kama Mh. BOMANI alivyoeleza-:

_*"Nilifanikiwa kumpata Bw. Telford Georges toka Trinidad & Tobago aliyekuwa na vigezo vyote vya Jaji Mkuu"*_.

15. *AG BOMANI Afanikiwa Kumpata Jaji Mmoja na Mahakimu 20*

_AG_ BOMANI alifanikiwa pia kumpata Jaji GABRIEL ONYIUKE wa Mahakama Kuu ya Nigeria na Mahakimu 20 toka Nigeria. Jaji Mkuu, Jaji ONYIUKE na Mahakimu hao 20 walitusaidia sana, kama Mh. BOMANI alivyodadavua-:

_*"'Jaji Mkuu Georges alifanya kazi kubwa na nzuri sana ya kuweka msingi imara wa Idara ya Mahakama na Mahakimu hao 20 pia walitusaidia sana kupunguza wingi wa kesi"*_.

16. *_AG_ BOMANI Afunga "Ndoa ya Mwaka" na Bi RAHMA MWAPACHU*

Mwaka 1967, _"AG"_ BOMANI alifunga pingu za maisha na Bi. RAHMA MWAPACHU (dada wa Mh. HARRITH BAKARI & JUMA MWAPACHU). Harusi hii huenda ilikuwa ndio bora zaidi kuliko zote zilizofungwa miaka ya 1960s. Harusi hii ilikuwa na _"Best men"_ wawili badala ya mmoja ambao walikuwa ni Mh. CHARLES NJONJO, _AG_ wa Kenya, na _"Advocate"_ JUMA MAWALLA, Mtanganyika wa kwanza kuwa "Barrister", UK mwaka 1960.

17. *Kuvunjwa Vyama Vya Ushirika Kulimkera Mno Mh. PAUL BOMANI*

Mwaka 1968, serikali ilikuja na uamuzi wa kuvivunja vyama vya ushirika. Kitendo hiki kilimkera mno Mh. PAUL BOMANI aliyekuwa Waziri wa Ushirika na Muasisi wa Ushirika nchini hadi akaribie kuutema uwaziri, kama Mh. BOMANI anavyoelezea-

_*"Uamuzi huo ulimsononesha sana kaka yangu Paul. Yeye akiwa Waziri mhusika na mimi nikiwa Mwanasheria Mkuu tulifanya mazungumzo magumu sana ikiwa ni pamoja na uwezekano wa yeye kujiuzulu. Lakini tukaona kujiuzulu kungeweza kuchafua hali ya hewa nchini hivyo tukakubaliana asijiuzulu"*_.

18. *_AG_ BOMANI Aendesha Kesi ya Uhaini 1970*

_AG_ BOMANI ndiye aliyeendesha kwa weledi mkubwa kesi ya kwanza ya Uhaini nchini iliyoanza kurindima Mahakama Kuu Jumatano, tarehe 24.6.1970 dhidi ya washtakiwa 7, akiwemo OSCAR KAMBONA (BOMANI alikuwa _"Best Man"_ wa KAMBONA) waliotaka kupindua serikali ya Rais NYERERE kati ya tarehe 4.3.1968 na 12.10.1969. Washtakiwa 4, akiwemo BIBI TITI MOHAMED, walipewa kifungo cha maisha, wawili miaka 10 na mmoja aliachiwa huru.

19. *Sheria ya Ndoa 1971 Ilimuhenyesha Sana _AG_ BOMANI*

Akiwa _AG_, Mh. BOMANI alishiriki kupitisha sheria mbalimbali. Moja ya sheria zilizomsumbua na kumkosesha usingizi ni _Sheria ya Ndoa ya 1971_ . Sheria hii ilikuja na vipengele vipya vilivyoonekana kukwaza watu mf kuwatambua watoto wote, wa ndani na wa nje ya ndoa, kuwa wana haki sawa na pia haki sawa kwa mali ambazo mke na mume wamechuma pamoja. Mwishowe, sheria hiyo ikapitishwa na bunge.

20. *_AG_ BOMANI An'gatuka*

Baada ya kuhudumu kama _AG_ kwa zaidi ya muongo mmoja, _AG_ BOMANI aliamua kung'atuka mwaka 1976 na Rais NYERERE akamkubalia-:

_*"Baada ya kuwa Mwanasheria Mkuu kwa zaidi ya miaka 10 niliona nitafute kitu kingine cha kufanya. Mwalimu akaniruhusu"*_.

21. *Mh. BOMANI Ajiunga UN*

UN iliunda Kitengo maalum cha kuwaandaa Wanamibia kuendesha nchi yao ikipata uhuru kwa kutoa mafunzo. Mh. BOMANI akajiunga kitengo hicho ambacho kilifundisha waliokuja kuwa Makatibu Wakuu wote na baadhi ya Mawaziri wa Namibia.

22. *Mh. BOMANI Awa Mshauri Mkuu wa Serikali ya Namibia*

Mh. BOMANI alipata heshma ya kuteuliwa kuwa Mshauri Mkuu wa serikali ya Namibia kwa miaka 2 kabla ya kurejea nchini mwaka 1992.

23. *Mh. BOMANI Ateuliwa Mwenyekiti wa Kamati ya Wataalam 10*

Baada tu ya kurejea, Rais ALI HASSAN MWINYI alimteua Mh. BOMANI kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Katiba ya Wataalam 10 (Bara 5, ZNZ 5). Kamati hii ilileta mapendekezo mengi mujarab mf. Rais aweze kushtakiwa iwapo ametumia vibaya madaraka yake (Impeachment) na Rais wa ZNZ asiwe VP nk.

24. *Mh. BOMANI Ateuliwa Mwenyekiti Kamati ya Kupitia sekta ya Sheria*

Mwaka 1993, Rais MWINYI alimteua Mh. BOMANI kuwa Mwenyekiti wa Kamati Maalum ya kupitia sekta yote ya Sheria. Kamati hii ilifanya kazi nzuri na kutoa mapendekezo yaliyokubaliwa mf uanzishwaji wa "Law school". Kutokana na ubora wa kazi hiyo, mwaka 1997 WB iliitisha mkutano Washington, US wa nchi zilizoendelea ili kujifunza toka kwa TZ. Hii ilikuwa ni heshima kubwa kwa Mh. BOMANI.

25. *Rais MWINYI Amteua Mh. BOMANI Mwenyekiti Tume ya Utangazaji*

Mwaka 1993, Rais MWINYI alimteua Mh. BOMANI kuwa Mwenyekiti wa Tume ya Utangazaji, ambako alihudumu hadi 2002.

26. *Mh. BOMANI Na Kinyang'anyiro cha Urais 1995*

26.1 *Wananchi Wamtaka Agombee*

Mwaka 1995, baadhi ya wananchi na marafiki wa Mh. BOMANI walimuomba agombea Urais wa TZ lakini alisita kwani alikuwa ameishi sana nje (miaka 16). Shinikizo lilipokuwa kubwa, akachukua fomu.

26.2 *Mh. BOMANI Aweka rekodi ya Wadhamini*

Mh. BOMANI alipata wadhamini 1,050 akifuatiwa na Mh. JOHN MALECELA (925), licha ya kwamba ni wadhamini 250 tu waliohitajika. Hii iliakisi kukubalika kwake nchini.

26.3 *CC _Yafyeka_ majina 10*

Wajumbe wa CC ya CCM walipitia majina ya wagombea 16 waliorudisha fomu za Urais na kupendekeza NEC majina 6 (J. Kikwete, B.Mkapa, C. Msuya, Pius Msekwa, J. Warioba & M. Bomani) na kuyafyeka majina 10.

26.4 *Mh. BOMANI Awa wa NNE*

Katika upigaji kura kwenye NEC, Mh. BOMANI alikuwa wa 4 baada ya Mh. J. Kikwete, B. Mkapa & C. Msuya.

26.5 *NEC _Yamchinjia Baharini_ Mh. BOMANI*

Kanuni ya Chama ilieleza kuwa "NEC ya CCM itapitisha majina yasiozidi 5 na kuyapeleka Mkutano Mkuu". Kwa vile Mh. BOMANI alikuwa wa 4 basi aliamini jina lake nalo lingepelekwa Mkutano Mkuu. Aliumia sana-:

_*"Ghafla NEC ilibadili Kanuni na kuamua itafikisha Mkutano Mkuu majina 3 tu. Hivyo kalamu ya NEC ikapita juu ya jina langu. Niliumia sana"*_.

26.6 *Wapambe Wamtaka Mh. BOMANI Ajitoe CCM*

Mh. BOMANI alidadavua-

*_"Suala hilo lilileta utata mkubwa kwani baadhi ya mashabiki wangu na viongozi wa UVCCM walinitaka nijitoe CCM niunde chama kipya. Nilikataa"_*.

26.7 *Baba wa Taifa Amfariji Mh. BOMANI*

Baada ya Baba wa Taifa kuona wapambe wa Mh. BOMANI wamefura kwa hasira na kuleta mtafaruki mkubwa viunga mbalimbali vya Idodomia, alimwita Mh. BOMANI nyumbani-

_*"Hali hiyo ilimfanya Mwalimu aniite nyumbani kwake na kunisihi nisiuchukulie vibaya uamuzi huo wa NEC. Nilimwelewa"*_.

26.8 *Vyama vya Upinzani Vyamnyemelea Mh. BOMANI*

Baada ya songombingo hiyo, vyama vya upinzani _havikulaza damu_-

_*"Baadhi ya vyama vya upinzani vilinifuata na kuniomba niwe mgombea wao. Nilivikatalia kwavile nilikuwa na "principles" zangu"*_.

Hatimaye, Mh. BOMANI alifanikiwa kuwatuliza wapambe wake waliokuwa na munkari na hivyo suala hilo likaisha.

27. *Baba wa Taifa Amwomba Mh. BOMANI kuwa Msaidizi Wake*

Mwishoni mwa 1995, UN & OAU vilimteua MWALIMU JK NYERERE kuwa Mpatanishi wa mgogoro wa Burundi. Mwalimu akamuomba Mh. BOMANI kuwa Msaidizi wake (Facilitator's Representative). Akakubali. Hivyo akaanza kutekeleza jukumu hilo na Mwalimu Mei 1996 Mwanza. Miundombinu hafifu ikafanya upatanishi uhamie Arusha. Hadi Mwalimu anafariki 14.10.1999, hakuna maafikiano yoyote yaliyofikiwa. Octoba 1999, OAU ikamteua Mh. Nelson Mandela kuwa Mpatanishi mpya huku Mh. BOMANI akimsaidia. Agosti 2000, pande husika walifikia makubaliano na kusaini mkataba.

28. *Rais JK Amteua Mh. BOMANI Mwenyekiti Kamati ya Madini*

Mwaka 2007, Rais J. KIKWETE alimteua Mh. BOMANI kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya watu 12 kupitia upya sera ya madini. Kamati ilifanya kazi yake nzuri na kutoa ripoti.

29. *Mh. BOMANI Ataka Muundo wa Serikali 3*

Tarehe 13.6.2013, Mh. BOMANI aliongea na waandishi wa habari na kuipongeza Tume ya Warioba kwa kupendekeza muundo wa Muungano wa serikali tatu- :

_*"Huo ndio muundo unaofaa na hilo ndilo limekuwa pendekezo la Tume zote zilizowahi kuundwa kuhusu Muungano; yaani Tume ya Jaji Mkuu Nyalali 1991 na Kamati ya Jaji Robert Kisanga 1998"*_.

30. *Mh. BOMAN alikuwa- _" The Most Senior Living Advocate in TZ"_*

Moja ya kazi ambazo alikuwa akizifanya Mh. BOMANI ni ya uwakili kupitia Kampuni yake ya Uwakili _"Bomani & Company Advocates"_. Mh. BOMANI alikuwa ndiye _"The Most Senior Living Advocate "_ kwani aliapishwa tarehe 21.1.1962.

31. *Mh. BOMANI Awa Mjumbe Bodi ya Udhamini CCM*

Mwezi Julai 2018, licha ya umri mkubwa, Mh. BOMANI aliteuliwa kuwa mmoja wa Wajumbe 5 wa Bodi ya Kwanza ya Udhamini ya CCM. Hii ilikuwa ni heshma kubwa sana kwake.

32. *Familia ya Mh. BOMANI*

Mh. BOMANI ameacha mke, Bi. RAHMA MWAPACHU BOMANI na watoto watatu wa kiume ie HERI (Mchumi aliyesomea Wales na aliwahi kuwa CEO & MD wa KCB), CLEMENT & ANDREW.

Tarehe 18.6.2016, ANDREW aliteuliwa kuwa Mkurugenzi wa Mikakati na Mambo ya Nje wa chama cha upinzani cha UDP cha Mh. J. CHEYO, "Mzee wa Mapesa".

33. *Bw. & Bi BOMANI Washeherekea _"GOLDEN Wedding Anniversary"_*

Mwezi Agosti 2017, Mh. BOMANI na mkewe Bi RAHMA walisheherekea miaka 50 ya ndoa yao nyumbani kwao Mikocheni. Sherehe hiyo iliyofana ilihudhuriwa na viongozi wengi akiwemo Mh. ALI HASSAN MWINYI.

34. *Afya ya Mh. BOMANI Yatetereka*

Afya ya Mh. BOMANI ilitetereka kutokana na umri na magonjwa na kupelekea kulazwa hospitali ya TMJ, Mikocheni.

35. *Naibu PM wa Namibia Amtembelea Mh BOMANI Hospitalini*

Tarehe 3.12.2019, Bi NETUMBO NANDY NDAITWA, Naibu Waziri Mkuu wa Namibia, alimtembelea Mh. BOMANI hospitalini TMJ. Hii ilikuwa kuonesha uungwana kwani Mh. BOMANI alilifanyia mambo makubwa Taifa la Namibia.

36. *Mh. BOMANI Afariki*

Baada ya kusumbuliwa na maradhi kwa muda mrefu, Mh. BOMANI alifariki dunia usiku wa tarehe 10.9.2020.

37. *TAMATI*

Huyu ndie Mh. MARK DANHI BOMANI, mmoja wa wasomi wa kwanza kabisa nchini aliyeheshimika vilivyo kutokana na kutoa mchango mkubwa, ndani na nje ya nchi. Baba wa Taifa alimuamini sana na kumpa majukumu mazito huku akiwa kijana mdogo na pia Marais wengine walimteua kuwa Mwenyekiti kwenye Kamati mbalimbali ikikwenyej walivyomuamini na akahudumu kwa weledi wa hali ya juu!.

_*Mh. MARK DANHI BOMANI:- UMEVIPIGA VITA VILIVYO VIZURI, MWENDO UMEUMALIZA PUMZIKA KWA AMANI
 
Kumbe hapa unagundua zile story za Nyerere kuwa mtanganyika wa Kwanza kuwa na masters..ni za uongo mtupu
 
Daaah! Historia yake inasisimua! Nikategemea itaishia MAZISHI, KANDA YA ZIWA!
Any way! Pote ni nyumbani kwetu! MWANGA WA MILELE AANGAZIWE, APUMZIKE KWA AMANI. Amemaliza vita vyake!
 
Juma Mwapachu alikuwa Tanzania one kwny matokeo yake ya kidato cha nne

Baba yao alikuwa Frontliner wakati wa uhuru
Bakari Harith Mwapachu akawa Waziri wakati wa Mkapa na Jk
Huyo mjane ni dada yake na akina mwapachu aisee wanafanana mno Rip mzee bomani
 
Juma ana nguvu za ziada. Mpaka leo ana chair board bado. Kudos
 
Juma Mwapachu alikuwa Tanzania one kwny matokeo yake ya kidato cha nne

Baba yao alikuwa Frontliner wakati wa uhuru
Bakari Harith Mwapachu akawa Waziri wakati wa Mkapa na Jk
Baba yao alikufa wakiwa wadogo sana ,nasikia mwalimu nyerere aliwalea kama watoto zake wa kuzaa,wadigo wa zamani walisoma sana sijui what happened latter
 
Back
Top Bottom