Informer
JF-Expert Member
- Jul 29, 2006
- 1,606
- 6,672
Marehemu John Chipaka enzi za uhai wake.
Aliyekuwa Mwenyekiti wa chama cha siasa cha upinzani nchini cha TADEA, John Lifa Chipaka amefariki dunia jana jioni katika Hospitali ya Ibrahim Haji ya jijini Dar es Salaam alipokuwa akitibiwa.
Marehemu Chipaka aliwahi kuwa Katibu wa ANC wakati wa kudai uhuru enzi za Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere.
Aidha, aliwahi kuchukua fomu ya kugombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mwaka 2015 na jina lake kukatwa na Tume ya Uchaguzi kwa kushindwa kutimiza vigezo vilivyowekwa na tume hiyo.
Apumzike kwa amani...
======
Kwa wasiomfahamu:
Miongoni mwa wanasiasa wakongwe wa nchi hii waliopambana na bado wanaendelea kupambana kwenye kambi ya upinzani, ni John Lifa Chipaka.
Chipaka alianza siasa tangu miaka ya 1950 akiwa na chama chake cha ANC. Hata hivyo, chama chake hakikufua dafu kwa TANU iliyoshinda uchaguzi na kuunda Serikali mwaka 1961 chini Mwalimu Julius Nyerere.
Alikuwa akiishi Kimara Temboni jijini Dar es Salaam na alipohojiwa na Mwandishi wa Gazeti la Mwananchi kuhusu hisyoria yake katika siasa, alijibu hivi:
Jibu: Mwaka 1954 baada ya kujiunga na Shirika la Reli la Afrika Mashariki, nilijiunga na Chama cha Wafanyakazi wa Reli (Railways African Union- RAU), baadaye mwaka 1956 hadi 1957 nikawa makamu mwenyekiti wa jimbo la Dar es Salaam. Baada ya hapo nikaacha kazi na kuingia rasmi kwenye siasa.
Mwaka 1957 nilianzisha chama cha Tanganyika’s African Association Congress (ANC) nilichokwenda nacho hadi kwenye uchaguzi wa mwaka 1961. Baada ya hapo nilijiengua na kuunda chama kingine cha People’s Democratic Party, Desemba 7, 1961.
Hata hivyo, chama hicho kilifutwa na sheria namba 45 iliyotungwa kufuatia mkutano mkuu wa TANU mwaka 1963.
Mkutano huo ulifanyika Januari 15, 1963 katika ukumbi wa Anatorglou ambapo wajumbe walipitisha sheria hiyo kwamba nchi itakuwa ya mfumo wa chama kimoja.
Baada ya mkutano huo, ikaundwa tume ya Kawawa (Rashid Mfaume) ambayo ilipita ikiwauliza wanachama wa TANU kama wanautaka mfumo wa vyama vingi (maana Nyerere aliona wao ndiyo Watanganyika halali). Wengi wakasema hawautaki.
Wakati huo Katiba ya TANU ilikuwa na nguvu kuliko hata ya nchi ambayo kwa wakati huo ilikuwa ya mpito.
Swali: Kwa nini hukupenda kuungana na Mwalimu Nyerere katika Serikali yake?
Jibu: Mwalimu Nyerere hakuwa na uzalendo. Sisi tulikuwa tukidai uhuru wa Watanganyika, yeye anadai uhuru wa kila mtu.
Kule India kulikuwa na Jawaharlal Nehru aliyekuwa akidai uhuru wa Wahindi, Kwame Nkrumah alidai uhuru wa Waghana, hata Uingereza ilikuwa ni ya Waingereza tu.
Lakini Nyerere aliingiza hata wasiohusika, kwa mfano katika Serikali yake kulikuwa na Waziri Mhindi aliyeitwa Amir Jamal na mbunge mzungu aliyeitwa Noel Bryceson. Unadhani wale waliacha uraia wa nchi zao?
Swali: Baada ya vyama vya upinzani kufutwa, ukaelekea wapi?
Jibu: Nilirudi kwenye shughuli zangu binafsi, lakini baada ya miaka mitatu, nikaundiwa kesi ya uongo, eti nilitaka kupindua Serikali.
Swali: Hiyo kesi ilikuwaje?
Jibu: Ilikuwa mwezi Oktoba 1969 ambapo tulikamatwa watu saba na kuswekwa rumande kwa makosa ya uhaini ambayo hata hatukuyajua.
Serikali ikatupeleka mahakamani lakini ikakosa sheria ya kututia hatiani. Mwaka 1970 wakaenda Bungeni kutunga sheria ili tukutwe na hatia. Hapo ndipo ikatungwa sheria, lakini ikarejeshwa nyuma, yaani ionekane kuwa ni sheria ya mwaka 1968.
Baada ya sheria kutungwa tukapelekwa mahakamani kushitakiwa rasmi. Mawakili wetu walipambana vikali, lakini mahakama haikujali, mwisho wake tukatiwa hatiani na kuhukumiwa vifungo vya maisha.
Swali: Kwa hiyo ndiyo mkaenda jela moja kwa moja?
Jibu: Hapana tulikata rufaa wakati huo Mahakama ya Rufani ilikuwa ni ya Afrika Mashariki. Tena ilibidi tufanye haraka maana tulisikia Mwalimu Nyerere alikuwa anatunga sheria ya kukataza wenye makosa ya kisiasa kukata rufaa.
Rufaa yetu iliwahi na kesi ikawa ya mwisho kusikilizwa. Baada ya majaji kusikiliza hoja zetu, wawili waliunga mkono hukumu hiyo na mmoja akapinga. Mwishowe tukaachiliwa huru.
Lakini hatukuruhusiwa kutoka, hasa kwa kuwa wakati huo kulikuwa na mlipuko wa magonjwa ya kipindupindu na baadaye kukawa na vita vya Kagera mwaka 1978, kwa hiyo tukaendelea kukaa gerezani hadi mwaka 1980.
Swali: Baada ya kutoka gerezani, ulirudi tena kwenye siasa?
Jibu: Baada ya hapo nilirudi uraiani na kuanzisha kampuni yangu ya biashara hadi mwaka 1992 uliporudishwa mfumo wa vyama vingi.
Hapo nilianzisha chama cha Tadea (Tanzania Democratic Alliance) na kuwa Katibu mkuu wa kwanza. Mwenyekiti alikuwa Flora Kambona, mke wa Oscar Kambona aliyekuwa Waziri wa zamani wakati wa Nyerere.
Swali: Baada ya kuanzisha chama hicho kumekuwa na maendeleo gani katika chaguzi?
Jibu: Uchaguzi wa mwaka 1995 tulisimamisha wagombea ubunge 118, hatukupata hata mmoja, tukapata madiwani wanne. Mwaka 2000 tulisimamisha wagombea ubunge 43 na wagombea madiwani wengi, lakini tulipata madiwani wawili tu. Mwaka 2005 na 2010, hatujaambulia kitu.
Swali: Mmewahi kusimamisha mgombea urais?
Jibu: Ndiyo, mwaka 2005 nilichukua fomu ya kugombea urais, lakini sikufanikiwa kupata wadhamini. Kwa kawaida mgombea urais anatakiwa kupata wadhamini 200 kila mkoa katika mikoa 10. Sasa hao wadhamini walikuwa wakitaka hela ili wanidhamini na mimi sikuwa na fedha.
Swali: Kwa hali hiyo huoni kwamba mwenendo wa chama chako hauridhishi?
Jibu: Kwako ndiyo hauridhishi, lakini mimi naona tunafanya vizuri. Hata kama tunakosa wabunge na madiwani, lakini tunajitahidi kushiriki chaguzi. Uhai wa chama ni kushiriki chaguzi.
Swali: Umekuwa kiongozi wa Tadea muda mrefu, je, wanachama wanapata nafasi ya kugombea nafasi uliyonayo?
Jibu: Mimi nilianza kama Katibu Mkuu wa chama na sasa ni Mwenyekiti. Lakini uelewe kwamba, uongozi wa vyama unapangwa na wenye chama. Hivi karibuni nimealikwa Dodoma kwenye uchaguzi wa CCM, waliochaguliwa pale walipangwa. Unataka tupite huko barabarani na kuokota watu wa kuja kutuongoza? Mwishowe tutaingiza mamluki kwenye chama.
Mwalimu Nyerere mwenyewe alishiriki chaguzi zaidi ya tano na alikuwa akisimama peke yake, hakuna mtu aliyehoji wala kupinga, itakuwa sisi?
Kila chama kinakuwa na utaratibu wake wa kupata viongozi na masharti yanawekwa, ukitaka unayafuata, hutaki basi.
Swali: Unasemaje kuhusu madai kwamba vyama vya siasa visivyo na wabunge vimekuwa vikitumika kama mamluki wa CCM nyakazi za uchaguzi?
Jibu: Hiyo siyo kweli, nisingependa kuvizungumzia vyama vingine, lakini mimi CCM hawawezi hata kunifuata. Tatizo letu ni mfumo mbovu wa uchaguzi na kama utarekebishwa kutakuwa na ushindani wa kweli.
Swali: Umejipangaje kwa uchaguzi wa mwaka 2015?
Jibu: Mambo ya siasa hayaendi hivyo na huu siyo wakati wa kuzungumzia 2015 ni wakati wa kufanya kazi. Nawashangaa watu wanaojipitisha pitisha eti wanataka kugombea urais.
Swali: Ikitokea umechaguliwa kuwa rais, utaendeshaje Serikali yako?
Jibu: Nisingependa kuzungumzia mambo yasiyokuwepo. Mimi ni mzee, nina miaka 83, sina tabia ya kujilimbikizia mali kwa sababu sikuja na mali na wala sitaondoka nazo. Hivyo ndivyo ninavyoishi.
Swali: Unaonaje mfumo huu wa vyama vingi kuelekea mwaka 2015?
Jibu: Mwaka 2015 utakuwa wa mabadiliko makubwa kisiasa. CCM iliyozoeza kupata kura nyingi itazikosa. Lakini sioni chama cha upinzani cha kuirithi CCM. Ukifika mwaka huo kitatokea tu chama mbadala.
KWA TAARIFA YAKO:
Marehemu John Dunstan Lifa Chipaka alizaliwa Desemba 9, 1932 kijiji cha Chiwanda, Nyasa mkoa wa Ruvuma. Mbali na siasa alikuwa akijishughulisha na biashara ambapo hadi mauti yanamkuta, alikuwa Mkurugenzi mtendaji wa kampuni yake ya Exporters Africa Ltd inayojihusisha na usafirishaji wa bidhaa nje.
Marehemu mwaka 1989 alijiunga na Chama cha Wafanyabishara, Viwanda na Kilimo Tanzania (TCCIA) na kuwa mjumbe wa kamati kuu kwa miaka minne. Alishiriki kwa kiasi kikubwa katika uundwaji wa sera za sekta binafsi nchini.
Vilevile alikuwa mwanaharakati tangu wakati wa ukoloni ambapo alijiunga na vyama vya wafanyakazi tangu mwaka 1954.