Hivi karibuni mkutano wa 4 wa wajumbe wote wa kamati kuu ya 20 ya chama cha kikomunisti cha China ulifanyika mjini Beijing, na kupitisha mpango wa 15 wa maendeleo ya miaka mitano (2026-2030). Pamoja na mambo mengine mpango huo una malengo manne makubwa, ambayo ni kuhimiza ongezeko la uchumi na kulifanya liwe endelevu na lenye ubora zaidi, kuhimiza uvumbuzi wa kisayansi, kutimiza malengo ya mambo ya mazingira kwenye kuongeza ufanisi wa matumizi ya nishati, hasa kuongeza matumizi ya nishati endelevu na kufikia uwiano wa kaboni kabla ya mwaka 2030, pamoja na kuhimiza maendeleo ya kijamii na kuwafanya watu wa China waishi maisha bora zaidi.
Kwa wataalam wanaofuatilia mambo ya siasa na uchumi duniani, mipango ya China maendeleo ya miaka mitano mitano si jambo jipya, hasa ikizingatia kuwa mipango hii imekuwa ni sehemu muhimu ya kuhimiza maendeleo ya China tangu mwaka 1953 ilipoanza utaratibu huu, na kasi yake kuongezeka baada ya kuanza kutekeleza sera ya mageuzi ya ufunguaji mlango. Umuhimu wa uchumi cha China duniani na kuongezeka kwa nguvu yake ya ushawishi duniani, vimefanya mpango wa 15 wa maendeleo ya kiuchumi na kijamii wa China, ufuatiliwe zaidi na wanahabari, wasomi na wanasiasa duniani kote.
Mhadhiri mwandamizi katika Idara ya Historia ya Chuo Kikuu cha Dar-es-salaam, Dr. Andrea Kifyasi, ni mmoja wa wanazuoni wanaofuatilia historia ya maendeleo ya China. Mhadhiri huyo ambaye ni mhitimu wa Chuo Kikuu Cha Zhejiang, China ameutaja mpango wa maendeleo wa 15 wa maendeleo ya miaka mitano wa China kuwa ni mpango wa kimapinduzi, unaolenga kuifanya China ijitegemee zaidi, na unaoweza kuwa na mafunzo mengi kwa nchi mbalimbali duniani, hasa nchi za Afrika.
Dr. Kifyasi anasema utaratibu wa kuwa na mipango ya maendeleo si jambo geni kwa nchi nyingi duniani ikiwa ni pamoja na nchi za Afrika, na ametoa mfano wa mpango wa maendeleo wa Tanzania wa mwaka 2050, na mipango kama hiyo ya muda mfupi na muda mrefu inayotekelezwa katika nchi mbalimbali duniani. Lakini ametaja umaalum wa mipango ya maendeleo ya miaka mitano ya China, kuwa ina mambo makubwa mawili ambayo nchi za Afrika zinaweza kujifunza.
Kwanza, ni utekelezaji wa mipango yenyewe. Amesema nchi nyingi za Afrika hazina tatizo kwenye kuandaa mipango ya maendeleo, na kwenye tafiti mbalimbali wanazofanya nchini Tanzania, wanakutana na nyaraka nyingi zenye mipango mazuri ya maendeleo. Tatizo lililopo ni kuwa mipango hiyo haitekelezwi na inabaki kuwa kwenye makabati tu, kwa sababu ya ukosefu wa raslimali za kuitekeleza. Wakati mwingine hata kama kuna fedha za kutekeleza mipango hiyo, yanapotokea mabadiliko ya kiongozi wa nchi au serikali, utekelezaji wa mipango hiyo au vipaumbele kuendana na nia ya kiongozi au serikali mpya. Hali inakuwa ya changamoto zaidi kwenye siasa za ushindani wa vyama, ambapo kama chama tawala kikibadilika, chama kipya kinaweza kuja na sera na mipango tofauti kabisa na ya serikali iliyopita.
Pili, ni kufanya tathmini (evaluation) ya utelekezaji ya mipango yenyewe. Dr. Kifyasi anasema mara nyingi wachina wanapopanga mpango wa maendeleo, kwanza wanafanya tathmini ya utekelezaji wa mpango uliopita na kuangalia utekelezaji wake umefikia hatua gani, na kama kulikuwa na changamoto, zinachambuliwa ili kuangalia zilisababishwa na nini, na kuhakikisha kuwa hazijitokezi kwenye mpango mpya wa maendeleo.
Mhadhiri huyo pia amesema hata kwenye hatua ya kuandaa mpango, wachina pia huwa wanapanga namna ya kupata raslimali kwa kujitegemea, ili kuhakikisha hakuna changamoto za upatikanaji wa raslimali za kutekeleza mpango wenyewe, tofauti na nchi za Afrika ambapo katika baadhi ya mipango, unaweza kusikia wanaopanga bajeti wakisema sehemu ya raslimali fedha zinazotakiwa kutumiwa kwenye utekelezaji wa miradi, inatarajiwa kutoka kwa wahisani, na kama wahisani wasipotoa fedha hizo basi mpango hautekelezwi.
Akiongea kuhusu mchango uliotolea na Rais Xi Jinping wa China kwenye kuandaa mpango wa maendeleo ya miaka mitano wa China, Dr. Kifyasi amesema Rais Xi ni kiongozi anayengalia malengo makubwa na ya mbali ya China. Amesema tangu alipoingia madarakani amekuwa akihimiza kutekeleza mipango ya muda mrefu sio tu kwa maendeleo ya China, bali pia kwa nchi nyingine duniani.