The Sheriff
JF-Expert Member
- Oct 10, 2019
- 747
- 2,112
Mwandishi wa habari Shireen Abu Akleh enzi za uhai wake
Mwandishi wa habari wa Al Jazeera Shireen Abu Akleh (51) ameuawa kwa kupigwa risasi ya kichwa akiwa katika majukumu yake ya kazi wakati akifuatilia uvamizi wa Jeshi la Israel kwenye kambi ya wakimbizi ya Jenin.
Wizara ya Afya ya Palestina imesema Bi. Akleh alipigwa risasi ya kichwa huko Jenin, na kufariki muda mfupi baadaye.
Al Jazeera imevishutumu vikosi vya usalama vya Israel kwa kumlenga na kumuua kwa makusudi Abu Akleh na kuitaka jumuiya ya kimataifa kulaani na kuiwajibisha Israel.
Jeshi la Ulinzi la Israel limesema vikosi vyake vya usalama vimekuwa vikifanya kazi katika eneo hilo "kuwakamata washukiwa wa shughuli za kigaidi," na washukiwa wa Kipalestina.
Mwandishi mwingine wa habari wa Al Jazeera, Al-Samudi, ambaye alikuwa na Abu Akleh wakati alipouawa, alisema hakukuwa na wapiganaji wa Kipalestina katika eneo hilo wakati huo. "Jeshi la Israel lilitupiga risasi," alisema Al-Samudi ambaye pia alipigwa risasi. "Hakukuwa na mpiga risasi wa Kipalestina mahali hapo."
Waziri wa Mambo ya Nje wa Israel, Yair Lapid, alisema kupitia Twitter kwamba serikali yake imejitolea kufanya uchunguzi wa pamoja wa Israel na Palestina, na kuongeza kuwa: "Wanahabari lazima walindwe katika maeneo yenye migogoro na sote tuna jukumu la kupata ukweli."
Akleh aliwahi kufanya kazi na UNRWA, Voice of Palestine Radio, Amman Satellite Channel, Miftah Foundation na Monte Carlo Radio kabla ya kujiunga na Al Jazeera.