[TD="class: content, width: 609"]
Wanazuoni-Allah awarehemu-wameigawa talaka katika mafungu mawili makuu; Talaka Rejea na Talaka Baini. Na hili fungu la pili (Talaka Baini) linagawika pia katika sehemu mbili; Talaka Baini Sughraa na Talaka Baini Kubraa kama utakavyo ona katika ufafanuzi ufuatao:
- TALAKA REJEA: Hii ni ile talaka ambayo isiyo ondosha hukumu za ndoa na wala haiondoshi milki ya mume. Bali uhusiano wa ndoa huendelea kuwepo maadam mtalaka (mke) yungali edani, hapo kunamuelea mume mtaliki kumrejea ndani ya eda hiyo bila ya muafaka kutoka kwa mtalaka wala ndoa mpya. Iwapo hakumrejea hata eda ikamalizika, bila ya shaka atapambanuka nae na wala hamiliki tena kumrejea ila kwa radhi yake (mtalikiwa) na kwa ndoa mpya kwa mujibu wa taratibu zote za kisheria.
Na Talaka Rejea hii hutuka kwa matamko ya talaka yenye kufumbuliza katika kufahamisha talaka, nayo ni yale matamko yote yanayo chimbuka kutokana na kitenzi TWALAQA AMETALIKI. Mithili ya mume kumwambia mkewe: Wewe ni mtalikiwa au nimekutaliki au Wewe ni mwenye talaka au i juu yangu talaka. Na wala kutuka kwa talaka kwa matamshi haya na mfano wake miongoni mwa matamko fumbulizi, hakuhitajii nia. Bali talaka hutuka kwa matamshi hayo bila ya kuwepo haja ya nia kutoka kwa mume, bali lau atadai mtaliki (mume) kwamba yeye hakukusudia talaka, hatokubaliwa wala kusikilizwa. Naam, kama hivi na kwamba Talaka Fumbulizi inakuwa Rejea, iwapo ni talaka ya kwanza au ya pili. Ama ya tatu, hapana rejea baada yake mpaka mwanamke mtaliki aolewe na mume mwingine. Hii ni kwa sababu talaka hiyo ya tatu inampambanua mwanamke na mwanaume huyo Bainuuna Kubraa kama lijulikanavyo hilo kisheria.
- TALAKA BAINI SUGHRAA: Hii ni ile talaka ya kwanza na ya pili ambazo mume huzitoa kwa kutumia mojawapo ya matamko ya Kinaaya Fumbo, pindi atakapo nuia talaka kwa tamko fumbo hili. Tamko Kinaaya la talaka ni pamoja na mume kumwambia mkewe wakati wa ugomvi: Nenda kwenu akikusudia talaka kwa tamko hilo na hutuka talaka hiyo kuwa ni Talaka Baini.
Na hukumu ya aina hii ya talaka ni kwamba talaka hii inaondosha hukumu za ndoa pale pale na unyumba haubakiwi na athari yo yote zaidi ya eda. Kwa hivyo basi, hawawezi kurejeana ila kwa kifungu kipya cha ndoa kwa mujibu wa sheria.
- TALAKA BAINI KUBRAA: Hii pia huitwa kwa Istilahi za Kifiq-hi Talaka Batti Talaka ya kukata nayo ni ile talaka ya tatu. Na hukumu ya talaka hii ni kwamba inaondosha pale pale milki ya ndoa na uhalali vyote pamoja. Mke mtalikiwa hawi halali tena kwa mumewe mtaliki huyu mpaka aolewe na mume mwingine, halafu amuache na eda imalizike. Baada ya yote hayo, ndipo kunamjuzia mume wake huyu wa awali kumuoa upya kwa ndoa ya kisheria na kwa kufuata taratibu zote husika.
Na hapa tunapenda kuitumia fursa hii kuwatahadharisha waume ambao hukithirisha kuacha dhidi ya wayatendayo kinyume na hukumu za sheria. Wenye kuzitumbumkiza nafsi zao na familia zao katika majanga na taabu zinazo kuwa mzigo lemavu juu yao. Sote tunajua ada ya kuacha acha imeenea na kutapanyika katika miji mingi hivi leo kwa sababu ya kuenea kwa ujinga. Hakika mshahara wa ujahili wa majahili hawa na kulinda familia na kuchunga haki za wanandoa, hauwi kwa kutunga sheria/kanuni nyepesi katika masuala binafsi. Wala kwa kufuata/kutumia kauli za baadhi ya maulamaa ziwe ni dhaifu au zina nguvu zinazo tolewa kwa hoja ya kulinda familia. Bali kwanza utengenefu huwa kwa kuzitengeneza nafsi zilizo fisidika na kuwafundisha majahili hawa hukumu za dini. Na kuwakemea wanao chezea hukumu za sheria kwa kuzembea majukumu na amana waliyo pewa na uma.
iv.
Kuhalalikiwa na mtalaka talaka tatu:
Tunacho kimaanisha kwa mas-ala haya, ni kuhalalika mwanamke aliye achwa talaka tatu (Talaka Baini Kubraa) kwa mume wake kwa kwanza. Na uhalali huu hupatikana kwa kuolewa na mume mwingine, kama alivyo sema Allah Taala: NA KAMA AMEMPA TALAKA (ya tatu) BASI SI HALALI KWAKE BAADA YA HAYO MPAKA AOLEWE NA MUME MWENGINE. NA AKIACHWA (na huyo mume mwengine), BASI HAPANA UBAYA KWAO KUREJEANA WAKIONA KUWA WATASHIKAMANA NA MIPAKA YA ALLAH. NA HII NI MIPAKA YA ALLAH ANAYO IBAINISHA KWA WATU WANAO JUA. [2:230]
Hukumu ya kisheria inayo patikana ndani ya aya hii ni kwamba mwanamke aliye achwa Talaka Baini Kubraa (talaka tatu), anahalalika kwa mume wa kwanza. Pale itakapo malizika eda kwa mume wake wa sasa aliye muoa baada ya kuachwa na yule wa kwanza, kisha nae akamtaliki. Na hii ndoa ya pili inayo muhalalisha muachwa wa talaka tatu kwa mume wa awali, ni wajibu makusudio yake yakawa ni dhati ya ndoa na isiwe kutafuta uhalali kama wafanyavyo watu majahili wanao ichezea sheria ya Allah. Ikiwa ndoa hii lengo lake ni kuhalalisha, atapata dhambi aliye kusudia hivyo.
[/TD]