Shujaa ameondoka, akiwa juu jukwaani,
Pambano la uhakika, likiwa bado matatani,
Majahili yenye shoka, mapanga na uhayawani,
Kweli umetokwa roho, Shujaa umelala chini!
Ulipotoka Arusha, Mwanza ukajikita,
Vijana uliwakosha, kwa semi zenye kumeta,
Ujasiri ukawasha, wakawa kama ukuta,
Kweli umetokwa roho, Shujaa umelala chini!
Nilipokuona kwanza, nilidhani ni Samora,
Mawazo yakaangaza, Ukombozi ulo bora,
Zama za mwangaza, Mapambano yenye sura,
Kweli umetokwa roho, Shujaa umelala chini!
Nashindwa kusema sana, rohoni nina huzuni,
Japo ulikwisha nena, tuchukue yako thamani,
Mapambano yenye kina, yatokemeze wahaini,
Wanaodhani Tanzania, ni mali ya vitukuu vyao.