Mwenyekiti wa Kampeni ya Mama Asemewe, Geofrey Kiliba, amewataka wanasiasa wanaopinga juhudi za Rais wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kuacha kupotosha jamii na badala yake kuheshimu juhudi za serikali katika kuleta maendeleo.
Akizungumza na waandishi wa habari leo, Machi 15, 2025, jijini Dar es Salaam, Kiliba amesema Tanzania iko salama na hakuna vitisho vinavyohatarisha amani ya nchi. Ametoa kauli hiyo wakati wa uzinduzi wa Wiki ya Mama, tukio linalotathmini kazi kubwa ya Rais Samia katika miaka minne ya uongozi wake.
Amesisitiza kuwa Rais Samia amefanya mageuzi makubwa katika sekta mbalimbali, hivyo wananchi wanapaswa kuendelea kumuunga mkono kwa ajili ya maendeleo endelevu.
Kiliba pia ameainisha kuwa Machi 19, 2025, ni kumbukumbu muhimu kwa taifa, ikitimiza miaka minne tangu Rais Samia aingie madarakani, akiwa Rais wa kwanza mwanamke wa Tanzania, hatua ambayo ni ya kihistoria na inayopaswa kuenziwa.