Tarehe 10/2/2019 Ngome ya Vijana tulitoa ujumbe kupitia kwenu uliosema ''UVCCM WAMEAMUA KUWA INTERAHAMWE POLISI IWADHIBITI KABLA SISI HATUJAWADHIBITI''.
Juzi zimesikika kauli za Mwenyekiti wa UVCCM Taifa Ndugu Kheri James na Mwenyekiti wa UVCCM Mkoa wa Iringa Ndugu Kennani Kihongozi kuwa Kiongozi wa Chama chetu Ndugu Zitto Kabwe auliwe.
Kauli hii ya UVCCM ilitanguliwa na Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano kuruhusu mjadala usiokuwa na maana na uliojadili waziwazi kumuua Zitto Kabwe bila Spika Job Ndugai kudhibiti hoja hizo za kijinga na zinazodhalilisha Bunge letu tukufu.
Sisi tunajua uvccm ilishakufa zamani waliobaki ni wachumia tumbo ambao wanaongea bila kuangalia athari ya maneno yao kwa mustakabali wa ulinzi, usalama na Amani ya Taifa letu ili waendelee kubebwa kwenye ulaji usiozinagita maslahi ya Taifa letu.
Pamoja na hayo ngome ya vijana tunawataka uvccm waanze, Sisi tutamaliza kwa vitendo kwamaana tumechoka maneno.
Spika wa Bunge ndugu Job Ndugai anajua Tanzania imeingia mikataba ya kimataifa na ile ya kikanda na anajua ukishaingia kwenye mikataba hiyo lazima utii na kuheshimu mikataba hiyo.
CCM inajua ukweli kuwa anayezuia pesa za mkopo wa elimu unaotolewa na Bank ya dunia siyo Zitto Kabwe bali Mwenyekiti wa chama cha mapinduzi, Rais John Pombe Magufuli baada ya kauli yake ya kibaguzi ya kuzuia watoto waliopata ujauzito kutokuendelea na shule baada ya kujifungua kinyume na mikataba ya kimataifa tuliyoingia, kimyume na sera za vyama vyote hapa nchini ikiwamo CCM yenyewe.
Ngome ya vijana inaamini siku Rais John Pombe Magufuli ataifuta kauli yake ile na kuruhusu watoto wanaopata ujauzito kuendelea na masomo baada ya kujifungua Benki ya Dunia itatoa mkopo huo mapema sana.
Ngome ya Vijana tunapinga na kulaani kauli ya Spika Ndugai kuwa Zitto Kabwe alivoiandikia Benki ya Dunia barua alifanya jinai na hivo achunguzwe, tulitegemea Zitto Kabwe apongezwe na Bunge kwa kitendo chake cha kishujaa.
MSIMAMO WETU.
1. Ngome ya vijana tumejiandaa vya kutosha kumlinda na kumuhami Kiongozi wetu dhidi ya uovu wowote. Dalili zozote za uchokozi dhidi ya Kiongozi wetu tutazijibu kwa vitendo.
2. Tunavitaka vyombo vyetu vya ulinzi na usalama visifumbie macho kauli za kumwaga damu zinazotolewa na viongozi wa CCM. Ukimya wa vyombo vya ulinzi na usalama unaonesha waziwazi kuwa wanakibeba Chama cha Mapinduzi.
3. Tunamtaka Msajili wa Vyama vya Siasa kuichukulia hatua CCM kwa kauli hizi za mauaji zinazotolewa na Viongozi na wabunge wa CCM ambazo kwa hakika zinakwenda kinyume na Sheria ya Vyama vya Siasa.