GE2025 My side: Hali jinsi ilivyokuwa tarehe 29. Maandamano, usaliti, uhalifu na mauaji

GE2025 My side: Hali jinsi ilivyokuwa tarehe 29. Maandamano, usaliti, uhalifu na mauaji

Matukio, Taarifa, Habari na Mijadala ya Wananchi WAKATI wa Mchakato wa Uchaguzi Mkuu 2025

Robert Heriel Mtibeli

Platinum Member
Joined
Mar 24, 2018
Posts
40,153
Reaction score
93,069
MY SIDE: HALI JINSI ILIVYOKUWA TAREHE 29. MAANDAMANO, USALITI, UHALIFU NA MAUAJI.

Anaandika, Robert Heriel
Mtibeli.

1. Kulikucha vizuri. Hali ya hewa ya jiji la Dar ilikuwa tulivu.
2. Saa moja unusu nilikuwa nje kijiwe ninapokaaga siku ya jumapili(offday) lakini siku hiyo ya jumatano kutokana na kutangazwa kuwa siku ya mapumziko nilikuwa nje nafurahia hali ya hewa ya asubuhi

3. Asubuhi iliyovaa vazi la kondoo lakini ndani yake kulikuwa na mnyama hatari mwenye kiu ya damu.

4. Hali ya siku za nyuma haikuwa inatabirika hiyo ilinifanya niandae vyakula vya kutosha kama mchele, unga wa ugali, ngano, dagaa, maharage, sukari, mafuta, tambi, na madawa ya kifua, n maumivu. Pampas za watoto, Kwa emergency zozote ambazo zingejitokeza. Upande wa pesa Cash zilikuwa kwa dharura lakini hazikutumika.

5. Daladala chache mojamoja ziliendelea na kazi huku bajaji na bodaboda zikiwa nyingi zaidi.

6. Magari ya kivita hasa kifaru cha kijeshi na magari ya polisi ya Doria yalikuwa yakiendelea na shughuli ya kuhakikisha hakuna kitakachotokea.

7. Mpaka saa mbili na nusu hali ilikuwa shwari kabisa.

8. Saa tatu watu kadhaa walikuwa wamesimama huku na huku barabarani huku wengi wao wakiwa na huzuni ni kwa nini watu hawaandamani lakini hakukuwa na kuaminiana.

9. Majira hayohayo nilishuhudia makundi kwa makundi ya watu hasa wadada wenye umri kati ya miaka 20-30 hivi wakitokea Mbezi ya kimara wakielekea Ubungo. Makundi hayo yalikuwa na watu watano au wanne. Mengine yalikuwa sita na wengine labda wawili wawili.

10. Mwanzoni niliamini wanaenda kazini huko ubungo, Manzese, Magomeni au kariakoo lakini uvaaji wao ambao kwa kiasi kikubwa ulikuwa umefanana ulinijulisha jambo kuwa mambo yatachangamka muda sio mrefu.

11. Walikuwa wamevaa suruali zile za mazoezi, wamevaa kofia, na raba, huku baadhi yao usoni wakiwa wamepaka sijui vitu gani. Hao walikuwa wanawake. Na ndio walikuwa wengi kuliko wanaume kwa uwiano.

12. Punde tukasikia milio ya bunduki na mabomu maeneo ya Kibo. Hapo bado hayo makundi hayajafika Hata Kimara Corner ndio yalikuwa yanamalizikia kimara Bucha na Baruti.

14. Mtandaoni nilipoingia muda huohuo ndio nakutana na habari ya kinachoendelea maeneo ya Kibo.

15. Ilikuwa kama filimbi ya refa uwanjani kwamba mchezo ndio umeanza. Hapo tayari ni saa nne na madakika.

16. Kulikuwa na watu wa aina zaidi ya tatu mpaka muda wa saa nne na nusu kuelekea saa tano; makundi hayo ya watu ni pamoja na;
a) Kundi la waandamanaji ambalo bado lilikuwa linasubiri kuhamasishwa.
b) Kundi la wanaotamani maandamano yafanyike lakini halipo tayari kufanya maandamano.
c) Kundi la watu ambao linataka kuona tukio jinsi litakavyokuwa. (Watazamaji filamu).

Makundi yote haya yalikuwa mengine yamesimama pembezoni mwa barabara, yakishangaa wengine wakijificha kwa kuhofia lolote kutokea.

17. Kilichotokea kibo kilileta athari ya Foleni barabarani na hapo hekaheka ya magari kurudi yalipotokea upande wa Mbezi mwisho ukaanza.

18. Hatimaye Morogoro Road ilikuwa tupu hakuna gari yoyote ya abiria au binafsi wala bajaji iliyokuwa ikipita.

19. Upande wangu nilielewa hiyo inamaanisha jambo gani. Kwenye mtafaruku au mapambano yanayonukia ukiona hali ya ukimya, utupu, utulivu uliopitiliza ujue kifuatacho ITV ni kishindo na shambulizi baya sana ambalo lingeacha athari kubwa.

20. Ghafla nikaona vijana saba. Kutokea upande wa Mbezi mwisho wakiwa katikati ya barabara ya lami wakiimba na kurusha mawe huku na huku wakiimba kwa uchungu na hasira kali. Wimbo wa wenye hasira. Wale vijana kwa kweli hakuna aliyejua walitokea wapi, sura zao kila mtu alikuwa na jibu lililo karibu na jibu la mwenzake. Yakuwa vijana wale ni wabobevu wa kutumia vilevi na madawa hasa Bangi. Sura zao hazikuwa na mzaha hata kidogo.

21. Wakawa wanarusha mawe kwa watazamaji wa filamu waliosimama pembeni ya barabara wakitaka watazamaji nao kushiriki kile wanachokifanya.

22. Kweli baadhi ya watu ambao sasa ni wengi na hatujui walitokea wapi waliosimama pembeni ya barabara wakaunga mkono na kuingia kwenye filamu.

23. Kufumbua na kufumbua natazama nikaona anga limefunikwa na wingu jeusi la moshi. Kituo cha Korogwe kilikuwa kinaungua, kituo cha Kimara mwisho kilikuwa kinaungua.

24. Sasa kulikuwa na makundi manne yaliyojitokeza;
a) Waandamanaji barabarani hawa walikuwa very very aggressive
b) Wanaotaka kuandamana lakini bado wanaona waandamanaji ni wachache. Hawajawashawishi.
c) Watazama filamu ambao tuite hadhira hawa walikuwa wakishangilia kila kundi lililokuwa likipita. Huku wengine wakionyesha kupinga lakini kwa siri kwa kuogopa kuumizwa.
d) wachukua Kamera, video picha.
Hawa walikuwa hawapigwi na waandamanaji.
Walikuwa wanaambiwa wasirekodi na wale wapinga maandamano ambao ni kundi dogo. Kwani waliogopa sura zao kutokea kwenye video huko mitandaoni.

25. Hiyo ilikuwa saa tano. Maeneo mengine kama ubungo, shekilango, na Manzese na Magomeni nako kukawaka.

26. Wakati huo ndio mtandao ukapunguzwa nguvu na kuzimwa kabisa.
Sasa ilikuwa kama mapambano kwenye usiku wenye kiza kinene.

27. Niligundua kuwa uwepo wa mtandao ni kama uwepo wa nuru kwenye vita. Nuru ya kuwamulikia waandamanaji.

28. Kuzimwa mtandao kulipelekea jambo jingine kujitokeza. Nalo ni ubize wa bodaboda..
Bodaboda zilizobeba vijana watatu mpaka wanne ambao ni waandamanaji ziliongezeka maradufu zikipita service road au vichochoroni huko kutoa taarifa kutoka pointi A kwenda B.
Huku wengi wakitafuta wapi kuna maandamano yaliyokolea.

29. Kupigiana simu kwa waandamanaji kuliongezeka hasa wale waendeshaji wa bodaboda waliokuwa wakifanya movement.

30. Mpaka saa tano unusu Askari ni kama walikuwa hawajachukuli hali hiyo serious sana. Hivyo hapakuwa na hekaheka za nguvu za askari.

31. Vituo vyote vya mwendokasi barabara ya Morogoro vilikuwa asilimia 90 vimechomwa. Kituo cha mwisho kuchomwa kilikuwa Kimara Bucha ambacho hata hivyo kutokana na uhaba wa mafuta ya petroli hakikuungua vizuri.

32. Waandamanaji wengi hawakuwa wanatokea sehemu maandamano yalipo.
Mfano waandamanaji wengi wa barabara ya Morogoro road wengi walitokea njia ya maji chumvi, tabata, Magomeni na maeneo mengine. Huku waandamanaji wa maeneo ya mbezi ya kimara wakiwa walienda Ubungo shekilango, Magomeni na Manzese.
Sasa nilielewa kwa nini ile asubuhi kulikuwa na movement ya wanaotoka mbezi kuelekea mjini , huku bodaboda zikitokea vichochoroni kutokea maeneo kusikojulikana.

33. Mbinu hii ilifanya kazi kwa sababu waandamanaji wa eneo husika ingekuwa ngumu kuandamana kwa kuogopa kuripotiwa na mamluki au viongozi wa mtaa.

34. Hii ni kusema, viongozi wengi wa mtaa walishuhudia idadi kubwa ya vijana wageni ambao ni unknown.

35. Majira ya saa sita tayari makabiliano makali baina ya waandamanaji na askari yalianza kuripotiwa huku nguvu kubwa ikipelekwa maeneo ya kuanzia Manzese Bakhressa kuelekea Magomeni.

36. Nataka niwaambie kulikuwa na mvutano baina ya waliokuwa kwenye maandamano.
Wahusika waliokuwa kwenye maandamano ni kama ifuatavyo;
a) Waandamanaji waliotaka njia salama bia kuharibu mali wala kufanya uhalifu.
b) waandamanaji wahalifu ambao wao walikuwa na lengo la kujipatia mali za wizi.
Wengine kuharibu miundombinu ya serikali.
Waandamanaji wenye hasira na kisasi kwa walioiunga CCM mitandaoni hawa walienda baadhi ya maeneo waliyoambiwa yanamilikiwa na waunga mkono ccm.

c) Wachambuzi, waandishi, watunzi, wanahabari ambao nao walitaka kushuhudia kila kitu nao walikuwa sehemu ya waandamanaji.

d) Askari kanzu, makachero, na majasusi ambao kazi yao ilikuwa wanajifanya waandamanaji lakini walikuwa wakitoa ripoti kwa njia ya mawasiliano ya siri kwenda kwa Askari kwamba waandamanaji wapo njia fulani, wako wengi kiasi fulani, wamebeba silaha au wana means kadhaa. Hawa nao walikuwepo.

37. Palikuwa na kizuizi katikati ya Kimara Baruti na Corner. Niliona Askari watano wakiwa na silaha wakirusha mabomu ya machozi, bunduki na fataki.

38. Watu kadhaa waliuawa. Wengine kujeruhiwa kwa kupigwa miguuni na sehemu mbalimbali za mwilini.

39. Hiyo ni saa sita unusu.
40. Nilibahatika kwenda Ubungo kwa njia za panya. Kwani hali ilianza kuwa mbaya. Kutokana na baadhi ya askari nao kuuawa. Hivyo hapakuwa na utani tena. Kila mmoja alikuwa akitaka kujiokoa. Huku sisi wengine tukitaka kushuhudia kwa macho yetu historia hii yenye kusisimua, kuumiza, kutia hofu na kusikitisha.

41. Mara kwa mara familia yangu, mke wangu alikuwa akinipigia simu akinitaka nirudi nyumbani. Huku nami nikimpa maelekezo kuwa asitoke nje, avunge geti na mlango, kisha akae sehemu ambayo haliangaliani na dirisha yeye na watoto.

42. Nilikuambia nyumba yetu ipo barabarani kabisa. Inauzio lakini geti lake lilivunjwa na kidanga na kimbiakimbia ya waandamanaji na askari.

43. Nilitokea ubungo kwenye soko la kimataifa la wachina, pale kulikuwa na ulinzi mkali wa jeshi lenyewe(JW), hawakuruhusu watu wapite eneo lile ingawaje hekaheka zilikuwepo. Eneo lile halikudhurika.

44. Sasa ni saa saba mchana, mji mzima ulikuwa kwenye machafuko hasa maeneo ya barabara kuu. Mikoa mingine kama Mwanza, Arusha, bado kulikuwa kimya. Mpaka muda huo.

45. Maeneo niliyopita mengi vituo vya kura viliunguzwa. Hasa Morogoro road.

46. Nilifika shekilango, pale kuanzia Big brother mpaka Manzese Bakhressa kulikuwa kumechangamka sana.
Hivyo njia hiyo niliona haiko salama sana na tayari nilianza kukutana na watu waliopigwa risasi huku ambulance zikiwa busy sana.

47. Nilipita njia ya shekilango road inayotokea SINZA. Huku kulikuwa kumepoa askari na magari yao ndio yalikuwa yako busy yakienda na mengine yakirudi. Ilikuwa kama vita.

48. Nikatokea Sinza Uzuri. Huku pia kulikuwa kimya huku magari ya polisi na bodaboda chache zilizobeba vijana zikiwa wanguwangu kwa kukimbizana.

49. Nikatokea Manzese Bakhressa, huku ndio kulikuwa pamoto, nilishindwa kutokea barabarani kwani kulikuwa na vita vikali na milio ya risasi zilishamiri.

50. Familia yangu ikanitishia. Walikuwa na hofu kubwa. Huku mimi nikiwaambia wao wajichunge zaidi kwa sababu kwenye hekaheka hizi. Niligundua kuwa wengi waliozurika ni wale waliojiona wako salama na wapo nyumbani. Na wale waliokuwa front hasa dakika za mapema wakati mchezo unaanza.

51. Nikarudi lakini majira ya saa nane unusu hiyo. Njia zote hazikuwa zinapitika tena.

52. Barabara zilikuwa zimejaa moto na mawe.
53. Kuna jambo ambalo niligundua ambalo najua waandamanaji wengi hawakukubali ukweli hata nilipowagusia. Nikaona niwaache tuu.

54. Watanzania wengi hasa waandamanaji waliamini jeshi la wananchi (JW) lipo upande wao. Lakini tathmini yangu ilinipa utata baada ya kuona jambo lifuatalo;

55. Iko hivi, waandamanaji huweka vizuizi barabarani na kuchoma barabara ili kuzuia magari ya polisi yasiweze kufanya movement yatakavyo. Hii inawasaidia sana waandamanaji kuendelea na shughuli zao.

56. Maandamano na vurugu kwa sehemu kubwa zilidhibitiwa kwa sababu barabara zilikuwa nyeupe. Hivyo magari ya polisi yalikuwa yakienda yatakavyo kwa uharaka na kufikia watu kirahisi. Hapa naongea kama mchambuzi na niliyeshuhudia kilichokuwa kinaendelea.

57. Wakati vizuizi vilivyowekwa na waandamanaji vikiwepo barabarani kulikuwepo na magari ya kijeshi(JW) na wanajeshi kadhaa waliovalia nguo za kijeshi. Wanakuja na gari lao nawaona waandamanaji wanashangilia na wengine kupanda kwenye yale magari. Unasikia sauti ya mjeshi kwenye kipaza sauti kikiongea kwa lugha ya kijeshi" tafadhali tafadhali! Wananchi msizuie barabara, fungueni barabara kwani kuna watumiaji wengine"

58. Hapo waandamanaji bila ya kujua maana ya maneno hayo. Wanafungua barabara na kutoa vile vizuizi. Wanaenda kwenye kizuizi kingine hivyo hivyo mpaka wanafika kimara mwisho wanarudi upande wa pili kuelekea ubungo.

59. Kwa jicho la kiuchunguzi, kiutunzi, kijasusi na mambo ya kimedani akili yangu iiniambia sio muda magari ya polisi yenye polisi yatakuja sio muda. Na yake magari ya maji washa.

60. Kweli! Hazipitagi dakika tatu yale magari ya polisi yanatokea kwa mbali muda huu yanakuja bila ukinzani wala kizuizi barabarani kwani viliondolewa. Watu waliokuwa barabarani wakiandamana wanaanza kukimbia kama mizimu iliyokoswakoswa kuingia jehanamu.

61. Kwa vile magari hayana kizuizi yanawafikia kwa urahisi sana na kuwapa dozi kadiri ya utashi wa askari. Wakiamua kumwaga maji wanamwaga.

60. Panakuwa peupe watu wamekimbia mitaani. Kisha yale magari nayo yanaondoka. Panakuwa kimya kwa muda kisha watu wanarudi barabarani. Wakati huu ni pembeni sio tena katikati ya barabara. Hali inakuwa kama asubuhi majira ya saa 3-4.

61. Nikajaribu kudodosa kwa watu kujua uelewa na mtazamo wao kuhusu jeshi la wananchi (JW) nikagundua wanaimani kubwa. Maskini! Nilipowagusia kidogo kuhusu lile gari la JW kuwaambia wasafishe njia nikagundua bado wanaimani na hawaelewi chochote. Kwa vile kazi yangu haikuwa kuwafundisha au kuwaeleza mambo ya kimedani nikaona haina maana. Nikawaacha.

62. Saa tisa unusu naenda kula.
63. Hofu bado ni kubwa sana eneo letu lakini bado ubishi uliendelea kuwepo.

64. Baada ya kula nilirudi tena kuchukua ripoti.

65. Kundi la mwisho ambalo sasa hili lilikuwa kubwa kuliko yote. Majira ya saa kumi unusu hivi lilikuwa likitokea Mbezi. Walikuwa watu wengi sana. Wengi sana. Linaimba! Linaimba! Linalia! Linalia! Linapiga kelele! Nakupaza sauti zao.

66. Kundi hili lilifanya makosa ya kiufundi yafuatayo;
a) lilitakiwa kila lilipopita lichukue mawe au vizuizi vikubwa liweke barabarani kwani tayari hapakuwa na vizuizi kwani viliondolewa.
Hii ingewasaidia pakubwa wakati wa kukimbia na kujihami ili wasifikiwe kirahisi na yale magari kwani kwa wakati ule hakuna askari ambaye alitaka kushuka juu ya gari na mji mzima ulikuwa umechangamka.

b) Kuvamia maeneo na kufanya uhalifu na uharibifu.
Kundi hili lilipofika kimara Baruti kuna Kituo cha mafuta pale na kisuper market huku mbele kidogo barabarani katikati ya Kituo cha Corner na Baruti lilikuwepo gari la askari na askari watano hivi.

Waaandamanaji walijikuta wakigawanyika makundi makubwa mawili huku wahusika wakiwa walewale niliowataja kule juu kuwa ni waandamanaji amani, waandamanaji wahalifu, waandamanaji wachukua habari, waandishi, watoa ripoti, na waandamanaji makachero, majasusi na askari kanzu.

Makundi mawili yakawa ni waandamanaji wahalifu na waandamanaji wanaotaka amani.

b.i) Wakasema tuvamie kituo cha mafuta hapo wapo Baruti. Wengine wanasema hapana jamani tusifanye hivyo. Haitakuwa na maana sasa. Huo ni uhalifu. Wengine tupo kimya hatuzungumzii chochote tunatembea tuu.

b.ii) Tatizo wale viongozi waliokuwa mbele wengi wao walikuwa wakorofi, wenye hasira kali, na wengi wao wanatumia madawa kama bangi. Tulipofika pale natazama kwa ghafla risasi zikalia sana. Nikainama chini huku na roll na mikono nikikazana huku wengine wakikimbia kurudi upande wa mbezi. Nilipoona mambo yanakuwa magumu na nitakuwa mbele kabisa hapo nikaamka kwa upesi na kukimbia nikiwa nimeinama mpaka kwenye ngoma ya barabara na kujitupa service road huku risasi na milio ya mabomu vikiwa vimechachamaa. Sasa nillikuwa nimekaribia kituo cha baruti na mambo yalikuwa magumu sana. Nikisema niende na barabara itakuwa rahisi kukamatwa au kupigwa risasi. Upande nilipo kuna yadi ya magari ambayo inauzio. Pembeni yake kuna ngema ya zege kwa wanaojua eneo hilo mtaelewa.

Naona watu wanapanda kwenye ile ngema. Sasa ukiwa kwa pale juu ni rahisi sana kwa wale askari waliopo kwenye gari zao kukupiga risasi ni kama umewarahisishia kazi.

b.iii) Nikasema pale sitatoboa. Bado wengine wananipita lakini wanakimbia kimbia bila hesabu. Mimi muda huo nimelala chini karibu na dimbwi la matope yenye maji kumbuka jana yake mvua ilikuwa imenyesha.

b.iv) Lile gari la askari lilikuwa limeshafika usawa wa kituo cha mafuta. Kama mita sitini kutokea nilipo. Hapa nitapigwa lakini wale askari nao walikuwa wanapata upinzani kutokea kwa watusha mawe, chupa na rungu. So mara nyingi walikuwa wanashambulia eneo yanapotokea mashambulizi.

b.v) nikainuka upesi baada ya kuona kigenge na nyuma yake kuna mbuyu nikajificha hapo nikiwa nimeinama. Sasa natazama filamu nikiwa hapo. Huku macho yangu yakiwa yanahangaika huku na huku nikiwa siachi kuangalia walipo askari nisije pigwa risasi.

b.vi) simu inaita, alikuwa mke wangu. Namwambia atulie ndani na akae nilipomuelekeza. Kutokea Baruti na korogwe sio mbali sana. Anasikia sauti ya milioni kama ipo karibu kabisa na mimi analia. Rudi nyumbani. Rudi! Namwambia nakuja. Kisha nakata simu.

67. Nasikia kutoka barabarani kwa wale waandamanaji waliokuwa barabarani wamelala chini huku wengine wakirusha.
Nikasikia, wameishiwa wanabadilisha risasi.

68. Watu waliokuwa mtaani na barabarani wakaanza kuwakimbiza lile gari la polisi likarudi nyuma nyuma kisha kukatisha na kurudi mpaka kituo cha Corner.
Hapo ndipo wale waandamanaji wahalifu walioikimbilia kile kituo cha mafuta huku wengine wakiwalaumu msifanye hivyo. Kila mtu anaongea lake. Twende Ubungo jamani haraka wenzetu wanatusubiri Ubungo na wengine wapo Magomeni. Saa kumi na moja hiyo.

69. Nikaona waliobeba mitungi mikubwa kwa midogo ya gesi, waliiba kila kitu huku bodaboda zikisaidia kubeba vitu hivyo. Wanawake kwa wanaume. Kisha wakawa wanaipiga ile mitungi chini ili ilipuke.

70. Kuona hivyo nikajua nini kitafuata. Nilijua mara hii wale askari wakija watakuja wakiwa wengi na watakuwa wanakuja kufanya kweli.

71. Kwa upole nikaondoka kumbe sikuwa pekeangu.
Walikuwepo wengi waliokuwa wakirudi uelekeo wa mbezi.

72. Kila kundi lililokuwa linarudi nililidodosa kwa nini linarudi.
Wengi walikuwa wakilalamika kwa kitendo cha wengine kuvamia na kuiba.
Oooh! Zile ni mali za watanzania wenzetu. Badala tuandamane kupinga serikali na Samia wao wanaharibu mali za watanzania wenzao. Hayo yalikuwa maoni ya waliokuwa wanarudi.

73. Ni kwamba sasa waandamanaji walikuwa wamegawanyika waziwazi. Huku uwezekano wa kuendelea kwa maandamano ulikuwa mdogo kwani zile interest na goals zilianza kupishana sio moyoni tena bali waziwazi dhahiri shahiri.

74. Niliona vidada virembo sana hili kundi lilinivutia nikaharakisha ili nitake kujua wadada wazuri kama wale nini kimewaleta katika mazingira yale hatari na kuhatarisha maisha yao.
Niligundua sio tuu warembo bali hata shule wameenda, niligundua baadhi yao wana watoto na wameolewa, na baadhi sio njaa kali yaani wana maisha ya kubadilisha mboga na kuendesha magari.

75. Wao wanasema wametoka kuandamana kwa sababu ya kuungana na watanzania wengine kudai haki na usawa katika uchaguzi pia katiba mpya.
Lakini kilichowakatisha tamaa ni wahalifu kuvunja na kuchoma kituo cha mafuta na kuiba maduka ya vinywaji yaliyokuwa na vioo tuu. Wanasema wao wenyewe wana maduka sinza na kariakoo hivyo wanajua maumivu ya kuharibiwa biashara.

76. Nilifika nyumbani mwendo wa dakika 15 tuu tayari ni saa kumi na moja unusu.
Na hapo ndipo nikasikia mabomu, fataki na risasi kutokea baruti huku yale magari ya kiaskari yakiwa yameongezeka zaidi. Hawakuwa na mzaha tena.

77. Nilimkuta mke wangu na watoto wanalia wanadhani ati nimeshakufa. Yaani ukitoka tuu wakisikia bomu wanajua niliyepigwa ni mimi. Yaani booom baam, fyyuuu taa taa taa. Dadeki!

78. Mchezo huu kuelekea kumi na mbili haukuwa wa masikhara hata kidogo. Na somo lilikuwa limeeleweka kikamilifu kwani askari hawakuonyesha utani tena.
Hata fataki hawakutumia tena. Milio ya mambo ya machozi na risasi ndio ilitawala.

79. Saa kumi na mbili barabara zote hazikuwa na mtu hata mmoja isipokuwa wale wachache ambao hawakuwa kwenye maandamano ambao hawajui seriousness iliyopo na wengi walikutana na moto wa chuma.

80. Ni kweli wahalifu wengi walipoiba walipotea moja kwa moja na hawakuonekana tena.

81. Watu wachache waliosimama pembeni ya barabara ni wale waliokuwa wanataka kutazama kuona nini kinaendelea. Na hawa nao waliumia wengi sana.

82. Kati yao wengine walikuwa hawaamini kwamba kweli maandamano yamedhibitiwa kwani walitamani yaendelea kwani malengo yao bado yalikuwa hata nusu hayajafikiwa.

83. Saa moja usiku eneo letu lilikuwa giza kwani umeme ulikatika baada ya kituo cha mwendo kasi kuunguzwa.
Na bado watu wachache waliokuwa wanaranda randana pikipiki wakitafuta yalipo maandamano walikuwa wakiendelea kupiga doria chocho kwa chocho na wakitokea barabara wakikuta watu nao wanasimama ili pembeni ili watu wajae.

84. Mimi somo nililielewa hivyo nilikuwa ndani ya fensi ya nyumba ninayokaa nikitazama. Nilijua nini kinaenda kujiri. Giza likiingia.

85. Ghafla magari ya polisi yaliwasili na wale watu waliosimama wakawa wankimbia kuingia mtaani. Polisi wakirusha mabomu ya machozi na risasi.
Sasa wamekimbia lakini Kwa haraka haraka polisi walijua. Huenda nyumba zetu za barabarani ndiko wanakojificha. *****!

86. Jamani tulinyooshwa! Risasi zilikoma lakini mabomu ya machozi yalifuatia na fataki zilirindima. Tulirushiwa mabomu kama yote. Mengine yanaangukia juu ya bati,, yapiga dirisha, basi moshi kama wote.
Watoto ni kulia. Macho kuwasha, kukohoa na milio ya hofu vilitawala. Hiyo ni saa moja unusu kuelekea saa mbili usiku.
Kufikia saa mbili kulitulia. Milio ya risasi mara moja moja ndio inasikika.

87. Tunawasha taa za sola. Tunakula. Tunaomba tunalala. Nje milio ya risasi kwa mbali inasikika. Siku ya tarehe 29 inaishia kwa mtindo huo kwa kishindo kikuu.

88. Hakuna mtaani kwetu aliyeuwa wala kupigwa risasi kwa tarehe 29. Wote tulikuwa salama.

Kimbembe tarehe 30. Siku inayofuata ambayo ilianza kwa hekaheka tofauti na siku ya tarehe 29 iliyoanza kwa upole wa hila, amani ya mtego, na utulivu wa kijoka.

89. Tutaendelea na stori yetu. Kwa tarehe inayofuata tarehe 30.
Je wale walioingia mtaani ni kina nani? Kesho yake tarehe 30 waliingia askari wawili nyumbani kwetu. Wakiwa wamevaa nguo za kiaskari wamebeba silaha za moto.

90. Baada ya stori. Niwaombe jambo moja. Tupunguze hasira, mihemko, chuki, na tuandae mazingira ya kuwekana sawa. Tuache ujeuri na kiburi. Kutunishiana misuli hakutatufikisha popote.

91. Kulaumiana. Na kunyoosheana vidole huku kila mmoja akitaka kumwona mwingine mbaya kutatupeleka kubaya zaidi.

92. Mambo haya yanatokea kwa sababu. Yasiwe sehemu ya kuongeza chuki na utengano bali tuyatumie kama fursa ya kuona umuhimu wa kuwa pamoja, kutenda haki na kupendana.

93. Ni busara na hekima kila mtu ajishushe ajione anahusika kwa namna moja ama nyingine kwa hiki kilichotokea.

94. Viongozi wakuu wawe mfano kujishusha na kuomba msamaha kwa kilichotokea kwani hawatapungukiwa na chochote. Kusema "Naomba msamaha" ni moja ya kiashiria kwa kiongozi thabiti.
Sio kuonyesha kwamba wewe ni dhaifu na mbaya kuliko wengine.
Bali kuonyesha tumaini, faraja na kutaka kwaa dhati umoja na mshikamano kama taifa.

95. Vitisho havitatufikisha pazuri. Vitisho ni muhimu la lazima kwa wahalifu na watenda maovu lakini kutisha watu wanaoamini wameonewa, kudhulumiwa na wengine ndugu zao kuuawa sio suluhisho na haina mustakabali mzuri

96. Ni kweli wapo watu wengi wameuawa hawakuwepo kwenye maaandamano. Hivyo ni muhimu kuliona hilo.
Pia wapo waandamanaji wengi ambao hawakuwa wahalifu na ameuawa. Hilo pia ni muhimu kuliona.

97. Ni muhimu kujali mambo hayo kwani yanagusa maisha na familia za watu moja kwa moja.

98. Ni muhimu maswala ya utekaji na mauaji yaliyokuwa yanatokea vikawa kipaombele kuyazuia kwani ni moja ya hoja za waandamanaji. Na tumeshaona sio suluhisho.

99. Ni rahisi kuwazuia wahalifu kimabavu lakini ni ngumu kuzuia kimabavu watu wanaoamini wanatetea haki zao fulani fulani. Haki haizuiwi kimabavu.

100. Upendo hata upendo bandia ndio njia pekee ya kuleta utulivu ndani ya familia au taifa. Lakini mabavu kamwe hayawezi kudumu kumuongoza mwanadamu iwe kwa ngazi ya familia au taifa. Yaani Baba hata uwe mbabe vipi na utumie mabavu kuongoza mkeo na watoto tambua wao nao wanatafuta namna ya kukunyoosha. Na familia bora na imara haindeshwi kimabavu bali kwa upendo na masikilizano

Acha nipumzike sasa!

Taikonmaster
Kwa sasa Dar es salaam
 
Umerudi tena na makala yako ndefu baada ya maandamano makubwa kuwahi kutokea nchini kufanikiwa!?,si uliandika makala ndefu kama hii ukielezea kwanini hakuwezi kuwa na maandamano Tanzania!?.., hii makala inafuta Ile ya tarehe 28!?,umeomba samahani kwa makala ya uongo ya wiki iliyopita!?,wakati mwingine mnajipaga umuhimu msiokuwa nao. Kukaa kimya nayo ni busara tosha.
 
Umerudi tena na makala yako ndefu baada ya maandamano makubwa kuwahi kutokea nchini kufanikiwa!?,si uliandika makala ndefu kama hii ukielezea kwanini hakuwezi kuwa na maandamano Tanzania!?.., hii makala inafuta Ile ya tarehe 28!?,umeomba samahani kwa makala ya uongo ya wiki iliyopita!?,wakati mwingine mnajipaga umuhimu msiokuwa nao. Kukaa kimya nayo ni busara tosha.
Machawa kama Lucha funaku na nyutro uchwara kama hawa na wengine kama adriz Ritz ni mojawapo ya janga kubwa kwa nchi yetu.
 
Umerudi tena na makala yako ndefu baada ya maandamano makubwa kuwahi kutokea nchini kufanikiwa!?,si uliandika makala ndefu kama hii ukielezea kwanini hakuwezi kuwa na maandamano Tanzania!?.., hii makala inafuta Ile ya tarehe 28!?,umeomba samahani kwa makala ya uongo ya wiki iliyopita!?,wakati mwingine mnajipaga umuhimu msiokuwa nao. Kukaa kimya nayo ni busara tosha.

Tarehe 30 watu kama nyie ndio mlishushughulikiwa vilivyo.

Mnachochea watu alafu mnawasaliti hamtoki.

Wengi wanasema waliuawa nyumbani. Swali linakuja, wenzenu wanaandamana kwani nini nyie mpo nyumbani amejificha.

Baada ya maandamano kufeli hali ndio ilikuwa ngumu hasa kwa ambao hawakutoka.
Mpaka saa saba saa nane mchana hapakuwa na mauaji mengi.
 
Keyboard worrior...unachochea maandamano halafu hautoki hiyo ni tabia ya kinafiki.
Mnawadanganya watoto wa watu wamepata majanga halafu nyie mnabaki kusambaza picha.

Hawa walijificha ndani alafu wanataka watumiwe picha waone kilichotokea au wanataka serikali iwashe mitandao ili wapate umbeya wakati wenzao wakiwa field.
 
Hawa walijificha ndani alafu wanataka watumiwe picha waone kilichotokea au wanataka serikali iwashe mitandao ili wapate umbeya wakati wenzao wakiwa field.
Roho ya selfishness kabisa.
Wanamanipulate watoto wa watu na kuwaingiza matatizoni
 
Back
Top Bottom