"Tatizo kubwa la nchi, ukishavunja haki, ukishavunja misingi ya haki, hutapata amani na vyama hivi vyote sasa hivi kwa kasoro yao vimejitumbukiza katika kuvunja haki, vinakula rushwa"
Mzee Butiku amepinga kauli zinazodai kuwa mfumo wa siasa za vyama vingi ndio chanzo cha vurugu, akifafanua kuwa katiba na sheria zilikabidhi vyama vya siasa jukumu la kuongoza na kusimamia siasa za nchi. Tatizo lililopo sasa ni vyama hivyo kuweka mbele migogoro badala ya kuwatumikia wananchi.
"Nchi hii tumemkabidhi nani kuiongoza kikatiba? Vyama vya siasa! Vyama vya siasa ndivyo vinasimamia siasa ya nchi hii kwa katiba na sheria. Vyama hivi leo vinagombana tu."
Mzee Butiku ameeleza kuwa hata Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambacho ndicho kilichojenga nchi na kuweka Katiba chini ya uongozi wa Mwalimu Julius Nyerere kimekuwa kikivunja miiko na misingi hiyo, jambo ambalo ameshawahi kuwaonya mara kadhaa.
"Lakini wanavunja miiko, Wote CCM wanavunja, na nimeshawambia. CCM chama kikongwe ndicho kilichojenga nchi hii. Katiba ya nchi hii imewekwa na CCM na Mwalimu."- Amesema Mzee Butiku